Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, nami nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha katika Bunge hili kwa miaka mitano sasa, ni baraka tu za Mungu na ni upendo wake. Pia nipende kuwashukuru sana sana wananchi wa Mdunduwalo kwa sala zao na kuniombea nikaweza kuwa salama na mwenye afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi nyingi sana kwa Wizara ya Afya, Mheshimiwa Waziri, pamoja na Naibu wake. Kijiji cha Mdunduwalo kilipata shida sana, ninajua Mheshimiwa Mbunge huyo ambaye ni Waziri, lakini na zahanati ile sasa imekamilika. Nikushukuru sana kwa sababu Wizara yako ilileta kile kifaa cha kuhifadhi dawa za chanjo, ahsante sana Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitoe pongezi kwa watendaji wako ambao ni wanafunzi wangu wazuri akiwemo Dkt. Mafumiko, pamoja na Dkt. Paul Muhame wa dawa asilia. Wale ni vijana wangu niliwafundisha biology, kwa hiyo una vijana wazuri ambao ni tunda langu hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niseme kwamba ninawapongeza na kuwashukuru Wabunge wote ambao mmenitia moyo wakati ninatetea vyuo vikuu akiwemo Mheshimiwa Profesa Muhongo, Mheshimiwa Dkt. Bashiru, Mheshimiwa Mama Anne Kilango, Mheshimiwa Profesa Manya; rafiki zangu akina Mheshimiwa Janeth na Mheshimiwa Esther Matiko, mmenipongeza na mlinitia moyo wakati ninapambana na eneo hili la vyuo vikuu, ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nizungumze kama alivyozungumza Mheshimiwa Tecla, ma-nurse wanahitajika sana na tukumbuke kwamba ma-nurse wanahitajika sana duniani kote sasa hivi. Mheshimiwa Waziri ma-nurse katika dunia hii walifariki wengi sana wakati wa Corona, hata Tanzania ma-nurse wamepungua. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, sasa mjikite kwenye kuona kwamba ma-nurse wetu wanapata elimu ya chuo kikuu tena wawe wengi kama walivyofanya Aga Khan. Aga Khan wameweza kusomesha sasa ma-nurse. Kwa hiyo na sisi Tanzania tujikite katika kuona sasa ma-nurse wanapata elimu na waongezeke, kwa sababu idadi yao imepungua sana. Wewe unajua una zahanati nyingi Tanzania, una vituo vya afya, una hospitali za rufaa, lazima ma-nurse wanaokaa muda mrefu na wagonjwa, waongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudia tena, ninaona sasa Waziri Mheshimiwa Jenista, wewe ni ndugu yangu, siyo tu ndugu wa hivi hivi, unajua wewe ni ndugu yangu, hebu acha legacy kwenye hili eneo la teaching hospitals. Naibu wako alijibu hapa alisema “ooh! Sasa hivi kuna ushirikiano mzuri na nini.” Mimi ninakuomba leo utoe tamko, teaching hospitals; MUHAS, Benjamin pamoja na UDOM, wapate 80% ya kuhusika kwenye zile teaching hospitals zao. Mloganzila ichukuliwe kwa 80% na MUHAS, Benjamin nayo 80% na MUHAS. Maprofesa wako hapo wananisikiliza, wanajua umuhimu wa teaching hospitals kwa vile vyuo vyote vinavyofundisha masomo ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wameongea na mimi nimeongea, mimi ni daktari tu, lakini jana ameongea Mheshimiwa Profesa Muhongo, sasa hata Mheshimiwa Profesa Muhongo mawazo yake kweli hamyachukui? Ameongea Mheshimiwa Dkt. Bashiru. Hebu hakikisha sasa hivi unaacha legacy, watatucheka huko duniani. Ninaomba ulichukue hilo Mheshimiwa Jenista, lifanyie kazi na utoe tamko. (Makofi)

Mheshimiwa Nwenyekiti, nije kwenye hili suala la matumizi ya P2. Mimi nililiongea, sasa kuna watafiti wenzangu wamekaa wamelisema. Kuna Dkt. Jane Muzo anatoka Aga Khan, kuna David Myemba yeye anatoka MUHAS, wametoa madhara 10 ya P2. Kwa ruhusa yako kuna Wabunge hapa hawajui hizo P2, hawazijui kabisa. Hapa nina hizo P2, ninaomba utume mtu aje azichukue, Wabunge wazione, waone watoto wao wakiweka kwenye meza wasione kwamba ni kidonge cha kawaida, wazijue hizi P2. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara yake, Waheshimiwa Wabunge nisikilizeni; hizi P2 kwa sababu zinatumika hovyo bila elimu Mheshimiwa Jenista, ninaomba mtoe elimu ya wazi kabisa. Ninakwambia hiki kizazi kitapotea. Mabadiliko ya mzunguko wa damu na kiharusi, kwa maana wanatumia hovyo, wanaweza wakapata stroke, hii ni kutokana na utafiti wa hawa niliowataja, wanaweza wakapata cancer ya uzazi, mimba zinaweza zikatoka mara kwa mara, wakati mwingine wanapata damu nyingi na wakati mwingine wanapata damu kidogo (spot), wakati mwingine wanapata hata magonjwa ya zinaa.

Kwa hiyo, hili suala nimelizungumza kwa sababu juzi tu kuna mama mmoja alitoka Arusha, wale walioalikwa kwenye chama, akaniambia; “Mheshimiwa hivi mnaongelea hili suala la P2.” Sasa ujue kumbe hata akinamama wameanza kuogopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la P2 tusifanye mzaha Mheshimiwa Jenista, angalia namna gani mtatoa elimu bora ya matumizi hayo kwa sababu inaonekana kuna hasara zaidi kuliko faida. Nimelisema hilo na ninaomba Waziri sasa mtalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ninaweza kumalizia ni kuhusu huu Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote. Kuna hivi vipimo vya CT-Scan, MRI na Dialysis. Walisema wenzangu, hivi vitu tulienda pale Temeke hivi vipimo ni ghali sana, kuanzia shilingi 200,000 na kuendelea. Sasa nimwombe Waziri, hii elimu ya Bima ya Afya kwa Wote bado, itoeni hii elimu ili vipimo hivi watu wote waweze ku-afford. Kukiwa na Bima ya Afya mtu ataweza kupima, lakini otherwise ninawaambia zile mashine ziko pale zitawasaidia tu watu wenye pesa. Kwa hiyo, mtoe elimu ili angalau watu waweze kujua sasa Bima ya Afya kwa Wote itasaidia nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninaomba kwenye tiba asili, Serikali mshirikiane na watu waliotusaidia. Leo kuna mtu anaitwa Shekilindi, amesaidia sana watu wakati wa Corona, dawa ya kisukari, magonjwa ya meno; kuna rafiki yangu mmoja ananiangalia pale, sijui ni Mheshimiwa Mariam Nyoka. Sasa msaidieni huyu, mshikane naye, Shekilindi anasaidia sana, watu wanakwenda pale anasaidia, je, Serikali kwa nini msimhusishe huyu? Mtafute Paul Muhamepamoja na wengine na muwashirikishe Shekilindi aweze kusaidia watu katika magonjwa ya kisukari, meno, pressure na magonjwa mengine. Sasa watu kama hawa wanafanya kazi nzuri, tunawafuata tu wakati wa Corona, hebu muwashirikishe asaidie kufanya hiyo kazi ili tuweze kuepukana na magonjwa haya madogo madogo, msione aibu. Tezi dume watu wanaona aibu, jamani wanaume wenye tezi dume mwende mkamwone Shekilindi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Waziri nikuombe hebu toa tamko zile dawa za kuua vizalia vya malaria, kidogo nimalizie hapo. Zile dawa za kuua vizalia vya malaria, hivi wakurugenzi mliwaaagiza je, wameenda kuchukua? Mpaka lini sisi tutateseka na hii malaria? Waende wakachukue zile dawa pale Kibaha, tutokomeze malaria. Yaani ninyi mnawaagiza humu ndani, lakini wala hawaendi kuchukua. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri hebu pambana nao, waambie, utoe amri wakachukue dawa, zisambaze kwenye sehemu ambazo mbu wanazaliana ili tuepukane na malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)