Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tanganyika

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nawapongeza sana Wizara ya Afya kwa juhudi kubwa ambazo wamezifanya kwenye Taifa letu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuleta fedha nyingi za maendeleo hasa kwenye maeneo ya jimbo langu. Wilaya ya Tanganyika imepokea vifaatiba vingi na vya kisasa ambavyo kiukweli vinavutia sana na vinatoa huduma nzuri kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudia kuipongeza Serikali, Serikali ya Awamu ya Sita imeleta fedha nyingi sana za maendeleo kwenye maeneo mbalimbali katika sekta ya afya. Kwenye eneo hili ni lazima tuipongeze Serikali kwa sababu vitu vilivyoletwa na Serikali vimeonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Katavi ulikuwa hauna Hospitali ya Mkoa, lakini leo hii tunayo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambayo inafanya kazi na inawasaidia wananchi wote wa Mkoa wa Katavi. Wilaya ya Tanganyika tulikuwa hatuna Hospitali ya Wilaya, leo tunavyoongea huduma zinatolewa na tunapata huduma nzuri, tuna vifaa ambavyo hata maeneo mengine hawana, sisi tumepata. Bahati mbaya tu ambayo ningependa kuishauri Serikali, itusaidie wananchi wa Wilaya ya Tanganyika, ni uhaba wa watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili tuna uhaba mkubwa sana. Mahitaji ya watumishi wa kada ya afya ni 776, waliopo mpaka sasa ni 276; kwa hiyo, tuna tofauti ya watumishi 500. Ukiangalia uhalisia wa kile ambacho kimepelekwa, bado huduma tunayoipata ni duni sana kutokana na uhaba wa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo vipo kwa sasa ni 43. Kabla ya hapo tulikuwa na vituo 28, vituo vingi havina watumishi. Tulikuwa na vituo vitatu vya afya, lakini kwa sasa tunavyo vituo tisa, kati ya hivyo, vituo vingine vimeshindwa kufanya kazi kwa sababu ya kukosa watumishi. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri tuangalie kwa jicho la huruma, tunahitaji watumishi kwenye hospitali ya wilaya, kwenye vituo vya afya na kwenye zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Naibu Waziri alishafika kwenye maeneo hayo, anatambua amefika na anajua mazingira ya Wilaya ya Tanganyika jinsi yalivyo. Nawaomba sana mtuletee watumishi, kada ya manesi na madaktari. Tumepewa vifaa vya kisasa vya x-ray karibu vituo vyote vya afya na hospitali ya wilaya; tuna mtaalam mmoja tu ambaye yupo anatumika maeneo yote hayo kiasi kwamba huduma nyingine zinashindwa kufanyika kwa sababu huyo ndiye anayetembea kwenye maeneo ya wilaya nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Mheshimiwa Waziri watuletee watumishi wa kada ya afya ambao wanahitajika kwa wakati, kwa muda huu ili waweze kuja kutatua tatizo lililopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninazungumzia ni bima ya afya. Kwenye eneo hili bado hatujafanya vizuri. Halmashauri yangu ya Wilaya ya Tanganyika iliingia bima ya afya kupitia vijiji vile vinavyopata fedha za hewa ya ukaa, wamelipa; vijiji vyote nane ambavyo vinanufaika vilipata fedha na kulipia, lakini bahati mbaya sana huduma hii imekuwa haipatikani kwa sababu ya mfumo wa bima ya afya ulivyo na vikwazo. Naomba hili mlifanyie kazi na muangalie ni jitihada zipi ambazo zitafanyika ili tutatue tatizo la bima ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kulingana na Mwongozo wa Bima ya Afya kwa Wote uliopo kwa sasa, ninataka tupate ufafanuzi; je, wale waliolipia kwa mfumo huu mwingine mpya unaokuja kwa bima ya afya ya watu wote, Serikali itafanya vipi kuhakikisha wale waliolipia kipindi hiki cha nyuma wanaingia kwenye mfumo huu uliopo au wataenda kwenye mfumo mpya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tupate ufafanuzi wa Serikali, ili tupate mwongozo wa bima ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia sana juu ya kulinda matumizi ya vyakula na pombe kali. Hili ni jambo ambalo kila eneo linaathirika sana hasa kundi la vijana. Bodaboda wengi wameathirika sana na matumizi mabaya ya pombe ambayo yanatumika siku hadi siku. Naomba maeneo haya tuyafanyie kazi, bila hivyo Taifa litaingia kwenye gharama kubwa sana ya kutibu Watanzania na fedha hizo hatutakuwa nazo, gharama ya kutibu wagonjwa karibu wote nchi nzima itakuwa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee juu ya wataalam wa maabara kwenye Wilaya ya Tanganyika; pamoja na jitihada zilizofanywa za kuleta vifaatiba, kila kitu kimeletwa kwenye eneo hili, lakini hatuna wataalam wa maabara. Eneo hili tunaomba muweze kuliangalia vizuri ili kutatua kero ambayo inatokea pale wataalam wanapokosekana ambao ndiyo wanaobaini chanzo cha magonjwa ambayo yamekuja kuripotiwa kwenye vituo vya afya au hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba ambulance; Wilaya ya Tanganyika iko na mtawanyiko na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri mmefika huko. Tunaomba ambulance moja ili iweze kusaidia kwenye Ukanda wa Ziwa Tanganyika ambao hauna kabisa ambulance. Eneo hili ni muhimu sana tuweze kupata ambulance walau mbili, moja iende eneo la Mishamo na nyingine iwepo kwenye eneo lile la Ukanda wa Ziwa na ile iliopo iweze kusaidia kwenye eneo la hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana Serikali na ninampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na watumishi wote wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuleta fedha nyingi kwenye kada ya afya. Ninaomba kuishukuru sana Serikali kwa dhati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)