Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii. Pia ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Dkt. Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo Sekta ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na pia Uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza Mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza Mhesimiwa Balozi Dk Pindi Chana, Waziri wa Maliasili na Utalii kwa Hotuba Nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa Letu katika ya Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kusababisha Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na program ya kutunza maliasili zetu, Serikali iweke usimamizi wa msitu hasa ya asili, ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya nishati. Katika kupangilia matumizi mazuri ya ardhi, ihusishe Wizara zote zinazosimamia Maliasili, Ardhi, Kilimo, Wizara za Maji na pia Wizara inayosimamia Mazingira. Kwa vile binadamu tunaongezeka ni muhimu kuhakikisha ulinzi kwa kuhifadhi mazingira yetu na kuwepo msukumo zaidi kwenye kuboresha mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza hatua zinazo-chukuliwa na Serikali kurejesha mahusiano mazuri kati ya TANAPA (Hifadhi ya Kitulo) na wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma, Ulenje na Inyala. Kuna mgogoro wa miaka mingi wa mpaka kati ya TFS na wananchi wa Kijiji cha Mwashoma, Kata ya Inyala. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mgogoro huu kuchukua muda mrefu na kusabisha hata uvunjifu wa amani, kuna ahadi ya mwaka 2015 alitoa Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli na kumwelekeza Waziri wa Ardhi na pia Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo kupitia upya mipaka, ili wananchi wa Kata za Inyala, hususani Kijiji cha Mwashoma waachiwe maeneo yao. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yenye mgogoro ni mashamba ya wananchi na wamekuwa walinzi wazuri wa misitu na vyanzo vya maji, ni imani yangu wakiachiwa hayo maeneo yanayogombewa na TFS kwa maslahi mapana kwa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza juhudi za Serikali kuweka umuhimu wa kipekee na kupewa kipaumbele kwa Sekta ya Utalii ili iendelee kuchangia pato la Taifa, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii kupitia fursa za matumizi endelevu ya rasilimali za utalii. Mheshimiwa Rais, amekuwa mstari wa mbele kutangaza utalii kwa kutumia mikakati mbalimbali ikiwemo Programu ya Tanzania - The Royal Tour. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2025 umekuwa mzuri sana kwa Sekta ya Utalii nchini Tanzania. Kwa mara ya kwanza katika historia, nchi imefanikiwa kuvuka lengo lake la kufikisha idadi ya watalii 5,000,000 mapema zaidi kuliko ilivyotarajiwa. Kwa jumla, watalii 5,360,247 wameitembelea Tanzania, ikiwa ni ongezeko kubwa lililochangiwa zaidi na watalii wa ndani ambao wamefikia 3,218,352, huku watalii wa kimataifa wakiwa 2,141,895.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2022, mapato yatokanayo na watalii yameongezeka kwa 93% hadi kufikia Dola za Marekani milioni 2,527.72. Mchango huu wa Sekta ya Utalii bado ni mdogo sana kulinganisha na nchi shindani na lakini umeanza kulingana na maoteo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/2022-2025/2026) umeelekeza kufikia idadi ya watalii wapatao 5,000,000 na kukusanya mapato ya kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni sita kufikia 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa Sekta ya Utalii unakabiliwa na changamoto ya ushindani mkubwa katika soko la utalii wa kimataifa hasa kutokana na miundombinu na hata mazingira ambayo siyo rafiki kwa wawekezaji ikiwemo utitiri wa tozo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya utalii ni sawa na biashara zingine za nje zinazotegemewa katika mapato ya fedha za kigeni, lakini inakabiliwa na utitiri wa tozo katika mnyororo mzima na kusababisha kuwa mzigo mkubwa kupambana na ushindani wa kimataifa. Watalii kama ilivyo kwa biashara zingine wanaangalia sana na ubora wa huduma pamoja na gharama katika mnyororo mzima wa utalii. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nchi yetu kubarikiwa utajiri wa vivutio vya aina mbalimbali, inatakiwa kuwepo na mkakati madhubuti wa kuhakikisha uendelezaji wa vivutio ili kuongeza wigo wa shughuli za utalii na hata kuondoa tozo ambazo ni mzigo kibiashara. Serikali iangalie kuondoa kodi zote ambazo hazitozwi na nchi shindani na pia mnyororo wa biashara ya utalii ichukuliwe kama biashara ya nje (export).
 Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja.