Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kujaribu kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge kufuatia mjadala wetu unaoendelea. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia afya njema na kwamba leo tunaijadili hotuba ya Wizara yetu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ninatumia fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo yake kwa Wizara yetu na kwa msaada mkubwa anaotupa katika Wizara hii. Yeye kama mtaalam wa mambo haya ya utalii anatusaidia sana katika kufanya kazi yetu. Tunamshukuru sana na siku zote amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Wizara hii inapata rasilimali zinazotuwezesha kufanya shughuli zetu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru vilevile Mheshimiwa Waziri wangu, Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana. Amekuwa na msaada mkubwa sana kwangu. Anajitahidi sana kunisaidia niweze kumudu majukumu yangu ya kumsaidia, uzoefu wake katika shughuli za Kiserikali kwa kweli ananisaidia sana, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee ninawashukuru sana Kamati yetu; wamekuwa na msaada mkubwa sana kwa Wizara yetu. Ni watu makini ambao siku zote wanapenda kuona kwamba Wizara hii inafanya vizuri zaidi. Ninataka niwaahidi kwamba tutajitahidi ndani ya Wizara kwa uwezo wetu wote kusikiliza kwa umakini mkubwa yale wanayotushauri na kuyafanyia kazi. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja ambazo zimeibuka, zipo hoja ambazo zimeibuliwa na Kamati yetu. Ninapenda nijielekeze kwenye maeneo hayo, lakini vilevile hoja hizo zimegusiwa na Waheshimiwa Wabunge. Kwenye maoni ya Kamati, Kamati yetu imetuelekeza au imetoa ushauri kwamba Wizara ihakikishe inaendelea kubuni mbinu mpya za kutangaza vivutio vya utalii ili sekta hii iweze kusonga mbele. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili, kazi kubwa inaendelea kufanyika ndani ya Wizara yetu. Wengi wamesema kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Rais katika kutangaza utalii kupitia Filamu ya Royal Tour. Mara baada ya Mheshimiwa Rais kufanya jukumu lile sasa ni jukumu la Wizara na wataalam wetu kuhakikisha habari ile inayafikia masoko yetu. Katika kufanya hivi, tumeweza kuyafikia masoko mengi ambayo yamekuwa na tija katika Sekta yetu ya Utalii. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejitahidi sana kufanya utangazaji kwa kutumia mifumo ya kidijiti ili kuyafikia masoko makubwa. Vilevile, katika misafara yetu ya kwenda kutangaza utalii nje, tumejitahidi sasa kuwa wabunifu; kwamba badala ya kuwapa maneno tu, kule ambapo tunakwenda, wenzetu kule wanakuwa na access ya kuweza kuona moja kwa moja vivutio vyetu kwenye hifadhi zetu. Hili limekuwa na tija sana kupitia mifumo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kuratibu misafara ya namna hiyo kulifikia Soko la China, tumeweza kulifikia Soko la India na sasa tumeanza kuona matokeo ya jitihada hizi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivi hatukuishia kwenye Filamu ya Royal Tour. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, alikubali kwa mara nyingine kushiriki kwenye filamu nyingine ya Amazing Tanzania ambayo tunamshukuru vilevile Mheshimiwa Rais wa Zanzibar ambaye na yeye alishiriki kwenye filamu hii. Filamu hii nayo imezinduliwa kule China, lakini vilevile tumeizindua hapa Tanzania na tumeanza kuona manufaa ya filamu hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejielekeza vilevile kwenye kutumia watu maarufu na tunajielekeza kutumia Sekta ya Michezo ili kuweza kutanua wigo wa maeneo ambayo tunaweza kuyafikia. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi ni mashahidi, hivi karibuni tumekuwa na mazunguzo ya karibu na mmiliki wa ile Timu ya Manchester United. Tulikwenda kufanya mazungumzo kule Uingereza na yeye amekuja hapa na timu yake. Hii yote ni katika kutanua wigo wa jinsi ya kutangaza utalii wetu.  (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashirikiana na mashirika ya ndege katika kutangaza utalii wetu. Mtaona hivi karibuni jinsi ambavyo tunashirikiana na Shirika letu la Ndege la Air Tanzania. Vilevile, tunashirikiana na wenzetu wa Turkish Air na tuna mipango ya kushirikiana na Emirates. Hii yote ni katika kuhakikisha tunafikia soko kubwa zaidi katika kuutangaza utalii wetu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi tunazo fursa za kutangaza utalii na tunazo rasilimali kubwa ambazo tumekuwa tukizitumia hapa nchini. Tukio la nyumbu katika nchi yetu ni tukio kubwa la kiutalii. Sasa tumeamua kutengeneza aina ya kulitangaza hilo tukio la wale nyumbu kuzaliana kwa mamilioni. Liwe ni tukio ambalo dunia inaweza kuja kulishuhudia. Katika mipango yetu, tutaandaa filamu maalum kwa ajili ya jambo hilo. Niseme tu, mikakati ya kutangaza nchi yetu iko mingi na sisi tumejipanga kuelekea huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo Kamati yetu ililisema kwa msisitizo mkubwa ni katika kuhakikisha kile Kituo chetu cha Utangazaji cha DDMNC, tuhakikishe tunawachukulia hatua wale wote ambao walifanya ndivyo sivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Wizara imeanza kuchukua hatua kwa ajili ya watu hao, lakini kama wanavyofahamu sheria zetu za kazi, zimeweka mfumo ambao ni low boost ambao unahakikisha kwamba yule ambaye anatuhumiwa, lazima na yeye atendewe haki ya kusikilizwa ili hatua zikichukuliwa zisiwe na mashaka. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tunachukua umakini mkubwa sana kwenye kulishughulikia jambo hili kwa mujibu wa sheria ili tusiende kwa pupa tukajikuta kwamba tumeliharibu jambo hili badala ya kulitengeneza. Ninaliomba Bunge lako Tukufu liwe na subira, tunaifanya kazi hii kwa umakini mkubwa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ambayo yalisemwa; dada yangu Mheshimiwa Hawa alisema kwenye ubunifu. Ninataka nimpe mfano mmoja tu, kwenye mazao ya utalii, utalii wa kuwaleta watalii kwa meli lilikuwa siyo jambo linalozungumzwa katika nchi hii, lakini ndani ya hii miaka miwili tumefanya kazi kubwa sana ya kuleta cruise ships, watalii wanakuja kwa meli kuja kutembelea katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwanzo wa mwaka huu mpaka kufika mwezi Aprili tayari tulikuwa na meli karibu saba ambazo zimefika katika nchi yetu na jumla ya watalii 936 walikuwa wametembelea. Mwamko wa meli za kitalii kuja kwenye nchi yetu unaendelea kuongezeka. Ninaomba tuendelee kuiamini Wizara yetu, jambo kubwa linafanyika katika kuhakikisha Sekta ya Utalii inaimarika. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo ambayo yamesemwa na dada yangu Mheshimiwa Ritta, katika kuhakikisha utangazaji wa utalii kwenye kanda ile anakotokea unaweza kufanyika. Sisi kama Wizara tumesikia, wenzetu wa TTB watakwenda kulifanyia kazi jambo lile ili kuhakikisha tunashirikiana na maeneo haya ambayo yameanzisha maonesho ya kiutalii. Tusiyapokee majukumu yao lakini tufanye kazi kwa pamoja ili kuweza kuongeza thamani katika shughuli hizi wanazozifanya. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, ninakushukuru kwa kunipa muda huu. Ahsante sana. (Makofi)