Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa nami nichangie katika hoja hii iliyopo mezani. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuweza kupata nafasi siku ya leo kuja kuchangia hapa. Nami niungane na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kusema kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na njema ambayo ameifanya katika kubadilisha kabisa sekta hii ya afya ambayo ilikuwa na changamoto nyingi, lakini kwa sasa imeweza kuhudumiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Waziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya. Kwa kweli Mheshimiwa Jenista ni kiraka kama Mheshimiwa Rais alivyosema kwamba katika Waheshimiwa Mawaziri kiraka wake mmojawapo ni Mheshimiwa Jenista, kweli umeonekana ni kiraka kwa sababu kila unapowekwa una-fit, hongera sana Mheshimiwa na Peramiho walisikie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo machache tu kwanza kupongeza sana programu ile ya madaktari bingwa wanaotembea katika maeneo na kutoa huduma, kwa kweli huduma ile imekuwa ni njema sana kila wanakokwenda wanaacha faraja kwa wananchi na wengi wanakuwa wana magonjwa pengine ambao wameshindwa kuhudumiwa katika hospitali zingine za kawaida kutokana na kutokuwa na pesa, lakini huduma hii imeweza kuwabeba kwa kiasi kikubwa hongera sana Mheshimiwa Rais kwa kuja na mawazo chanya mawazo ambayo yanagusa mtu wa kawaida kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine napenda tu kukumbushia Wizara, Hospitali ya Kanda ya Bugando ni hospitali ambayo inahudumia karibu mikoa nane, lakini pia nishukuru Serikali kwa kuiteua pia kufanya huduma ya saratani na kuweza kuwekeza pale kwa kuweka jengo kubwa na zuri, kuweka miundombinu ambayo inaweza kuwekewa zile mashine kwa ajili ya saratani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya pale kidogo inasuasua kutokana na mashine zilizopo pale zinashindwa kukidhi mahitaji ya watu na mashine inafanya kazi mpaka masaa 16 na inapokuwa imezidiwa haiwezi tena kuendelea kufanya kazi. Kwa hiyo, unakuta ile azma nzuri ya Serikali ya kusogeza huduma kwa wagonjwa wa kanda ile inakuwa tena haina maana kwa sababu mashine ile inapokuwa imezima wanalazimika kuwapeleka Ocean Road, jambo ambalo ni changamoto kubwa sana kwa wagonjwa katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kwa sababu kumekuwa na ahadi nyingi na mara ya mwisho Waziri Mheshimiwa Jenista alihudhuria pale Mwanza walipokuwa na function yao, pale Bugando na akaahidi kwamba watasaidia katika kuwaletea mashine zingine hasa ile mashine wanayoita linear accelerator inatakiwa sana, nadhani Mheshimiwa Dkt. Mollel anafahamu vizuri sana kwa sababu ni mtaalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana msaidie Hospitali ya Bugando kwa sababu inazidiwa, lakini huduma ile inahitajika sana na wote mlikuwa mnaona tulivyokuwa tunasema kwamba wagonjwa wengi Kanda ya Ziwa wanakuwa wanaonekana pale Ocean Road. Sasa kwa kusogeza huduma basi tuiwezeshe na ile hospitali iweze kufanya kazi kuweza kukidhi mahitaji ambayo yapo, na kwa nyakati tofauti tofauti viongozi kila akienda wanaahidi, kila wakienda wanaahidi. Niombe sana basi ahadi hizi zikatekelezwe ili hospitali ile iweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la wataalam, madaktari bingwa ambao wanapangwa katika hospitai zetu za wilaya wataalam wale wanastahiki zao kulingana na utaalam ule. Sasa anapokwenda wilayani wakati mwingine anapangwa hata kwenye kituo cha afya kwenda kufanya kazi pale, sasa unakuta ile huduma ya ushauri ile consultation fee hawezi kuipata kama anavyopata siku zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ningeomba kwa sababu sasa tunawapeleka mpaka kwenye hospitali za chini waweze kupata stahiki zao kulingana na ujuzi walionao ili tuweze kuwatia moyo katika suala zima la kuona ni namna gani tunaweza pia kuwatia moyo hata wanapokwenda kutoa huduma sehemu ambazo ni za chini kabisa katika huduma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kutoa pongezi kwa Wizara katika ile huduma wanayoitoa kwa kutoa mtoto tumboni, nadhani ni kwa uzazi wa operation. Naomba nitoe ushauri hapa kuongezeka kwa huduma hizi sioni kama zina tija sana kwa sababu sasa hivi vijana wengi wanashawishika kujifungua kwa njia ya operation, anaogopa kujifungua kwa njia ya kawaida. Kwa hiyo kadri tunavyoongeza hizo huduma nadhani pia tunaleta ushawishi na anapojifungua kwa operation nadhani kuna limit ya watoto na sidhani kama Tanzania tumefikia wakati na kuwa na watoto labda mmoja au wawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningeomba ushauri zaidi utolewe kwa mabinti ni namna gani anaweza akabeba ujauzito, akafanya mazoezi gani na katika kujifungua akajifungua kawaida ili tuwaepushe na uzazi wa operation kwa sababu uzazi wa operation una limit utakwenda watoto wawili, watatu halafu basi huwezi kuongeza tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana kwa sababu hapa inaonekana huduma zimeongezeka kutoka 388; mwaka 2021 mpaka kufikia 577 Machi, 2025. Kwa hiyo, bado pia ni nzuri imeongezeka, lakini haina tija kwa watu wetu kwa sababu kuna limitation tunaweza tukawa tunapunguza idadi yetu kwa kuweka kipingamizi hicho cha wazazi kujifungua kwa operation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala la watoto wenye uzito pungufu ambao nao wanaongezeka kutoka 80 mpaka kufikia 365. Huduma hii inapatikana katika hospitali zetu za wilaya 200; umesema kwenye taarifa katika hospitali zetu za wilaya 318 bado pia ushauri upo pale pale kwenye masuala ya lishe inakuwaje mtoto anazaliwa akiwa na upungufu wa uzito? Tunahitaji kuwafundisha watu wetu pia katika suala zima la lishe, bila kufanya hivyo tutazaa watoto wenye uzito pungufu, lakini pia afya zao zinakuwa siyo nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado nalo hili nishauri wakunga wetu, manesi wetu wanalo jukumu kubwa la kushauri sana katika suala zima la lishe ili tuweze kuona ni jinsi gani tunaweza kuepukana na watoto hawa wanaozaliwa na upungufu mzito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie utalii wa tiba; kwa kweli nimpongeze na hongera nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika zile hospitali za kanda na hospitali za rufaa. Tumeona nchi zaidi ya nane wanakuja kutibiwa hapa, kwa hiyo, kama tunaweza kupata watu kutoka nje maana yake huduma zetu hapa ni nzuri, huduma zetu zinafaa na mpaka zinawavutia nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niweze tu kupongeza na kusema kwamba tuongeze bidii katika kuboresha huduma hizi ili tuweze kupata wagonjwa wengi wanaokuja kwa kutibiwa hapa ambao tunaita ni tiba ya utalii ambayo inasaidia sana katika kuleta pia pesa za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la matibabu ya Waheshimiwa Wabunge nje ya nchi. Nadhani tuna hospitali yetu kule India ambayo mara nyingi tunaenda, naomba nishauri sana, Serikali ione namna ya kuongeza nchi zingine ambazo zinaweza kuleta kutibu wagonjwa badala ya kujikita katika hospitali moja ya India. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema India ni mabingwa kweli, lakini pale unapokwenda msongamano wa watu ni mkubwa mno, kwa hiyo, kunakuwa na changamoto pia katika suala zima la kupata matibabu. Kwa hiyo, ningeomba sana hili lifanyiwe kazi ili watu waweze kupata option ya kwenda kutibiwa katika maeneo mengine kutokana na hali halisi ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niongelee suala la jimboni kwangu tunacho Kituo cha Afya cha Buzuruga, kituo kile ni kikubwa sana kwa sasa kinafanya kazi kama hospitali ya wilaya na tunatambua hasa katika vituo vya afya wagonjwa wanatakiwa walau 10,000 hawazidi sana hapo, lakini kituo kile kwa sasa kinatibu watu zaidi ya 200,000 kwa mwaka sasa uone kwamba ni namna gani hapo tunavyofanya siyo kwa mwaka kwa mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tuone ni namna gani tunaweza kukipandisha hadi walau hata katika kutoa huduma za pale waweze kupata vifaa tiba na mambo mengine ya dawa sawa na hospitali ya wilaya kwa sababu wanatibu wagonjwa zaidi ya uwezo wake na kituo kile ni kikubwa na ni tegemeo kubwa sana katika wilaya, lakini pia katika kata za jirani ambazo zinatoka katika wilaya jirani ya Nyamagana, niombe hili kwa sababu imekuwa na changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la kutibiwa kwa wazee, tumesema wazee kweli wanatibiwa bure, lakini pia sheria inge-categories ni wazee wa aina gani kuna? Kuna wazee wengine wana uwezo wa kuweza kujitibisha, lakini kuna wazee wengine ambao hawana uwezo kabisa, lakini unakuta naye pia anapata changamoto akifika pale hapati matibabu anayostahili kwa sababu tu pengine ya kutoelewa watoa huduma au namna ya sheria yetu ilivyokaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuweze ku-categories kuona ni wazee wapi? Kwa sababu unaweza ukasema kuanzia miaka 60, miaka 60 wengi tu hata ni miaka zaidi ya 60 naweza nikasema na mimi nitibiwe bure, lakini kumbe nina uwezo wa kufanya hivyo. Kwa hiyo, tuangalie na tuweze ku-categories ni wapi ambao wanastahili kuweza kufanyiwa hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe kwa Wizara, tunahitaji pia kuwa na ambulance katika vituo vyetu vya afya hatuna ambulance katika maeneo hayo tuliyonayo kidogo imechoka na tuna vituo vya afya vitano. Sasa katika vituo hivyo vyote kama ambulance ni moja na nyingine inasuasua kidogo, ni changamoto, niombe sana haya ili tuweze kuona tunakwendaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais ambaye amepewa tuzo ya Bill Gate Keeper wanasema ya goalkeeper ambayo amepunguza vifo vya kinamama wajawazito. Kwa kweli nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu tulikuwa na vifo vingi na vimeshuka mpaka 101. Niombe tu watumishi wetu waendelee kufanya kazi kwa bidi, vifo vipungue walau tubaki na digit mbili au moja ikiwezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, ameshaonesha uhodari na kupewa tuzo, basi tuendelee kupunguza vifo hivyo ili tuweze kuwa na huduma nzuri kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na napongeza kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)