Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Afya. Kwanza kabisa niunge bajeti mkono kwa sababu ni bajeti nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amewekeza kwa kiwango kikubwa sana kwenye Wizara hii ya Afya, amewekeza kwa sababu kwa kiwango kikubwa ameweza kuweka vifaatiba katika kila hospitali, vituo vya afya mpaka zahanati. Leo hii katika zahanati zetu kuna vifaatiba, kwenye vituo vya afya kuna vifaatiba, lakini ukija kwenye hospitali zetu za Wilaya na Mikoa tumepata vifaatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watumishi wote wa Wizara hii kwa sababu wanaitendea haki Wizara ya Afya, hongereni sana na tunawatakia kila la kheri muendelee kuchapa kazi bila kuchoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. Kwa mara ya kwanza leo katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Manyara tumepata mashine kwa ajili ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo. Hii ni hatua ya pekee kwa sababu wagonjwa wetu wengi. Wananchi wa Mkoa wa Manyara wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kuja hospitali ya Benjamini Mkapa na wengine imewalazimu kuhama makazi kwa sababu ya kufanya dialysis katika hospitali ya Benjamin Mkapa. Kwa hiyo, kuletwa kwa huduma hii katika mkoa wetu imekwenda kuwapunguzia gharama wananchi wa Mkoa wa Manyara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, gharama ya nauli kuja Benjamin Mkapa, lakini wengine walikuwa wanaenda kupangisha nyumba, hivyo gharama hizo zinakwenda kuondoka na wananchi wanakwenda kupata huduma ya dialysis katika Hospitali ya Mkoa wa Manyara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kwa sasa hivi kumekuwa na mlipuko au kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa ya figo, magonjwa ya kansa kwa wananchi walio wengi. Mimi ninaiomba sasa Wizara, kwa kuwa tumefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye vifaatiba na kujenga hospitali za kutosha, vituo vya afya vya kutosha sasa ione namna gani inakwenda kuweka mkakati. Kwanza, kujua kwa nini kumetokea ongezeko kubwa la magonjwa ya figo pamoja na kansa ili wananchi waweze kupewa elimu ya kutosha kuepukana na ugonjwa huu wa kansa na figo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani tulijua kwamba ugonjwa wa figo ni kwa ajili ya wazee, lakini sasa hivi watoto wadogo waliozaliwa wanapata pia tatizo la figo. Kwa hiyo, hili lazima kama Serikali iweke mkakati wa pekee na kuweka uwekezaji mkubwa kugundua chanzo ni nini na namna ya kuondokana na huu ugonjwa kwa sababu umeendelea kuongezeka kwa kasi kubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ningependa kabisa Serikali ione namna gani pamoja na kwamba kuna ongezeko kubwa la haya magonjwa, lakini ione kwamba kuna uwezekano mkubwa wa lifestyle ya kwetu sasa tunavyoishi nayo, yawezekana vyakula tunavyovitumia na matumizi mengi ya dawa ndiyo maana sasa ugonjwa huu umeendelea kuongezeka siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa Serikali ifanye uchunguzi hasa kwenye vyakula. Mfano tunatumia dawa kwenye mboga mboga, mazao na matunda, hebu Serikali iweke utafiti pale tuone kwamba zile dawa zinazotumika kwenye mboga mboga huenda ndiyo tatizo kubwa. Pia dawa zinazotumika yawezekana wafanyabiashara walio wengi kwa sababu ya tamaa na kukosa uaminifu, dawa inapigwa ndani ya wiki moja mtu anaenda kuchuma mboga anapeleka sokoni, anauza, halafu mboga unaenda kupika ina harufu ya dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili liangaliwe na hili linawezekana pale ambapo Serikali ione namna ya kuweka vifaa vya kupima pale sokoni ili kuona kama kuna ubora wa vyakula tunavyokwenda kuvitumia na kama chakula kina sumu basi kisitumike. Hili linawezekana kwa sababu Serikali imewekeza sana kwenye vifaatiba. Badala ya kuendelea kutibu basi tuanze kwenye kuzuia kwanza, kuanzia kwenye vyakula tunavyotumia maeneo ya sokoni kama mboga mboga pamoja na matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee sasa kwenye hospitali yetu ya mkoa; Hospitali ya Mkoa wa Manyara tumepata CT-Scan lakini CT-Scan tuliyonayo haina mtu wa radiology hivyo inasababisha kwamba watu wengi wanafanya vipimo, lakini hawapati majibu kwa muda kwa sababu mpaka watafute mtaalam wa kusoma yale majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni uwekezaji mkubwa umefanyika, tuna CT-Scan lakini haifanyi kazi kama inavyotakiwa. Kwa hiyo, niombe Serikali ituletee mtaalam wa radiology pale mkoani ili wananchi waendelee kupata huduma ya radiology badala ya kuendelea kuhangaika kwenda Mount Meru na Benjamin Mkapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa kujenga hospitali ya mkoa. Niombe sasa Hospitali yetu ya Mkoa wa Manyara ikamilike kwa sababu bado haijafika kuitwa hadhi ya Hospitali ya Mkoa kwa sababu tuna upungufu mkubwa wa majengo. Hili nimeshalisemea mara nyingi hapa ndani, ninaomba tena niliseme kwa mara nyingine tena. Tuna upungufu wa majengo, sasa hivi tuna jengo la maternity ward na jengo la utawala tu hivyo imewalazimu hata jengo la utawala kutumika kama ward. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sasa fedha zipelekwe ili majengo yakamilike. Jengo la ICU likamilike kwa sababu ina umuhimu mkubwa hasa kwa wagonjwa wanaofika hatua ya kwenda ICU. Jengo hili la ICU limesimama kwa muda mrefu na hakuna mfumo wa gesi. Kwa hiyo, niombe fedha zipelekwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia jengo la damu salama na jengo la emergency bado kuweka mfumo wa maji na mfumo wa floor pamoja na jengo la idara ya watoto, jengo la upasuaji na wodi ya wanaume na wanawake. Kwa hiyo, niombe sana majengo haya yakamilishwe. Fedha zipelekwe kwa wakati ili basi hospitali yetu ya mkoa ifanye kazi kama Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara badala ya kuendelea kuwasumbua wagonjwa kwenda kutafuata huduma kubwa kubwa katika hospitali kubwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna upungufu mkubwa sana wa madaktari. Kama nilivyokwisha kusema kwamba tuna upungufu wa watumishi kuanzia mtaalam wa radiology, lakini pia manesi hatuna wa kutosha pale kwenye hospitali yetu ya mkoa ukilinganisha na population iliyopo katika hospitali yetu ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatuna madaktari bingwa wa mifupa na madaktari wa magonjwa ya ndani kwani mpaka sasa tuna daktari mmoja tu. Kwa hiyo, Serikali ione namna ya kutuongezea daktari. Pia madaktari wa watoto nao waongezeke ili huduma ziweze kutolewa kwa wagonjwa bila kuwasumbua wagonjwa kwenda kutafuta matibabu katika hospitali nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Hospitali yetu ya Mirembe. Ninaomba nikumbushie hapa Hospitali yetu ya Mirembe iongezewe watumishi. Kulingana na uhitaji uliopo kwa sasa watumishi ni wachache na hawatoshelezi. Pia hata majengo yaliyopo ni chakavu. Kwa hiyo, Serikali ijielekeze kuangalia namna ya kuboresha yale majengo ili huduma itolewe vizuri katika hospitali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona taa imewaka basi niunge mkono hoja kwa mara nyingine na pia nishukuru sana. Niwatakie kila la kheri Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwenye uchaguzi mkashinde na mrudi hapa mkiendelea kuwatumikia wananchi. (Makofi)