Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza maswali hapa wakati Wabunge wanachangia, nikajiuliza swali moja, hivi ikitokea kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekataa kupitisha bajeti ya Wizara ya Afya hivi kutatokea nini? Tutaenda kugombea au tutakaa humu Bungeni? Maana yake si wananchi wote huko watapata matatizo? Kwa hiyo, hii ni Wizara ambayo inaitwa mtakuja, kwa hiyo, haina namna yoyote ya kutounga mkono Wizara ya Afya ili watu wetu waendelee kupata afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza mimi naunga mkono hii Wizara kabla sijaendelea kwa sababu siwezi kwenda huko wakaniambia watu wamekufa huko tena nikaanza kupiga simu kwa Mheshimiwa Jenista, haiwezekani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Jenista na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Dkt. Mollel, Katibu Mkuu, Mganga Mkuu wa Serikali na watumishi wote wa Wizara ya Afya. Kimsingi, sasa sijui Mheshimiwa Rais huwa anaona, huwa anaona nikimweka huyu na huyu watakuwa sawa, maana Mheshimiwa Dkt. Mollel yeye mawazo yake yote wala siyo kutafuta madaraka, mawazo yake yote Mheshimiwa Dkt. Mollel ni namna ya kutafsiri vifungu vya dawa na vifungu vya afya ndiyo akili yake. Namna umpigie simu, ukimpigia simu Mheshimiwa Dkt. Mollel ya kumsaidia mtu anaona ndiyo wito wake, hapo hapo atapiga simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ameingia dada yangu Mheshimiwa Jenista na yeye ni hivyo hivyo. Kwa kweli mioyo yao labda Mungu ndiye anayejua kwenye mipango yao. Wana mioyo ya ki-Mungu tunawaombea waendelee kuwepo watusaidie. Kwa kweli tunaomba watu wa majimbo yenu wasikie Wabunge tunasema nini, wasiwasumbue wawaache mje mtusaidie nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, kwenye Jimbo langu ninayo Hospitali ya Wilaya ambayo imejengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 4.6 na sasa tumepewa shilingi milioni 680; shilingi milioni 680 itaenda kumaliza Hospitali ya Butiama ya Wilaya, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ilikuwa imekwama kidogo, sasa itaenda kumalizika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata vituo viwili vya afya, Kituo cha Mgeta na Kituo cha Unyali, vyote vina shilingi bilioni moja na milioni mia mbili na kitu, lakini Kituo cha Afya cha Unyali hakijakamilika na kitaendelea kukamilika, tumeomba Serikali itakimalizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, hizi shilingi milioni 250 zilizotoka sasa hivi nimepata Kituo kipya cha Afya cha Mihingo, kiukweli watu wale walikuwa na tatizo kubwa. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kupata hizi fedha ili ziweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mollel, wewe ulikuja juzi, ulikuja Mara, wakati Katibu Mkuu wa CCM, wa chama chetu na Mgombea Mwenza wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Nchimbi alipokuja kukagua utekelezaji wa Ilani kwenye Hospitali ya Rufaa Kwangwa, Mheshimiwa Dkt. Mollel ulipata maelekezo kwamba ile hospitali, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameipeleka mpaka imebaki ni kama 35%, tunaomba hayo maeneo yaliyobaki ya ujenzi na vifaatiba vilivyopo pale mmalizie. Maagizo yote ulipewa na unayajua. Tunataka tupate hospitali ile, ikamilike ili watu wetu wa Mkoa wa Mara watibiwe palepale katika Hospitali ya Kanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza mambo mengi sana kuhusu vifurushi vya bima ya afya. Nilikuwa napitia kifurushi kimoja kimoja, nikapitia kifurushi cha Tarangire, yaani watu umri wa miaka 18 hadi 35 wanasema ni shilingi 160,000; miaka 36 hadi 59 shilingi 192,000; miaka 60 na kuendelea mpaka miaka 115 maana sijasikia mtu amefika miaka 120 ni 115 nimewahi kusikia ni shilingi 240,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi vifurushi vya Tarangire vitatusaidia sisi kutibiwa ndani ya nchi yetu. Sasa kuna watu wanazungumza ukubwa wa fedha kwa vifurushi, lakini nataka niwaambie sijui kama mnaenda hospitali. Juzi nimeenda matibabu ya mtu wa kawaida tu ana pressure kidogo tu dawa zake nimekuja private kununua wameniambia shilingi 240,000; ukienda pale Hospitali ya Benjamin Mkapa dawa hizo hizo ni shilingi 130,000. Ukiwa na bima ya afya, ukienda hospitali matibabu yako yanakurahisishia kuishi. Kwa hiyo, tusiangalie ukubwa wa hivi vifurushi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kifurushi kingine kinaitwa Mikumi, hiki kina shilingi 240,000 kutoka miaka 0 hadi 17, miaka 18 hadi 35 shilingi 432,000, miaka 36 hadi 59 shilingi 540,000, miaka 60 na kuendelea ni shilingi 708,000. Hivi vya Tarangire havina magonjwa yenye utata, hivi vya Mikumi vina magonjwa yenye utata, una tatizo la figo, una tatizo la moyo, una tatizo la magonjwa sugu inakusaidia. Sasa mimi sioni ukubwa wa fedha hiyo, watu waelimishwe, kwa sababu kuna jamaa mmoja aliniambia anataka kwenda India na kwenda India private lazima uwe na shilingi milioni 30 au shilingi milioni 20. Hivi kweli shilingi milioni 20 kwa hizi hela ambazo zimetajwa hapa ni kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kifurushi ambacho amekitaja hapa ambacho ni Tanzanite kinakuruhusu kwenda kutibiwa nje, miaka 0 hadi 17 shilingi 1,500,000, miaka 18 hadi 35 shilingi 2,700,000, miaka 36 hadi 59 shilingi 2,800,000, umri wa miaka 60 hadi 115 shilingi 6,700,000. Hivi kweli kwenda India kama watakupeleka kwa shilingi 6,700,000 si ni bure? Bure kabisa! Mimi nimetoka India juzi, wakikuacha tu bima ya afya, wakikutoa nje, kile chakula cha nje tu, unakula pale wiki mbili unakula karibu shilingi milioni 20, milioni ngapi.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa wapi?

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Noah.
TAARIFA

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Getere kwa mchango wake mzuri, lakini afahamu kwamba kuna maskini wa maskini katika vijiji vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa asilinganishe na matajiri wenye uwezo wa kulipa vifurushi vikubwa na ndiyo maana michango ya Wabunge inaelekea kwamba kazi nzuri inayofanywa na Wizara iendelee kufanya kazi nzuri ya kuangalia na watu maskini wa maskini, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere, unapokea mchango wa Mheshimiwa Noah?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, aah, sasa unajua hapa duniani tumeumbwa watu tofauti tofauti, na ninaipokea taarifa yake, siwezi kusema ninamkatili, lakini na yeye aelewe hapa duniani tumeumbwa watu tofauti, ukisema kwenda India tutumie shilingi 500,000, tukisema kwenda India tutumie shilingi 100,000 tutafia hapa wote. Ni lazima, kwa mfano kwa hivyo vifurushi vilivyowekwa ninaamini kwamba shilingi 6,700,000 Serikali imeweka wakikupeleka India kwa shilingi milioni labda 25 au 30, hiki ni kifurushi wamekuwekea tu, sicho kinachokutunza wewe.

Kwa hiyo, mimi naomba watu waelewe kwamba lazima tujikite kwenye bima ya afya ili tuendelee kuishi, vinginevyo tutafia hapa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nijue kifurushi cha bima ya afya kwa Wabunge, bima ya afya kwa Bunge ina upendeleo fulani. Serikali inaisha mwezi wa kumi na moja, bima ya afya ya hapa inaisha mwezi wa saba, yaani wewe Mbunge uko kwenye harakati za kugombea bima ya afya imeisha, ukiugua unafia hapo, hapana. Bima ya afya ya Wabunge na yenyewe iende kwenye mwezi wa kumi na moja ifike kama Serikali ilivyo. Haiwezekani mimi niko kwenye kampeni, ninapambana, nimepata matatizo ya afya ninafia hapa, hakuna bima ya afya inaisha mwezi wa saba, haiwezekani jamani.

Kwa hiyo, lazima tuipeleke huko mbele ili na sisi tuweze kupata bima ya afya, tuendelee kuishi, lakini vinginevyo Serikali iendelee kufanya marekebisho, iendelee kuboresha bima ya afya, ikae vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)