Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninachukua nafasi hii kutoa shukrani za dhati kabisa kwa kupata fursa hii ya kuhitimisha hoja. Pia ninatoa shukrani kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na ninasema, kwanza michango imeingia kwenye Hansard, lakini pamoja na michango kuingia kwenye Hansard, tutahakikisha tutaweka kwenye maandishi kila mchango na kuwasilisha. Kwa hiyo, tunatoa shukrani za dhati kabisa kwa Waheshimiwa Wabunge kwa michango yote. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunatoa shukurani nyingi kwa Kamati yetu ya Bunge; Kamati ambayo imekuwa ikitushauri mambo mengi mazuri na imeweza kufanya hata mapato ya utalii yameongezeka, idadi ya watalii pia wameongezeka sana. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kuelezea suala ambalo limezungumziwa kwa kiasi kikubwa, ambalo ni suala zima la uhifadhi na hasa mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori. Kwa kweli eneo hili sisi kama Wizara tunazidi kutoa kupaumbele cha hali na mali kuhakikisha kwamba tunadhibiti wanyamapori na tunahakikisha kwamba takwimu za ajali (injury) na takwimu zingine zinazotokana na wanyamapori kuleta uharibifu kwa binadamu na mazao zinazidi kupungua au kutokuwepo kabisa. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazidi kuweka mikakati thabiti kabisa ya kuhakikisha kwamba tunadhibiti eneo hili.  Katika bajeti hii, tumesema tunakwenda kununua helicopter zipatazo mbili za TANAPA na Ngorongoro NCAA. Hii yote ni katika kudhibiti mwingiliano utakaokuwepo na kufika kwa haraka kuratibu. Pia, tumeshaelekezana kwamba, sasa wakati umefika wa kulinda maeneo yetu ya hifadhi kwa njia ya teknolojia. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa na teknolojia, maana yake unaweza ukaona eneo lako la hifadhi na unaweza ukaona kwamba, sasa tembo wametoka. Hii ni pamoja na kufunga collar maalum. Collar hizi unaweza ukaziona kwenye computer na ni rahisi kujua, katika hifadhi fulani, kuna tembo wanatoka kwenye hifadhi kwenda kwenye maeneo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubaliana tutakwenda kununua collar na tutakwenda kuchimba mabwawa katika bajeti hii. Haya mabwawa yataweza kusaidia kuhakikisha kwamba maeneo ya hifadhi yana maji na hata Mheshimiwa fulani amezungumza hapa kwamba, wakati wa mvua imedhihirika kabisa tembo hawatoki zaidi katika maeneo ya hifadhi. Kumbe maji ni kipaumbele katika maeneo yetu ya hifadhi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda vilevile kuweka ujenzi wa vizimba ambavyo vitasaidia sana kudhibiti mamba na viboko katika maeneo yetu mbalimbali. Hivi sasa tumeshaanza kuweka vizimba na Waheshimiwa wengi wameomba vizimba. Tumesikia na tutakuja huko kuhakikisha kuna vizimba ili watoto wanapoenda kuoga na akinamama kufua, wawe salama. Kwa hiyo, tutakwenda kuweka vizimba. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakwenda pia kuendeleza ujenzi wa vituo vya askari katika maeneo yetu ambayo ni korofi yanayoonyesha kwamba takwimu za mwingiliano ni nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tunakwenda pia kununua pikipiki na magari kwa ajili ya kusaidia askari wetu. Tumewasiliana na Waheshimiwa, kuna Waheshimiwa wanasema maeneo yetu hayana vitendea kazi vya kutosha. Tutahakikisha maeneo hayo tunasogeza vitendea kazi ili askari wetu wapate vitendea kazi, iwe ni pikipiki, magari au iwe ni ranger post. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda pia kununua ndege nyuki. Ndege nyuki hizi ni drones ambazo zinatoa sauti kama ya nyuki ambapo tembo akisikia anaikimbia ile sauti na mara nyingi tunatumia ndege nyuki kusogeza hawa tembo kurudi katika hifadhi ili wasilete madhara. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia takwimu tangu nimeingia kwa kweli, takwimu hizi za ajali (Injury) na matatizo mengine ya mwingiliano, ni takwimu ambazo nimeelekeza na kukubaliana kwamba lazima zishuke. Tuweke mikakati, mipango imara na tuhakikishe kwamba takwimu za mwingiliano, ajali za wanyama na wananchi zinakwenda kushuka na hatimaye kutoweka kabisa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kununua mabomu na kugawa mabomu. Haya yanaitwa mabomu baridi ambayo yanasaidia kusukuma wanyama. Pia, Waheshimiwa wamesema kwenye baadhi ya maeneo kuna upungufu wa askari na hayo maeneo tumeshayachukua, lakini tunakwenda pia kuajiri askari wa kutosha ili kuona ni kwa namna gani tunakwenda kuwapeleka katika maeneo mbalimbali. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha tumeomba askari 850 na mpaka sasa mchakato wa kufanya shughuli za utumishi ili askari hao wafike unaendelea. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na askari, kuna mafunzo ya wanyamapori kwa askari wa vijiji ambao tunawaita Village Game Scout. Mafunzo hayo hutolewa kwenye vyuo vyetu kama Likuyu Sekamaganga na vyuo vingine na mafunzo haya yanasaidia sana vijana wetu hawa wanapopata mafunzo ili kuhakikisha kwamba wanaweza kudhibiti pale inapotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, tayari kwa kushirikiana na TAWIRI, tunakwenda kuhakikisha kwamba na mikanda inanunuliwa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tunakwenda kuweka mkakati wa kukabiliana na wanyamapori, mkakati huu tunakwenda kuuanzisha 2025 – 2030. Tulikuwa na mkakati wa awali wa 2020 – 2024, na sasa tunakwenda kuhuisha na kuwa na mkakati mwingine ambao utaanza Julai, 2025 – 2030, lakini tumesikia changamoto ya tembo, changamoto ya nyani katika maeneo ya Rombo, Kyela na wanyama wengine kama mamba, kiboko tumesikia na haya yote tunakwenda kushughulikia ipasavyo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mengine ambayo tumeyazungumza hapa ni suala zima la fedha za utalii (Tourism Development Levy). Awali ya yote nichukue nafasi hii kutoa shukurani za dhati kwa Serikali kuridhia tuwe na asilimia sita ya TDL, asilimia sita hizi wakati wa UVIKO tulikuwa hatuzipati na mnamo 2021/2022 kutokana na hali ya UVIKO hatukuwa na na fedha hizi za TDL. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi tunalishukuru Bunge lako, tunamshukuru Mheshimiwa Rais tumeanza kupata mnamo bajeti iliyopita Julai, mwaka jana. Tunatoa shukrani za dhati kabisa kwa fedha hizi ambapo Kamati pia imezungumza na Wabunge wengi, fedha hizi zimesaidia katika sehemu kubwa sana. Fedha hizi za TDL ni kwa manufaa ya kuendeleza utalii nchini. Tuseme kwamba katika kipindi hiki tumeweza kupata fedha hizi hadi mwezi Juni. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zimesaidia maeneo mengi kama walivyosema Kamati na mpaka sasa bado tunazo fedha takribani bilioni 22 hatujazitumia na tutazitumia kwa maelekezo ya Kamati ya Bunge. Kamati ya Bunge imeelekeza vizuri kwamba ili kutumia fedha hizi ni lazima tuwe na vipaumbele. Kamati imeeleza vizuri kabisa kwamba, ni vizuri tunapotumia fedha hizi tutumie kama ilivyo Mfuko wa Tanzania Forest Fund, nasi tunasema haya ni masuala ya msingi na ndiyo maana tumekuwa tukijadiliana na Kamati. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata kiasi kisichopungua takribani bilioni 33 na sasa bado tunazo bilioni 22. Kwa hiyo, tunatoa shukrani kwa mawazo mazuri. Fedha hizi ni lazima zitumike kwa mujibu wa utaratibu ambao tumejiwekea na utaratibu ambao ni wa wazi. Kwa hiyo, tunashukuru sana, kwa mawazo na ushauri wa Kamati. 
Mheshimiwa Spika, tumesema kwanza tutakuwa na Mratibu maalum, Mratibu ambaye atakwenda kusimamia fedha hizi vizuri, pia tutakuwa na Kamati ya Ushauri, tunaweza tukasema ni Kamati ya Ushauri kwa mujibu wa GN, tunaweza tukasema ni bodi ambayo hata yale mashirika yanayochangia katika fedha hizi za Tanzania Tourism Development Levy asilimia sita ambapo zinatoka, TANAPA, Ngorongoro, Conservation Commissioners wote wanakuwa ni sehemu ya ile bodi ya kukubaliana kwamba fedha hizi ziende wapi. Hii ni Kamati ambayo ipo kwa mujibu wa Kanuni na Sheria na ni Kamati ambayo ni lazima itoe ushauri. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ushauri wa Kamati tumesema kwamba, maoni mengi sana katika fedha hizi yamekuwa ni miundombinu, hivyo tuangalie ni namna gani fedha hizi zinaelekezwa katika suala zima la miundombinu, iwe ni masula ya madaraja, iwe ni masuala ya barabara tuone ni namna gani tunakwenda kuboresha eneo hili. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu inasaidia sana kuongeza Watalii. Watalii wanapokuja wanataka kuona barabara nzuri, hapa tumeona maoni ya Waheshimiwa Wabunge, wanasema “barabara zifunguliwe” na sisi tunaunga mkono hizi ni hoja za msingi sana. Barabara zetu ni lazima zipitike, tena zipitike kwa wakati wote siyo tu wakati wa kiangazi au wakati wa kipupwe. Kwa hiyo, fedha hizi kimsingi zitakuwa na chombo maalum.  (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu UVIKO hii ni mara ya kwanza tumepata, tangu baada ya UVIKO 19, hapo katikati zilikuwa hazijatoka kutokana na hali ya UVIKO, kwa hiyo tunatoa shukrani sana kwa Kamati, shukrani nyingi kwa Bunge na sasa tuendelee kuboresha mikakati na hizi fedha zitasaidia.  Kama tulivyosema safari hii tunakwenda kukusanya bilioni za kutosha takribani trilioni moja, kwa hiyo fedha hizi zitasaidia masuala mazima ya kuboresha miundombinu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweka mfano wa 60%, 70% miundombinu, asilimia chache kidogo inayobaki tunaweza tukasema kuimarisha masuala ya masoko ya mafunzo na utafiti, tunahitaji utafiti, asilimia kidogo tunaweza tukasema 10% kwenye tourism marketing, training and research na masuala ya uwekezaji katika vifaa vya teknolojia, lakini asilimia kubwa ni miundombinu, tukiweza kufanikisha barabara, madaraja kama walivyosema Waheshimiwa “barabara yangu huku” wamezungumza hapa, malango, kwa mfano kufungua lango ambayo yapo karibu na hifadhi. Mheshimiwa Musukuma amezungumzia lango na Mheshimiwa Mama Sitta amezungumza lango.  Maeneo ya umwagiliaji Mheshimiwa Kakunda kazungumza, kuongeza na kufungua Utalii Kusini, hii yote inahitaji miundombinu ya kutosha. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi za TDL kwa kweli zitakwenda kusaidia na tunakwenda kuweka mikakati thabiti, ambapo zitakuwa na uwazi, zitakuwa na ushirikishwaji na kuhakikisha tunaweka kwenye vipaumbele ambavyo kimsingi vitasaidia kurudisha tena mapato. Hivyo tunaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ile filamu ya Tanzania the Royal Tour, Amazing Tanzania na mikakati mingi ya amani na utulivu katika nchi na ndiyo maana tumeweza kufikisha wataliii milioni 5.3 kama tulivyoelekezwa na mapato ya bilioni 3.9. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hii, Wabunge wamezungumzia suala la retention, tunaunga mkono suala hili, ni lazima kuwepo na retention. Katika maeneo haya ya hifadhi tunahitaji marekebisho iwe ni madaraja, sasa kama hakuna retention maana yake tutasubiri OC na tukisubiri OC yamkini daraja linabidi lirekebishwe haraka mara moja. Kwa hiyo, tunaendelea kushukuru kwa political will na maelekezo bayana kabisa kwamba sasa TANAPA na Ngorongoro kutakuwa na retention. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshalijadili hili jambo kwa kina na sasa tutaona mapendekezo haya katika Finance Bill inayokuja, kutakuwa na retention katika Shirika letu la TANAPA pamoja na NCAA (Ngorongoro) kwa kuanzia na baadaye kadri tunavyoenda tutaangalia na mashirika mengine jinsi ya kuwa na retention. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la Jumuiya za Wanyamapori za Jamii (Wildlife Management Area). Haya ni maeneo ambayo yapo pembezoni mwa hifadhi, baada ya hifadhi pembezoni. Wananchi wanasema sisi tunaachilia eneo letu litumike kama Jumuiya ya Wanyamapori ya wananchi, maeneo haya yanasaidia sana. Kwanza kupunguza changamoto kati ya wanyama wakali na wanadamu, wanyama hawajui mipaka anatoka kwenye hifadhi, anapotoka kwenye hifadhi kunapokuwa na WMA maana yake anaingia katika eneo lenye grade nyingine ya hifadhi, lakini siyo kama maeneo ya TANAPA, TAWA au Ngorongoro. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya wananchi wenyewe wanasema tuna-surrender kwa ajili ya manufaa yetu, wananchi wanawaalika wawekezaji wanaweka camp, wanaweka lodge, wanapata mapato, vijana katika maeneo hayo wanapata ajira za ulinzi kama vile Game Scout, wanapata ajira mbalimbali na fedha nyingi za utalii zinakuwa zinapatikana. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa wamezungumza fedha za WMA zinazotokana na masuala ya picha, kwa maana utalii wa picha una mapato, lakini kuna baadhi ya WMA wanafanya shughuli za uwindaji (hunting) na wao pia wanastahili haki yao. Hivyo, maoni ya Waheshimiwa wamesema fedha hizi, sheria zirekebishwe na zipatikane kwa wakati na kwa haraka. Hili ni eneo ambalo tumeshaanza mjadala ili fedha hizi ziweze kupatikana kwa wakati na kwa haraka. Kwa hiyo, eneo hili tunaendelea kuliboresha na niwashukuru sana wananchi. Yale maeneo ambayo yana hifadhi, yana maeneo ya wanyamapori ambayo hayana maeneo ya Jumuiya ya Wanyamapori, tuone ni namna gani ya kuanzisha haya maeneo, tayari Wizara yangu inaenda kutoa elimu, umuhimu wa kuwa na WMA. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimetoa fedha kwa WMA. Eneo ambako kuna WMA, kwanza Halmashauri inapata mapato kama halmashauri yanayorejeshwa, lakini ile WMA yenyewe inapata na Serikali ya Kijiji inapata. Tumeshuhudia baadhi ya WMA wanapata hadi bilioni 1.3 ambazo zinasaidia maendeleo, zinasaidia uhifadhi, lakini Serikali za Vijiji zinapata mpaka milioni 600. Haya ni maeneo ambayo kwa lugha ya kitaalam wanaita shoroba (corridor za wanyamapori) maeneo haya huwezi kuweka makazi, maeneo haya huwezi kuweka mashamba. Kwa hiyo wakati umefika wa kuridhia kwamba maeneo kama haya nje, kijiji chenyewe kinaamua kwamba haya tunayahifadhi kama buffer zones na wanaweka WMA. Kwa hiyo, haya ni maeneo ambayo yanasaidia sana na tayari nimeshaongea na baadhi ya Wakurugenzi tuone ni namna gani ya kuendelea kutoa elimu ili tupate maeneo ya WMA. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tayari tumeshaanza kurekebisha Sheria ya Kifuta Jasho na Kifuta Machozi. Hivi sasa kifuta machozi tumeoongeza 100%, kifuta jasho tumeongeza 50%. Hivi sasa tupo katika Mfumo wa PAIS, huu ni mfumo ambao utasaidia fedha hizi kama walivyosema Waheshimiwa zipatikane kwa haraka na kwa wakati. Mfumo huu unaitwa Problem Animal Information System. Tumeshakaa na Maafisa wa Wanyamapori katika Wilaya zetu zote nchini na kuwaelekeza jinsi ya kuweka data katika maeneo haya. Sambamba na hilo, tunaanza na pilot katika Wilaya 10 kuona ni namna gani ya kutumia huu Mfumo wa PAIS kwa ajili ya suala zima la kifuta jasho na kifuta machozi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, lipo suala la geti, suala la geti ni miongoni mwa vipaumbele vyetu. Tumesema sambamba na njia mbalimbali tuone ni namna gani tunakwenda kuweka geti au kwa lugha nyingine tunaita fence, fence zinasaidia sana kuhakikisha kwamba wanyama hawa hawapiti kwenda kudhuru wananchi, tayari tumeshaweka makadirio ya kujenga hizi fence, fence ambazo zitazuia mwingiliano kati ya wanyama wakali pamoja na wananchi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa kushirikiana na wadau tumeshajenga kilometa takribani 61 za uzio wa umeme katika bajeti hii na katika bajeti ijayo tumesema tunakwenda kujenga takribani kilometa 53, ikiwa ni kutoka Loduare kuelekea Oldeani kilometa 15 katika Wilaya ya Karatu ili kudhibiti wanyama hawa.  Pia, Hifadhi ya Ngorongoro, pia kilometa 38 kutoka Tabora ‘B’ hadi Mto Mara ili kudhibiti wanyama wanaotoka Hifadhi ya Serengeti, hii ni corridor nyingine. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani kabisa tukiweka mikakati hii uhifadhi utakuwa na manufaa, wananchi watakuwa na amani, watachangia uhifadhi, lakini sisi wenyewe wahifadhi tutaona kwamba wananchi wetu wako salama, wanaendelea vizuri na kuhakikisha kwamba uhifadhi unachangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, mengine yote tutaleta kwa maandishi, kunaomba kuwasilisha kama nilivyotoa ufafanuzi.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, bado unatoa hoja yako.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutoa hoja.  (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaafiki.