Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kingu, naomba ukae kidogo. 
Ninaomba wafuatao wajiandae baada ya Mheshimiwa Kingu kumaliza. Mheshimiwa Tecla Mohamedi Ungele atafuatiwa na Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara na Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga. Mheshimiwa Kingu, endelea.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa heshima ya kuwa mchangiaji wa kwanza asubuhi ya leo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niendelee kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI ambao mimi ni Mwenyekiti wao, kwa namna ambavyo tumeweza kufanyakazi kwa kipindi kifupi cha kuisimamia na kuishauri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme mambo machache; pamoja na kwamba jana tumetoa taarifa ya Kamati, tumeeleza mafanikio na changamoto, ninataka nikwambie kitu kimoja, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa kipindi cha huu mwaka ambao nimekuwa Mwenyekiti, ninataka nitumie fursa hii, nitakuwa mchoyo sana wa fadhila kama sitaeleza weledi mkubwa na ushirikiano mkubwa ambao Kamati hii umeipata kutoka kwa Waziri - Mheshimiwa Jenista Mhagama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ninawasihi sana wananchi wa Peramiho, kwa uhodari wa mama huyu, kwa namna na muda mfupi aliokabidhiwa kuiongoza Wizara hii ya Afya, Wizara ambayo ni very complex, Wana-Peramiho na Watanzania nataka niwaeleze, mama huyu ameonesha umahiri wa hali ya juu sana. Ameonesha umahiri wa hali ya juu sana kuiongoza Wizara hii ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie Mama Jenista mama yangu, tabia yake ya unyenyekevu na ushirikiano ndio umetufanya Kamati yetu tuweze kufanya kazi na yeye. Pale ambapo tulikuwa tunamwambia hili hapana, alikuwa unanyenyekea na kurudisha majibu yanayotakikana kwa maslahi ya watu wetu. Hongera sana mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimsemee Naibu wake, kaka yangu Dkt. Mollel. Ninamshukuru sana kwa niaba ya Kamati, Naibu wangu Waziri, naye pia ni kijana mnyenyekevu na msikivu. Ahsante sana Dkt. Mollel, amekuwa msaada mkubwa sana kwa Kamati yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimebahatika kusafiri na Mheshimiwa Jenista kwenye nchi kadhaa katika mambo ya kampeni hizi za kimataifa. Huyu mama si wa kawaida, ninaomba niseme hivyo. Unaweza ukahisi kwamba mama huyu ameweza kuwa na connection na Mawaziri wa Afrika kama vile ameweza kuwa na connection na Wabunge kwenye Bunge hili, kwa namna ambavyo ameweza kuzoeana nao. Mama Jenista ni hazina kwa nchi yetu. Mimi ninampongeza sana dada yangu na Mungu ambariki. Atashida Ubunge na In Shaa Allah akirudi hapa kama ataendelea kuiongoza Wizara hii, hayo siyo ya kwangu, lakini sisi Watanzania na kama Kamati tumeridhika sana na ushirikiano wake, yeye, naibu wake na Katibu Mkuu wake, kaka yangu Shakalaghe, mtu mahiri kabisa, pamoja na watendaji wote wa Wizara. Ahsanteni sana kwa ushirikiano. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nishauri mambo matatu; la kwanza; katika vifurushi ambavyo National Health Insurance Fund wamevileta, ninataka niwakumbushe Watanzania ili Watanzania waweze kupata picha wasije wakafikiri kwamba hii ndiyo bima ya afya sasa imeshaleta vifurushi. Vifurushi hivi ni option kwa watu ambao wanahitaji kupata huduma za extra za matibabu kama ilivyo katika mifuko mingine. Kwa mfano, tuna watu wa Jubilee Insurance, wana bima zao zingine zinakwenda mpaka milioni nane, milioni saba. Kwa hiyo, hivi si vifurushi vya universal health coverage, hizi ni option kwa mtu ambaye anataka kukata Jubilee, NHIF wameamua kujipanga kibiashara na wao wawe kama mashirika mengine ya kutoa bima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukisoma vifurushi hivi, bado wameweza ku-accommodate Watanzania. Kwa mfano, kifurushi cha mtu mmoja cha Tarangire, kipo kifurushi ya shilingi 168,000 ambacho kinampa mtu mmoja access ya kupata matibabu sawa sawa na mtu ambaye amekwenda kwenye Jubilee Insurance akaamua kukata kifurushi cha level hii. Itakapokuja Universal Health Coverage, rate ambazo zitatumika nchi nzima, hizo zitakuwa ni rate entry kwa Taifa zima, hazitakuwa na ubaguzi kwa nchi nzima. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ninaomba lieleweke ili kusudi Bunge hili lisije likaonekana kwamba limejadili kitu ambacho kitaleta taharuki kwa umma na kikawafanya NHIF waonekane kwamba huenda hawajatii maelekezo ya sheria tuliyoitunga ya Bima ya Afya kwa Wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni vifurushi optional ambapo na wao wameamua kuingia kibiashara kama ilivyo kwa makampuni mengine. (Makofi)              
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu MSD; ninataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, dada yangu. Hivi tunashindwa nini sisi Tanzania? Tumeweza kuwa na energy security kwenye nchi, tumeweza kuwa na water security kwenye nchi, tumeweza kuwa na food security kwenye Taifa letu, hivi ni kitu gani kinatushinda sisi kama Watanzania kuhakikisha ya kwamba tunakuwa na viwanda vya kutosha vya kuzalisha dawa katika Taifa letu ili kusudi fedha nyingi tunazozitumia kuagiza dawa ziweze kubaki ndani ya nchi? (Makofi)             
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikushauri Mheshimiwa Waziri dada yangu amtafute mtu anayeitwa Meja Jenerali Kingu aliyekuwa Balozi wa Tanzania Algeria. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikwambie, Taifa la Algeria ni marafiki zetu sana sisi Watanzania. Algeria wameweza kuzalisha dawa zao ndani kwa matumizi ya ndani na export kwa zaidi ya 80% mpaka 90% kwa viwanda vya ndani. (Makofi)              
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nishauri, walishafanya engagement na watu wa MSD kama sikosei. Mavere ni kijana, Taifa hili limemwamini na amefanya kazi kubwa sana ya kizalendo kuleta mageuzi makubwa MSD. Tumeona ameweza kupandisha kiwango cha ukusanyaji wa maduhuli na usambazaji wa dawa, ninampongeza sana kaka yangu. Hata hivyo, kwenye jambo hili la uzalishaji wa dawa kwenye Taifa letu, ili nchi yetu iweze kuwa na mambo ya usalama wa afya, ninawashauri, Algeria wameweka milango wazi kwa Tanzania. Waende wakafanye majadiliano na Taifa la Algeria ili tuweze kufanya PPP katika uzalishaji na usambazaji wa dawa katika Taifa letu. Tuweze kuokoa fedha za Watanzania zinazopotea kwa kununua dawa nje ya nchi. (Makofi)             
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie Mheshimiwa Jenista Mhagama, dada yangu, akiweza kuwasaidia MSD pamoja na private sector watakuwa wametenda haki na kuacha legacy jambo ambalo litakuwa limefufua ndoto na matarajio ya Mwalimu Nyerere aliyokuwa ameyawaza ya kuifanya Tanzania liwe Taifa la kuzalisha bidhaa zake ndani na kuuza kwa majirani zetu. (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwenda mbali, MSD tulishapewa mpaka opportunity ya ku-supply dawa kwenye nchi za SADC. Ninawaomba sana watu wa Wizarani pamoja na Wizara ya Fedha, na ninashukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu wa uwekezaji yuko hapa Profesa Kitila Mkumbo. Ninamwomba kama yangu akae na MSD, Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya na Wizara ya Viwanda na Biashara, watengeneze blueprint, specifically kwenye sekta ya uzalishaji wa bidhaa za dawa ili waweze kuacha legacy na wamfute machozi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya uzalishaji wa dawa. (Makofi)             
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili la vifurushi nimeeleza, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sita-recommend kazi nzuri inayofanywa na mwanamama Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote. (Makofi)             
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa kwenye Kamati hii kwa muda mrefu sasa. Wakati Irene anaingia madarakani mfuko huu ulikuwa umeanza kuleta hofu kwa Watanzania. Leo tunapozungumza makusanyo kwa mwezi dada huyu amepandisha fedha zinakwenda mpaka takribani shilingi bilioni 110. Hongera sana Mkurugenzi wa NHIF dada yangu. (Makofi)             
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ninalomwomba, aendelee kushirikiana na watu wake, pale ambapo Kamati ya Kisekta inatoa ushauri wasiupuuze ushauri. Kwa mfano, hata hili la vifurushi tuliwaambia wakimaliza kuvitengeneza wavirudishe kwenye Kamati. Sasa angalia watu hawana elimu ya kutosha, watu wamepata taharuki, kumbe jambo hili ni jema kabisa. Ikiwa wangeleta kwenye Kamati watu leo hapa Waheshimiwa Wabunge wangekuwa ma-champions, wangewaelekeza Wabunge wenzao wajue kwamba vifurushi hivi ni option, siyo universal health coverage. Hili jambo ni simple kabisa wala hakuna sababu ya kuwa na taharuki kwa nchi wala kwa Bunge. Kwa maelezo yangu ninaimani nimewasaidia kuliweka vizuri. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho na la tatu, ushauri ninaoutoa kuhusu nafasi ya Chief Medical Officer (CMO) wa Serikali kwenye Taifa letu, mimi nina maoni tofauti. Ninashauri, kulingana na unyeti wa nafasi ya CMO kwenye nchi yetu, kulingana na unyeti wa nafasi na roles zake CMO kwenye Taifa letu, ninawashauri Wizara wakae na wafikirie kama wanaweza wakatunga sheria ya kufanya Ofisi ya Chief Medical Officer wa nchi yetu iweze kuwa chini ya Wizara, lakini ipewe independence ambayo itaweza ku-safeguard interest za nchi katika kazi anazozifanya CMO. (Makofi)             
Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu ya CMO ni nyeti sana, kuna wakati mwingine zinaweza zikatokea rabsha za kisiasa zikamfanya CMO akashindwa kufanya majukumu ambayo yatalinda interest ya nchi yetu, interest ya watu wetu na kuhakikisha professionalism inafuatwa. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nitoe ushauri, waangalie namna kama inawezekana, wakaifanya taasisi hii ikawa independent chini ya Wizara, lakini usimamizi wake ukawa kwa namna ambayo wataweza kutanguliza mbele maslahi ya nchi na kuhakikisha kwamba Taifa letu linakuwa salama nyakati zote. (Makofi)    
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)