Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya kwa Wizara yetu ya Afya. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa fedha nyingi kwenye sekta hii ya afya ambayo imeleta tija kubwa sana kwa wananchi wetu. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze mtani wangu, dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwa kweli yeye ni mchapakazi. Ninakumbuka tangu akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu alifanya kazi kubwa sana na hasa wakati ule tukiwa na kadhia kubwa ya mafuriko na mvua za El-Nino kule Kilwa alitusaidia sana kuweza kutatua changamoto mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amefika huku vilevile amefanya kazi kubwa sana. Ninakumbuka kama zaidi ya mara mbili wananchi wangu walikwama kutoa maiti zao pale Muhimbili, aliweza kutoa ushirikiano mkubwa na tatizo lile lilitatuliwa. Tuliweza kuchukua miili ya ndugu zetu tukaweza kwenda kuzika kwa wakati. Ninampongeza sana na ninamshukuru sana, aendelee na moyo huo huo. Ni imani yangu wananchi wa Peramiho wanaliona hilo, watampa kura zote za ndiyo ili apate miaka mingine mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Mollel, tulishirikiana vizuri kuwaleta madaktari bingwa wa lile kundi la Madaktari wa Mama Samia na kwa kweli kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi katika Hospitali ya Kipatimu iliyoko jimboni kwangu walifanya kazi kubwa sana ya kuwasaidia wananchi wetu. Huduma zilizotolewa zilikuwa hazipatikani pale, lakini kwa kushirikiana na madaktari wa pale na wa Wilaya yetu ya Kilwa na Mkoa wa Lindi, kazi ilifanyika nzuri na watu walifurahi sana. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa katika kutatua changamoto mbalimbali za sekta hii na kufanya ufanisi uongezeke na tija kubwa ipatikane katika sekta ya afya, nilikuwa ninaomba nishauri mambo yafuatayo; kwanza kumekuwa na shida kidogo kwenye vifaa vile vikubwa vikubwa vya kitaalam kama MRI na CT-Scan. Bado kuna changamoto; kwa mfano hizi MRI zimekuwa zikitolewa mpaka katika level ya kanda. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninafikiri kuna umuhimu mkubwa wa hivi vifaa vya MRI kuweza kupelekwa katika hospitali za mikoa. Hii ni kwa sababu leo wananchi wengi wa vijijini kwetu wanasumbuka sana kuweza kufuata huduma hizi katika hospitali kubwa zilizopo Jijini Dar es Salaam, Benjamin Mkapa hapa na hospitali nyingine kubwa kubwa.
 Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hospitali nyingi kwa mfano za mikoa hizo hakuna hivyo vifaa. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba Serikali iangalie hilo jambo ikiwezekana hospitali za mikoa watu wapate nafuu ya kufika kule kupata huduma kubwa kubwa kama hizo ili hatimaye waweze kutatuliwa changamoto zao za maradhi. CT-Scan pia nilikuwa ninaomba zipelekwe mpaka wilayani ili tuwe na uhakika wa kuwatibu wananchi wetu kwa kutumia hii mitambo ya CT-Scan. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na changamoto kubwa ya ugonjwa wa figo na wagonjwa wengi wamelazimika kufuata mashine za dialysis katika hospitali kubwa. Matokeo yake wengi wamekuwa aidha wanashindwa au wanazifikia kwa kuchelewa sana au katika mazingira magumu sana kwa sababu zipo katika hospitali kubwa tu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba ugonjwa wa figo sasa hivi umekuwa ni ugonjwa mkubwa mno kuliko ilivyowahi kutokea huko siku za nyuma. Kwa maana hiyo nilikuwa ninashauri Serikali ipeleke mashine za kupima dialysis mpaka katika hospitali za mikoa na wilaya ili wananchi wetu wasisumbuke kwenda mbali.
 Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu anatoka Nandete huko Kilwa anakwenda mpaka Dar es Salaam - Muhimbili au Mloganzila kufuata huduma hii, kwa kweli inakuwa ni shida. Pia kumekuwa na gharama kubwa sana ya kutibu huu ugonjwa. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba Serikali itengeneze programu kama ilivyokuwa kwa wagonjwa wa kifua kikuu au kama ilivyokuwa kwa wagonjwa wa saratani ambao wanapata huduma hii bure na huduma hii ya kutibu ugonjwa wa figo pia itolewe bure. Katika eneo hili nilikuwa ninaishauri Serikali itafute chanzo cha mapato kwa ajili ya ku-subsidize hii huduma ya tiba ya figo. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikiendelea kuchangia niende kwenye NHIF na vifurushi vyake. Ninafahamu kwamba kuna vifurushi takribani vitano; kuna kifurushi cha Tarangire ambacho kinaanzia shilingi 168,000; Ngorongoro shilingi 240,000; kuna cha Mikumi kinaanzia shilingi 432,000; kuna cha Serengeti kinaanzia shilingi 660,000 lakini kipo cha Tanzanite ambacho hiki kinapeleka hadi wagonjwa nje ya nchi ambacho kinaanzia shilingi 1,500,000 mpaka 11,493,000.
 Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi kwanza nishukuru na kuipongeza Serikali wameweza kupunguza viwango vya kuanzia vya chini kabisa vya hivi vifurushi vya bima ya afya. Ninakumbuka kabla ya mwezi Mei mwaka huu, hiki kifurushi ambacho tunalipia shilingi 168,000 kilikuwa kinatolewa kwa shilingi 192,000 (hiki cha Tarangire). Pia kile cha chini kabisa cha Ngorongoro kilikuwa kinatolewa kwa shilingi 360,000 lakini leo kinatolewa kwa shilingi 240,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Serikali imepunguza, lakini ninafikiri bado tunao wananchi ambao hawawezi kumudu hizi gharama. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba tuangalie uwezo wa watu pia ikiwezekana tupunguze hadi kiwango cha chini kabisa chini ya hapo ili wananchi wetu waweze kunufaika na hizi huduma ambazo zinatolewa kwenye hivi vifurushi. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nilikuwa ninaomba kwamba kwa wazee tusifike mahali wazee wakatuona kama vile wao kundi lao ni kama kundi ambalo limepata laana au kama kundi ambalo limepata balaa au kama vile hatuwataki kwa sababu viwango vinakwenda kwa mujibu wa umri. Kadri umri unavyopanda na viwango vinapanda. Kwa hiyo, wazee wanatibiwa kwa gharama kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilifikiri katika eneo hili Serikali pia iangalie ile programu ambayo inakwenda kwenye dialysis pia waiangalie kwenye bima ya afya. Ikiwezekana huu mfuko uwe unapewa subsidies kutokana na chanzo fulani ambacho tutakibuni ili kuweza kuwasaidia wazee, ili hawa wazee ambao wamelitumikia Taifa hili kwa miaka mingi na wamezalisha sana tu wakulima, wafanyakazi na wengine nao waweze kunufaika au kuishi vizuri katika uzee wao. Tutakuwa tumewasaidia sana wazee wetu. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa ninaomba hii taasisi yetu ya NHIF imekopesha maeneo mengi sana kwa ajili ya kuimarisha miundombinu. Ninakumbuka kule MOI waliwahi kukopeshwa, hapa Benjamin Mkapa waliwahi kukopeshwa na taasisi ya NHIF zaidi ya shilingi bilioni 200. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali ihimize taasisi ambazo zimekopa hizo zaidi ya shilingi bilioni 200 waweze kurejesha hiyo mikopo ili taasisi yetu iweze kuwa himilivu, iweze kuwa endelevu, isifilisike na iweze kutoa huduma bora kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa ni suala la matumizi ya TEHAMA. Serikali imefanya kazi kubwa ya kuboresha huduma ya TEHAMA kwa kushirikiana na wadau wetu. Hii huduma ni nzuri sana kwani imeboresha kwanza kazi za madaktari wetu, manesi wetu na watumishi wengine katika kada hii ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninafikiri uimarishaji wa huduma hii ya TEHAMA uendelee ili kuhakikisha kwamba huduma hii ya afya inaendelea kuboreshwa, lakini pia tutadhibiti wizi na ubadhirifu wa fedha kwenye mapato. Kwa hiyo, ninaomba sana Wizara yetu na Serikali yetu itilie mkazo kwenye matumizi ya TEHAMA. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye NHIF ningeomba tuendelee kuboresha huduma ya upatikanaji wa dawa na vifaatiba kwenye hospitali zetu. Hii ni kwa sababu kama alivyozungumza Mheshimiwa Asenga, kuna maeneo unakwenda unaambiwa dawa ukachukue eneo lingine. Ukienda kule unaambiwa dawa hazijafika au kuna upungufu hazipo hivyo dawa nyingine unapata na nyingine unalazimika kwenda kununua kwa sababu ya hali ambayo unayo ya maradhi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaomba yote haya yaimarishwe ili kuhakikisha kwamba huduma ya afya inasonga mbele na inaendelea kuboreshwa zaidi. (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninasema ninaishukuru na kuipongeza Serikali kwa huduma bora ya afya inayoendelea kuimarishwa na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)