Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima na afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupambania afya za wananchi wa Tanzania na amekuwa mtekelezaji wa kwanza wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025, Ibara ya 83 inayosema “Kuhakikisha wananchi wanapata afya na siha bora.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Waziri huyu Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Mollel; Katibu Mkuu, Dkt. Shekalaghe na watendaji wote wa Wizara hii ya Afya mpaka ngazi ya kijiji. Watu hawa wanafanya kazi kubwa sana kuhakikisha Watanzania wana afya njema. Watendaji hawa wameendelea kuwa na ari ya kufanya kazi na ninaomba waendelee kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na tusonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninapongeza kazi kubwa zinazofanywa na watoa huduma za afya kule vijijini hawa Community Health Workers ni kazi kubwa sana. Ninaomba kama walivyoahidi wenyewe wataendelea kuongeza kada hii, ili waendelee kufanya kazi hii kwenye ngazi ile ya vijiji na mitaa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza kwa mageuzi makubwa yaliyofanywa kwenye Wizara ya Afya. Mageuzi haya nikitolea mifano michache tu, tunaona vifo vya wanawake wakati wa uzazi vimepungua kwa kiasi kikubwa sana kutoka wanawake 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwezi Februari, 2025. Haya ni mageuzi makubwa sana na ndiyo yaliyofanya mpaka Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan akapata tuzo ile ya The Global Goalkeeper Award. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili tunaomba vifaa viongezwe kwenye yale maeneo ya watoa huduma hawa wanaohudumia watoto na akinamama kwenye vile vyumba vya uzazi na huduma za watoto wachanga. Ninapongeza pia Wizara kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na wauguzi nchini Tanzania, tunaona ukurasa wa 144 mpaka 147 unaongelea kuhusu huduma za wauguzi nchini. Pia tunaona 80% ya huduma za afya zinafanyika na wauguzi na wakunga nchini Tanzania, hii kazi kubwa sana, tuwapongeze sana wauguzi na wakunga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu katika eneo hili, ninaomba kuwe na elimu. Elimu iendelee kutolewa kwa wauguzi na wakunga kuanzia ngazi ya kijiji mpaka ngazi ya Taifa kwa kuthamini mchango wao wa huduma za afya katika nchi yetu. Pia hata maeneo yao yaboreshwe, kwa mfano kuna hospitali nyingi katika nchi hii bado wauguzi na watoa huduma za afya hawana maeneo mazuri ya kuishi (nyumba za kuishi) katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwenye Mkoa wangu wa Lindi, sisi Wana-Lindi tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya, zahanati zimejengwa, vituo vya afya, hospitali za wilaya na hata hospitali ya mkoa, zimejengwa. Pia kuna huduma za ICU pamoja na huduma za dharura na vitendea kazi vimewekwa kwenye maeneo hayo. Tunashukuru sana kwa huduma hizo. Sisi Wana-Lindi tunashukuru, kwa maana huduma za ICU zinaokoa maisha. Pale ambapo mgonjwa anazidiwa sana, anapopewa huduma hizi za ICU (wagonjwa mahututi) inaboresha afya yake na pia inaokoa maisha yake. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hospitali yetu ya Mkoa wa Lindi pale Sokoine, majengo ni chakavu. Nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba majengo hayo yamehamishwa, yamejengwa majengo mapya kwa ajili ya uchakavu. Sasa ninachoomba jengo lile la hospitali ya mkoa ambayo ni ya rufaa, inayojengwa maeneo ya Mitwero, nimetembelea pale nimekuta bado majengo mengine hayajakamilika. Ninaomba majengo yale yakamilike ili huduma itolewe vizuri, kwa maana pale ilipokuwepo mpaka sasa hivi majengo yale ni chakavu sana, Hospitali ile ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa eneo lingine tunashukuru kwa majengo yale ya EMD ambayo ni majengo ya huduma za dharura, pia na ICU. Pia tunaomba kwa sababu huduma hizi ni nyeti sana, tunaona kwa Mkoa wa Lindi wilaya nyingine zina EMD, lakini wilaya moja tu ndiyo ina ICU. Kwa unyenyekevu mkubwa sisi Wana-Lindi, tunaomba majengo yale ya EMD, pia hospitali zote zikamilike, kuwe na majengo ya wagonjwa mahututi, lakini pia na huduma za wagonjwa wa dharura kwa sababu hizi huduma ni muhimu sana katika huduma za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sisi Wana-Lindi tunashukuru kwa Madaktari Bingwa wa ile Kampeni ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunashukuru wilaya zote wame-cover, wameenda kutoa huduma zile, hii imerahisisha wagonjwa ambao hawakuweza au wasingeweza kupata huduma za kibingwa kutokana na umbali au rasilimali fedha wamepata huduma zile kwenye wilaya zao, kwa kweli tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hawa Madaktari Bingwa wa Kampeni ya Dkt. Samia, imewezesha pia madaktari na watoa huduma katika hospitali za wilaya wamepata ujuzi na maarifa kiasi kwamba hata walivyoondoka bado wale waliobaki kutoa huduma kwenye maeneo yale wameendelea kuwa na ujuzi na maarifa kutokana na madaktari wale wa Dkt. Samia Suluhu Hassan. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la rasilimali watu; Mkoa wa Lindi ni mkoa uliopo pembezoni, lakini pia tuna changamoto nyingi, tuna changamoto ya kuwa na rasilimali watu wa huduma za afya wachache, tukiacha huduma za madaktari bingwa. Tunaona Hospitali ya Mkoa wa Lindi tukianzia hapo Sokoine hakuna Madaktari wa Dawa za Usingizi, hakuna Madaktari wa Mionzi, hakuna Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani (physician), lakini hakuna Madaktari wa Magonjwa haya ya ENT (koo, pua na sikio), madaktari hawa wengine wameenda kusoma. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa wale waliokuwepo sasa kuna upepo fulani ama kuna shida fulani ya kuhama, tunakuwa nao wakati fulani, lakini wanahama au wanahamishwa kwenda hospitali nyingine kubwa. Sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuwa unapanga mipango mbalimbali ya kuhusu kusambaza Madaktari Bingwa, ninaomba utukumbuke Mkoa wa Lindi katika hospitali yetu ile ya Mkoa ya Sokoine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi hii na ninapongeza kwa kazi kubwa ya Waziri huyu Mheshimwia Jenista Mhagama na tunamwombea kule Peramiho apate tena nafasi ya Ubunge na arudi tena hapa tuendelee kuchapa kazi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)