Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri, Mheshimiwa Dunstan Kitandula, Katibu Mkuu Dkt. Hassan A. Said, Naibu Katibu Mkuu (Maliasili) Ndugu Benedict M. Wakulyamba - CP, na Ndugu Nkoba E. Mabula (Utalii), wataalam wa Wizara, taasisi zilizo chini ya Wizara na wadau wa maendeleo kwa mchango wao mkubwa kwenye kujuza Sekta za Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye ni nini kifanyike ili kukuza Sekta ya Utalii hapa Tanzania.  Utalii, ni kitendo cha kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa lengo la kujiburudisha au kujifunza. Tanzania ni moja kati ya nchi zenye vivutio vingi vya utalii hapa duniani na ni nchi ya tatu Barani Afrika kwa nchi zenye utalii mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii hapa Tanzania umekuwa na faida nyingi kwa Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira, kuongeza kipato cha Taifa, kuleta fedha za kigeni na kutangaza utamaduni wa nchi yetu Tanzania. Utalii peke yake huchangia karibu 17.2% katika pato la Taifa na huko Zanzibar ni 30%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na faida zote, Sekta ya Utalii nchini mwetu imekua ni sekta inayosuasua kwani inaingiza idadi ndogo ya watalii kinyume na matarajio. Tanzania ni nchi yenye vivutio vingi na tukijipanga vizuri tunaweze kuingiza watalii millioni 10 kwa mwaka wakati kwa sasa bajeti hii ikisomwa tumeshaingiza watalii 5,360,247 (wa ndani - 3,218,352 na wa nje 2,141,885) na lengo letu kwa mwaka 2025 ilikuwa watalii 5,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya nyuma, watalii wa kimataifa walioingia nchini waliongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi 2,141,895 mwaka 2024 sawa na ongezeko la 132.24%. Ili kufikia lengo letu la kuongeza watalii wa nje, ni lazima Tanzania tujitathmini wenyewe na kufanya mabadiliko ili kukuza Sekta ya Utalii na kuingiza watalii wengi watakaolinufaisha Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha Sekta ya Utalii Tanzania, yafuatayo ni mambo muhimu ya kufanya ili kukuza sekta yetu hii: -
(i)	Kuweka mkazo kwenye kutangaza masoko ya utalii na kuhamasishaji watalii kutembelea nchi yetu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tumejionea umuhimu wa kutangaza soko letu la utalii kupitia filamu za The Royal Tour na Amazing Tanzania zilizotengenezwa na kumshirikisha Rais wetu kuonesha vivutio vya utalii katika Taifa letu. Filamu hizi zimekuwa mkombozi mkubwa katika Sekta ya Utalii kwani watalii wameongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi 2,141,895 mwaka 2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi ni muhimu kufanya kampeni za matangazo kwenye vyombo vya habari vya kimataifa na majukwaa ya kidijitali kama vile mitandao ya kijamii, tovuti za utalii na blogu za usafiri kuelezea vitu vya kitalii tulivyojaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kutangaza masoko yetu ya utalii, nchi ijizatiti kushiriki kwenye maonesho ya kimataifa ya utalii ili kuongeza ufahamu na kuvutia watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ushiriki wetu kwenye maonesho ya kitalii ya kimataifa kama yale ya Afrika Mashariki (East African Tourism Expo), Internationale Tourismus-Boerse (ITB) Berlin, World Travel Market (WMT) London, Group Leisure & Travel Show (GLT) ya Uingereza, FESPO ya Zurich, World Tourism Forum ya Lucerne, Stockholm Luxury Travel Fair, Fitur International Tourism Trade Fair ya Madrid, Tourisma & Caravaning ya Magdeburg na International French Travel Market (IFTM). Maonesho haya ni muhimu kushiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la utalii linaweza kutangazwa hapa nchini kwa kuandaa maonesho ya ndani na kimataifa yanayolenga kuonesha utajiri wa vivutio vya utalii vya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, soko letu la utalii linaweza kufanikiwa ikiwa tutawatumia baadhi ya watu maarufu katika jamii duniani kwenye kushawishi na kuvutia watalii kuja kutembelea mbuga zetu au kupanda Mlima Kilimanjaro. Kwa mfano, wachezaji maarufu wa mpira duniani kama Ronaldo au Lionel Mesi au watu maarufu wenye ushawishi duniani kama Barack Obama, Serena Williams, Bill Gates, Rashida Jones, Patrice Motsepe na wengine wanaojulikana wanaweza kutumika kutangaza soko letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabalozi wetu wanaweza kutumika na kusaidia kutangaza utalii wetu. Hawa wanatakiwa kupewa elimu ya utalii na mbinu madhubuti za kuutangaza utalii wa nchi yetu popote watakapokuwepo. Wote hawa wanaweza kutumia mitandao kuonesha vitu vya kitalii tulivyonavyo Tanzania.
(ii)	Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii wetu utaboreka sana ikiwa Serikali yetu itaweka mkazo kwenye kutengeneza na kuboresha miundombinu ya usafirishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu kama vile barabara ni muhimu sana katika Sekta ya Utalii. Barabara hutumika kuwapeleka watalii katika maeneo ya utalii. Kwa sasa barabara zetu nyingi zinazopeleka watalii site ni mbovu sana kiasi cha kuumiza watalii wakati wa safari kuelekea katika vituo vya utalii. Kutokana na ubovu wa barabara, watalii huishia kuchoka sana baada ya safari. Jambo hili hupelekea kuwakatisha tamaa na kupunguza idadi ya watalii, kwani wengi hawajazoea barabara mbovu kama za kwetu. Ikumbukwe kwamba watalii wengi hutoka katika nchi zilizoendelea na zenye miundombinu bora sana ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi ni muhimu kuimarisha na kujenga barabara za lami kuelekea kwenye mbuga na hifadhi za Taifa, barabara za kupanda milima iliyopo nchini na barabara zote zinazounganisha maeneo muhimu ya kitalii na miji mikubwa. Katika barabara hizi, ni jambo jema kuweka nakshi za asili kama za mawe kwa maeneo yenye miamba, madaraja ya kibunifu ya mbao kwa maeneo yenye miti mingi na kuweka kila aina ya sanaa za kibunifu zenye kuitangaza sanaa na utalii wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa usafirishaji, Serikali iwekeze na kupanua na kuboresha viwanja vya ndege vya kimataifa na vile vilivyo karibu na maeneo ya utalii kama vile Uwanja wa Ndege wa Arusha, Kilimanjaro, Iringa na kadhalika. Ubora wa huduma za ndege utasaidia kuwafikisha watalii karibu na maeneo ya utalii kwa wakati muafaka na kwa ufanisi mkubwa.
(iii)	Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utalii tunahitaji kuboresha huduma za msingi kama vile huduma za afya, mahoteli yenye hadhi na mawasiliano bora ya simu na internet.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma bora za afya ni moja ya sababu zitakazowapa watalii ari ya kuja kutalii hapa nchini. Ninaishauri Serikali iendelee kujitahidi kuboresha huduma za kiafya kwa kujenga au kushawishi wadau kujenga hospitali zenye hadhi ya nyota tano (five stars) kwa sababu inasemekana Tanzania hatuna hospitali yenye hadhi ya nyota tano (five stars) inayopendelewa kutumiwa na watalii. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasemekana, watalii kutoka nje wanaofika Mbuga za Ngorongoro, Manyara, Kilimanjaro, Mkomazi, Nyerere, Tarangire, Mikumi, Saadani, Gombe, Katavi, Arusha National Park na Serengeti wakipata changamoto kubwa hukimbilia kupata huduma ya afya mjini Nairobi, Kenya kwa sababu Tanzania hatuna hospitali yenye hadhi ya nyota tano (five stars). Kwa sababu hiyo watalii wanaokuja na kuugua hupata hofu ya kurudi tena au husita kushawishi wengine kutembelea Tanzania, hivyo basi idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania hupungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watalii wakija hapa nchini wanahitaji kulala kwenye nyumba safi na zenye hadhi. Ni vyema Serikali ikahimiza wawekezaji wajenge hoteli za aina mbalimbali zikiwemo zile za nyota tano zitakazotoa huduma nzuri za malazi, chakula na za kuwasafirisha watalii kutoka mahotelini kwenda maeneo mbalimbali kutalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo yote wanakopita, kulala na kutembelewa na watalii, ni vyema upatikanaji wa mawasiliano bora ya simu na internet ukawa ni wa uhakika. Serikali iweke minara kwenye maeneo yote haya ili watalii wapate mtandao kila watakapokuwa.
(iv)	Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupanua wigo wa maeneo mapya, ninaishauri Serikali iongeze ubunifu wa kuboresha na kukuza vivutio vya utalii.  Pamoja na kuwa hapa Tanzania kuna vivutio vingi vya utalii, lakini ubunifu katika kuboresha vivutio hivyo bado uko chini. Vivutio vya utalii tulivyonavyo sasa ni vilevile tulivyokuwa navyo miaka nenda rudi, hivyo ni lazima tuwe wabunifu katika kuboresha vivutio vya utalii au kuongeza vingine kwa sababu watalii wetu kila wanapokuja wanatukuta na vivutio vilevile na hakuna tulichoboresha wala kuongeza. Hii inawafanya wasipate hamu ya kurudi tena mara nyingine kwa kuhisi kuwa wamemaliza kutalii Tanzania hivyo hupelekea kupungua kwa idadi ya watalii katika misimu tofauti tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yanayotakiwa kuboreshwa ni yale yenye maporomoko makubwa na ya kuvutia kama yale ya Materuni Waterfalls, Marangu Waterfalls,  Choma Waterfalls, Mount Meru Waterfalls, Engare Sero Waterfalls, Ndaro Waterfalls, Soni Waterfalls, Kinole Waterfalls, Nduruma Waterfalls na Mwalalo Waterfalls, maeneo ya kihistoria kama vile Olduvai Gorge, Kondoa Rock Paintings, Miji ya Kihistoria ya Bagamoyo, Lindi na Mikindani, Magofu ya Kilwa na Bagamoyo, Mapango ya Amboni Tanga, Mahandaki yaliyokuwa yanatumika na wazee wetu wakati wa vita, Jumba la maonesho la Taifa lenye nyara mbalimbali kama mafuvu ya machifu wetu, Mti mrefu kuliko yote barani Afrika ulioko Kata ya Mbokomu, Mkoani Kilimanjaro na kadhalika. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema kufanya ubunifu mbalimbali katika kila eneo. Kwa mfano, wawepo watu wa kuuza vitu mbalimbali kama vinyago, nguo, t-shirt, kanga, skafu zinazotangaza bidhaa mbalimbali za utalii katika sehemu husika. Katika maeneo haya, ufanyike ubunifu wa kuonyesha na kutangaza tamaduni zetu (kupitia nadharia ya Utalii wa Utamaduni) ambapo tutaonyesha na kunadi ngoma, vyakula vya asili na vitu vingine vya kuvutia vya asili.
(v)	Mheshimiwa Spika, ili kuboresha Utalii hapa nchini, ni vizuri nchi ikaweka Sera na Sheria rafiki za kulinda Utalii.  Kufanikisha hili, ninapendekeza yafuatayo yafanyike:-
(1)	Kuboresha na kuimarisha Sheria za Usalama kwa Watalii wanaokuja kututembelea ili kujenga mazingira salama kwa wageni wote;
(2)	Kuhakikisha kuwa Sheria na Sera zinazingatia uhifadhi wa mazingira na haki za wenyeji ambao ni walinzi wa kudumu waraslimali za kitalii katika maeneo yao;
(3)	Kutunga Sheria na Sera madhubuti zinazovutia wawekezaji wa nje na wa ndani katika Sekta ya Utalii, ikiwa ni pamoja na uwepo wa vivutio vya kodi na motisha za kifedha;
(4)	Kuweka Sheria kali za kupambana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori ili kulinda Maliasili za Kitalii;
(5)	Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ya kuboresha ni ile ya huduma za utalii kwa Kundi la Waongoza Watalii. Tanzania inaweza kupokea watalii wengi zaidi ya tunavyopokea sasa ikiwa tutaelimisha waongoza Watalii wetu (Tour guides) na kuwaongezea ujuzi zaidi katika kufanya shughuli zao kwa ufanisi. Ili kufanikisha hili, ninapendekeza kuwepo na Sheria ambayo itawalazimu Waongoza Watalii kuwa na cheti cha fani hii kitakachotolewa na vyuo vilivyothibitishwa na mamlaka za Serikali. 
Sehemu ya mafunzo yao ijikite kwenye kwenda kujifunza namna ya kufanya majukumu yao na kuiga mifano kutoka nchi nyingine zenye mafanikio ya kupokea watalii duniani. Kupitia hili tutaongeza ubora wa huduma katika utalii na kufanya watalii kutoka nje kupenda zaidi kutalii Tanzania hivyo kuongeza idadi ya watalii. Kwa nyakati tofauti warsha na semina za mara kwa mara zitolewe kwa Waongoza Watalii ili wawe na ujuzi wa kisasa wa kutoa huduma bora kwa watalii;
(6)	Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania siku za mbele, ninaishauri Serikali iboreshe Sera ya Visa kwa kupanua Msamaha na Masharti ya Visa za Wageni ili kuwavutia watalii zaidi wa kigeni. Hii ni pamoja na kurefusha muda wa kukaa nchini kwani kufanya hivyo kutasababisha ongezeko la watalii wa kigeni na Sekta ya Utalii itachochea fursa nyingi za kibiashara na kutia nguvu mpya katika maendeleo ya kiuchumi kwani kila wakiwa Tanzania watakuwa wanatuachia fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba, ikiwa tutaziangalia kwa umakini na kutatua changamoto hizi, Sekta ya Utalii itaimarika na watalii wengi wataitembelea Tanzania na hivyo kuchangia kikamilifu katika pato la Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, ninaunga mkono hoja.