Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa ruhusa yako hii sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue fursa hii ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya na hivi sasa nimesimama hapa ili nichangie Wizara ya Afya. Ninamshukuru Waziri Mheshimiwa Jenista pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Dkt. Mollel, Mawaziri hawa wanafanya kazi vizuri sana na wanaisimamia hii Wizara ya Afya hasa katika hospitali zetu humu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kuna baadhi ya mambo mengi humu hospitalini yamepungua kweli kutokana na hii Wizara jinsi inavyofanya kazi, lakini kuna baadhi ya mambo mengine bado yapo na yanaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa katika ajenda yangu nataka nizungumzie kuhusu afya ya jamii; afya ya jamii bado kabisa kuna baadhi ya hospitali ukienda hata kama unayo ile bima ya afya bado wanataka uwape na chenji kidogo ndipo unapopata zile dawa, kama si hivyo huwezi ukapata dawa, maana ile bima ya afya wanasema mpaka sasa hivi wanasema dawa zetu hazikidhi kutokana na hii bima ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna baadhi ya wananchi wetu humu nchini, wanyonge na maskini wana bima zao za kinyonge kabisa, wale ndiyo hawapati dawa kabisa, utamuona mtu anatoka hospitali na unyonge hana pesa ya kwenda kujihudumia, yale maradhi yanazidi kumuumiza. Kwa hiyo, Waheshimiwa Mawaziri, naishauri Serikali hili suala la bima lisimamiwe na liweze kufanya kazi vizuri humu katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea kuna tiba ya afya humu nchini, hasa tiba ya jamii, tiba hii ya jamii wenzangu humu wameizungumzia, kuna baadhi ya hospitali zile kubwa zinawatoa madaktari kwenda kupima afya ya jamii katika maeneo yetu humu nchini. Mimi ninaishukuru sana Serikali yangu hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yetu pia kule Zanzibar kwa kulisimamia hili la baadhi ya kwenda kuwapima afya ya jamii watu huko wanakokaa maeneo yao, kwa sababu wenzetu kule wanakaa, wanafanya kazi zao, lakini kumbe wana maradhi ndani kwa ndani yanawaumiza hawajui, lakini ninapokwenda kule afya ya jamii wanapopimwa wanagundulika na yale maradhi, hasa pressure, sukari na baadhi ya maradhi mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nishukuru fursa hii, kwa kufanya hivi wazidi kufanya vizuri ili hawa wananchi wawatoe kule nchini, kule nje ili waweze kwenda kutibiwa katika hospitali zile na wanapogundulika kama wana maradhi madogomadogo basi kama kuna dawa wanakuwa wanapewa dawa bure. Kwanza nishukuru sana katika Serikali zetu hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea kuna maradhi ya sukari, pressure na shinikizo la damu, maradhi haya yanakuwa siyo ya kuambukiza, lakini haya maradhi sugu, baadhi ya maradhi haya wengine tuliokuwa nayo humu, basi kama kipindi hiki cha baridi unapata taabu sana. Haya hayataki ufurahi, haya hayataki unune, hayataki baridi sana, hayataki joto sana. Haya maradhi ni maradhi sugu. Vyovyote unavyoishi maradhi haya basi utakuta yanakuathiri katika mwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba kuna baadhi ya hospitali ukienda unakuta dawa, lakini kuna baadhi ya hospitali zingine wanakuwa hawana dawa. Wale wananchi wetu kule wanapata taabu, wenye maradhi haya ya sukari na shinikizo la damu wanakuwa wanaathirika na wanarudi nyumbani wengine wanafikia kufariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nakuomba hili suala mlisimamie ili hawa wananchi wetu waweze kwenda kutibiwa maradhi haya ya sukari, pressure pamoja na shinikizo la damu, maana baridi hii tena watu wanaanza kuganda damu mwilini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, hili ndilo ninaloliomba kwa sasa hivi kuishauri Serikali yangu ifanyie kazi wagonjwa wetu wa sukari na pressure wajisikie wawe tayari kufanyiwa matibabu na wajione kwamba hivi sasa niko afadhali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya hospitali, kuna nchi za wenzetu hawa humo nchini wanakuwa wanahudumia sana wake zao, wanahudumia sana wake zao hasa wanapokuwa wajawazito, wanawaendeleza wake zao mpaka wanafika kujifungua, wanawasimamia mpaka wanafika kwenda kujifungua kule hospitali wanakwenda wale wanaume, lakini hapa nchini baadhi yetu hawana mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu akishampiga mimba mtoto mwanamke hata kama mkewe basi hawezi kumshughulikia, anamuaacha kama alivyo, umefika muda Mungu kamsalimu salama anazaa imekuwa pale basi, lakini ninakwambia hili suala nalo vilevile lisimamiwe hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaume wapewe elimu, waweze kwenda kuwasimamia wake zao hasa wakati wa kwenda kujifungua. Yule mtoto anapotoka kwenye tumbo la yule mama basi baba awepo pale amuone jinsi anavyoathirika yule mwanamke, imuingie imani ya kuweza kukaa na mkewe vizuri. Wanaume humu wanatutelekeza, tunapochukua mimba hatuwezi kushughulikiwa na wanaume wetu, hata kama ile dawa basi hawezi, ukimwambia mume wangu mimi sina dawa nisaidie nipate angalau hii dawa ya damu tu mwilini, anakwambia mimi pesa sina! Kwa nini umeenda shirikisha lile suala mle ndani, kwa nini? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hili lisimamieni muweze kulifanyia kazi, wanawake waweze kuzaa vizuri na wanaume wao kule hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ninalotaka kuzungumzia, kuna baadhi ya hospitali, kuna maradhi, kuna ushirikishwaji kwenye hatua za watoto. Watoto wetu humu nchini baadhi, hasa wale watoto njiti, watoto njiti wakishazaliwa wale wanataka huduma nzuri sana, ukifanya masihara mtoto yule atakwenda na maji. Muda wote wakishazaliwa wanakuwa wabovu watoto wale, hawawi wazima na ndiyo tunapoomba walelewe kule hospitali, wanapolelewa kule hospitali, kama kwa baadhi ya miezi miwili/mitatu kisha wale watoto wapewe wazee wao waende nao nyumbani kwa kwenda kumfanyia huduma nyingine, pale inakuwa afadhali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto njiti akishazaliwa akipewa mzazi inakuwa shida na hili ndilo lililokuwepo, mtu akishamzaa mtoto wake njiti anakaa wiki tu hospitali na huko nyuma wanakaa zaidi ya miezi mitatu kisha ndipo mtoto wake anapewa. Kwa hiyo, nashauri hili nalo Serikali ilisimamie suala la watoto njiti ili waweze na wao kupata uhai, waishi kama sisi wazee wao waje wafanye kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja asilimia mia moja, ahsante sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, ahsante sana Mwenyekiti kwa ruhusa yako. (Makofi)