Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi ya kuchangia Wizara yetu ya Afya. Ni bahati njema kusimama mbele ya Bunge lako leo kuunga mkono mafanikio makubwa ya Wizara yetu ya Afya chini ya mama yetu Mheshimiwa Jenista Mhagama, Naibu Waziri wake na Wakuu wake wa Idara katika Wizara yake na viongozi wote wa Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaanza kwa kuunga mkono hoja. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri akisoma hotuba hapa akiomba shilingi trilioni moja point sita na kidogo. Ameeleza mafanikio makubwa ya bajeti iliyopita na mipango na mikakati ya bajeti ijayo. Mfano, ameelezea vizuri mafanikio ya utalii wa afya. Kwa mara ya kwanza nchi ya Tanzania ambayo ilikuwa inasemwa vibaya huko nyuma, leo kuna watu wanatoka maeneo mbalimbali kuja kutibiwa Tanzania, hayo ni mafanikio makubwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio yetu haya ni lazima sisi wenyewe Watanzania tuendelee kuyapongeza, tuendelee kuyashukuru kwa sababu kwa vyovyote vile hakuna mtu atakayekuja kuongoza nchi moja na siku moja tutapata mafanikio ya kila kitu. Hata hawa wanaotaka kukitoa Chama Cha Mapinduzi na wanaosema vibaya nchi yetu na viongozi wetu, hata ukiwa hapa nchi hii wao hawawezi kumaliza yote kwa wakati mmoja. Changamoto za maendeleo tunasema zinatokea wakati wowote mpaka mwisho wa maisha. Mimi ninamshukuru sana na nitasimama na Rais wangu potelea mbali, liwalo na liwe katika changamoto zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa nachangia masuala ya afya, nataka kusisitiza na kukumbusha maneno ya Sheikh wetu mmoja wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad. Sheikh Walid anasema kwamba anatusisitiza duniani huku unaweza ukaviheshimu vitu vingi sana na kuviogopa, lakini Sheikh Walid anasema jaribu kuheshimu sana moto, maji na mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheikh Walid anasema nawakumbusha Watanzania kwamba nchi hii inaongozwa na mwanamke, sasa msichukulie poa. Kwa hiyo, nami nataka kumkumbusha mtu yeyote mzee mchekea mwezi sisi waswahili tunasema ni muhimu sana ukazingatia hayo kwamba Mheshimiwa Rais wetu ni mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Afya ni mwanamke, ni mama jasiri, umekuja jimboni kwangu wewe na amekuja Mheshimiwa Naibu Waziri kabla hujaja Mheshimiwa Waziri wa Afya, umekuja jimboni kwangu na Mheshimiwa Naibu wako amekuja jimboni kwangu, kabla hujaja Mheshimiwa Waziri wa Afya alikuja Naibu Waziri Mheshimiwa Mollel, akanifanyia siasa kubwa sana pale jimboni kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nimkumbushe ahadi yake moja nzuri aliyonisaidia kufanya pale, lakini wakati amekuja alitembelea pia St. Francis Hospital na alitembelea hospitali yetu ya kansa. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri wakati ule Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya amekuja alikuta changamoto kubwa sana katika hospitali yetu ya Rufaa ya St. Francis na ndiyo maana wakati nauliza swali la nyongeza nilizungumzia kuwashukuru kumleta Mkurugenzi wa Hospitali yetu ya Rufaa mwanajeshi, askari Mr. Fusi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna mafanikio makubwa sana Mheshimiwa Waziri yametokea katika Hospitali yetu ya St. Francis kwa sababu ni hospitali ambayo Serikali inashirikiana na kanisa na sisi mpaka tufikie level ile itakuwa bado hatua ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka niwape pongezi nyingi sana kwa kumleta yule Comrade Fusi ili muone namna ambavyo mnaweza kumuongezea muda wa kubaki pale katika hospitali ile. Mara zote tulikuwa tunasikiliza maoni ya wananchi wakilalamikia Hospitali ya St. Francis Referral ya Ifakara, Malinyi, Ulanga, Mlimba Ifakara yenyewe Mikumi huku kote watu ambao hawawezi kwenda Morogoro katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Morogoro wanatibiwa katika St. Francis Hospital. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nikwambie yale malalamiko ya rushwa, uuzaji wa damu Mr. Fusi amekomesha. Nakutana na wazee wananiambia wanapokelewa na ma-sister pale wa kanisa wanahudumiwa, Mr. Fusi ameboresha kitengo cha mapokezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amejaribu kufanya St. Francis sasa inashirikiana na taasisi nyingine zote na hapa, kitu kikubwa ninachojifunza Mheshimiwa Waziri wa Afya kama kuna maeneo magumu basi ongea na Mheshimiwa Waziri wetu wa Ulinzi hapo awe anakuletea watu kama wale na hizi salamu zangu mzipeleke kwa Comrade CDF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama namtania na kumdanganya Mheshimiwa Waziri wa Afya pita Ifakara sasa hivi uliza mpaka bodaboda wa nje ya hospitali ameshawaita, amewajengea umoja, sasa hivi anawajengea banda pale. Ni mkurugenzi mzuri mmetuletea kama kweli Jeshi letu lina watu wa namna ile basi sehemu zote zenye utata utata hivyo ni vizuri mkapeleka watu kama wale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa hiyo, nakupongeza sana nami mswahili nikitaka kukupongeza Mheshimiwa Waziri nasema wewe ni mwanamke wa mbeko, mwanamke wa ulua, maslahi shamsi, mbeja mwenye umbeja Mwenyezi Mungu aendelee kukujalia baraka tele uendelee kuiongoza Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatusemi yale ambayo tunakuona kwenye vyombo vya habari huko ukimpigania Profesa Janabi, ukiwaapigania viongozi wengine waendelee kuchukua nafasi duniani, lakini kwa mambo makubwa ambayo unayafanya katika sekta yetu ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla sisi katika Jimbo la Kilombero, Halmashauri wa Mji wa Ifakara Mheshimiwa Dkt. Mollel alivyokuja pale Mheshimiwa Waziri, tulitembelea kituo chetu cha Afya ya Kibaoni na Mheshimiwa Naibu Waziri tukamwambia Kituo chetu cha Afya cha Kibaoni ni kituo ambacho kinahudumia watu wengi sana, tunashukuru Serikali tumejenga Kituo kingine cha Mbasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri alituahidi kwamba tutapata shilingi milioni 300 za kupanua Kituo cha Afya cha Kibaoni na kujenga Jengo la Wagonjwa wa Nje mnasema OPD, zile fedha mpaka leo hazijaja Mheshimiwa Naibu Waziri, nakukumbusha hapa mbele ya Mheshimiwa Waziri kwamba ni muhimu sana ukatusaidia zile fedha zikaja Kituo cha Afya cha Kibaoni kikaweza kujengewa Jengo la OPD na kwa namna yoyote ile tukaweza kupata huduma bora zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kushauri kwamba Wizara ya Fedha ipeleke pesa kwa wakati katika Wizara ya Afya kwa maana afya ni bora kuliko magari, wakati mwingine kuliko hata barabara. Kwa hiyo, kama Wizara ya Fedha nimeona kwenye Kamati hapa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Afya anasema uendaji wa fedha katika Wizara yako si mzuri, naomba fedha ziende kwa wakati na hasa kwenye MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hivi hamuwezi kugawa dawa zote hizi zinazotakiwa kuhudumia ni kwa wakati mmoja kwa mfano sisi Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Jimbo la Kilombero, Wilaya ya Kilombero mnaweza mkajua dawa muhimu na magojwa muhimu yanayotukabili wananchi wetu wakapata dawa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naunga mkono hiki kifurushi cha shilingi 168,000 ambacho hata jana nimemkatia mwananchi wangu mmoja wa Kibelege pale. Kukatia hizi bima kama kweli tunajihakikishia tunapata dawa na huduma wananchi wetu wapo tayari, nami nitashiriki kutoa elimu na tunaomba bei ya mpunga mwaka huu iwe nzuri. Bei ya mpunga ikiwa nzuri mwananchi akiuza gunia moja la mpunga atalipia kifurushi cha shilingi 168,000; lakini akienda katika kituo cha afya, akienda katika hospitali basi apate tiba ya kutosha ili aone gunia lake la mpunga limeenda kihalali. Sambamba na wazee wetu wapate tiba nzuri kabisa za kutibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata mafanikio makubwa sana, tumejenga vituo vya afya viwili kwa maana ya Msolwa Station na Mbasa kwa kushirikiana na Madiwani na viongozi wa vijiji na viongozi wa mitaa; tuna zahanati 12 ambazo hizi zinawezekana zipo TAMISEMI Mheshimiwa Waziri wa Afya, lakini tunaomba MSD iwezeshwe. Nafahamu MSD imefanya kazi kubwa sana kwetu, kwa maana kwamba kwa mfano Kituo cha Mbasa kabla hakijaisha vifaa vimekuja. Msolwa Station kule kabla hakijaisha vifaa vimekuja, Hospitali yetu ya Halmashauri ambayo tuna mpango nayo iende kuwa hospitali kubwa zaidi hata baadaye tukipata mkoa mpya imepata vifaa na wataalam. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, wataalam katika hospitali yetu ya halmashauri bado hawatoshi. Naomba sana mtuongezee wataalam katika Hospitali yetu ya Kibelege, na Mheshimiwa Waziri wa Fedha akiwaletea fedha basi mtusaidie kuboresha mpaka tupate fence katika hospitali ile ambayo kwa kweli itasaidia sasa wananchi wa jimbo zima na hata wale watakaoshindwa kutibiwa Ulanga, sasa Malinyi na Mlimba wanaweza wakaja pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusisitiza kwa kumalizia kwamba suala la bima ya afya ni suala la msingi sana na leo Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Afya ametuambia kuhusu kifurushi cha shilingi 168,000. Nami nataka kusisitiza inawezekana shilingi 168,000 imeshushwa kutoka shilingi 300,000. Mimi nilishanunua vifurushi vya shilingi 300,000, shilingi 240,000 sasa tuna shilingi 168000 ndiyo watu wa bima ya afya wameweka class kama SGR ukitaka kupata shilingi 150,000 ukitaka kupanda cha shilingi 100,000; cha ngapi unapata, sisi tutalipia sana watu wetu hiki cha shilingi 168,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kipunguzwe zaidi, lakini la msingi hata kikibaki shilingi 168,000 nataka kusisitiza ni muhimu sana katika afya watu wakapate dawa, watu wakapate huduma kuna baadhi ya maeneo kumekuwa na tabia ya watu wafuate huduma sehemu fulani, hili bado jambo linafanyika sio kwa watu wote, lakini kwa baadhi ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Halmashauri ya Ifakara Dkt. Erasto - DMO wetu amepunguza kwa kiasi kikubwa sana jambo hili, lakini kuna baadhi ya maeneo unakuta kuna malalamiko, nilisema pale Mbasa, naona sasa hivi yameboreshwa huduma imeanza vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mtusaidie dawa za msingi zipatikane. Kwa mfano sisi labda tunasumbuliwa sana na malaria kutokana na bonde letu la maji, dawa za malaria zinazotibu watu wetu zisikosekane, mkifanya utafiti kuna magojwa mtayagundua Ifakara ambayo dawa zile zipatikane kwa bei rahisi, mtu asiende akatibiwa, akapimwa malaria au kichocho ama nini akaambiwa tena dawa mpaka akanunue tena kwa gharama kubwa zaidi, ndiyo maana hata ile bima ya mwanzo ya jamii kule haikufanya kazi vizuri ndiyo hii bima ya shilingi 168,000 itafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, challenge ya kutibu watu ni kubwa, ninajua kisa hata cha Mwalimu Nyerere anasema amekaa nyumbani kwake pale wakati anasikia haya mambo ya kulipa gharama za matibabu na yeye alikuwa anaamini tiba ni bure, anasema ameletwa mtu anaanguka kifafa, lakini anaambiwa hana pesa akalipe, sasa tutafanyaje katika nchi yetu, tunaendelea kuzaa, tunaendelea kuzaliana, tunaendelea kuwa wakulima wazuri, lakini sisi sote tunataka huduma ya afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna gani maskini wa nchi hii, kuna watu maskini kule chini. Mheshimiwa Mbunge unatoka nyumbani unasema leo sitoi hata mia, unakutana na mtu nje hali yake ngumu, akiumwa ukimpeleka hospitalini; juzi nimekutana na mama mmoja ameungua moto mguu kwenda kumcheki tu shilingi 300,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lazima tuangalie kwa ujumla namna gani Mtanzania ambaye hana uwezo hata shilingi 168,000 hii. DC anaweza kupewa mamlaka ama Mkurugenzi wa Halmashauri akijiridhisha na Mganga wa Wilaya akatibiwe kwa barua yao bure tuwasaidie Watanzania wetu hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)