Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE: ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa rehema zake kwetu sote, lakini pia kwa Taifa letu kwa mambo mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana iliyofanyika. Kwanza, kwenye Jimbo la Mbulu Mjini na pia katika majimbo mbalimbali nchini kwa kazi kubwa katika Wizara hii ya Afya na sekta nyingine. Kwa kweli, kazi kubwa sana imefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naishukuru Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa nafasi mbalimbali. Pia nakushukuru wewe Mheshimiwa Waziri, kwa kazi kubwa unayofanya toka tulivyoanza hapa Bungeni hadi sasa ukiiongoza Wizara hii, hongera sana kwa utendaji wa kazi. Nakushukuru Naibu Waziri, tumeshirikiana mambo mengi sana kwa miaka mitano ya kwanza na mitano hii ya pili ukiwa kama Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa imefanyika, tunashukuru kwa ujumla na mimi ninakushukuru sana. Pia natoa shukrani nyingi kwa wateule mbalimbali wa Wizara kuanzia Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Serikali wa Wizara hii pamoja na Wizara nyingine kwa kazi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kueleza mafanikio na changamoto zilizoko. Kwanza, nizungumze suala la mafanikio; kazi kubwa ya ujenzi wa miundombinu mingi sana imefanyika katika Wizara hii kwa kipindi cha miaka minne ya Dkt. Mama Samia na pia kwa Serikali za awamu zilizopita, kwa kweli, hatujatarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwa ujenzi wa majengo, lakini pia kwa miundombinu na vifaa vya matibabu katika sekta yetu ya afya na hasa Jimbo la Mbulu Mjini. Tumefanikiwa pia ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali ya mji, kwa kweli, majengo mengi sana yamefanyika. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nieleze kwamba fedha hizi nyingi zilizopatikana katika miundombinu imepunguza matatizo mengi kwa wananchi wa Jimbo langu la Mbulu Mjini. Kwa zahanati kama tisa zilizojengwa zinatoa huduma, vituo vya afya vinne, magari, vifaatiba na majengo katika hospitali ya mji; kuna majengo mengi yamejengwa kwa mabilioni ya fedha na huduma zimeboreka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto chache tu; kwanza nielezee kwamba Jimbo la Mbulu Mjini ni jimbo lenye kata nyingi kati ya majimbo ya miji kwa Taifa letu kwa sababu sisi tuna kata 17 tofauti na majimbo mengine ya miji yenye kata nane, kata 10, kata 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna jiografia ya aina mbili, tuna vijijini na mjini. Kule vijijini tuna kata 10 na mjini tuna kata saba. Maeneo haya ya vijijini kijiografia ni magumu kidogo kuyafikia, lakini Serikali tumejenga vituo vya afya, nishukuru kwa fedha zilizopelekwa. Hivi juzi, ndani ya mwezi huu wa tano tuna ujenzi wa Kituo cha Afya Murai na tunaendelea kuomba fedha hizi zingine zilizobaki kwa ajili ya kituo cha afya, kwanza kile cha Bunyoda na kile cha Gehandu. Kwa kuwa iliwekwa kwenye mipango yetu na nimeahidiwa na Mheshimiwa Waziri na watendaji wa Wizara ya TAMISEMI kwamba fedha hizi zitapatikana kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha, basi tunaishukuru Serikali walau hata zile za shilingi milioni 250 zikija zitaanza ujenzi kwa sababu bado ni mwendelezo na bajeti zetu ni hizo ambazo tunatarajia kupata na wakati huo kwenda kutekeleza miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie eneo hili la mafanikio. Hospitali ya Mji wa Mbulu tumejenga majengo makubwa, tumeletewa vifaa, kwa maana ya jengo la dharura pia na jengo la uangalizi wa wagonjwa. Majengo haya yamekuwa chachu kubwa pamoja na gari za ambulance zilizopelekwa mbili. Kule kwenye Kituo cha Afya Kainam tayari imeanza kutoa huduma. Katika mgao unaokuja kituo hiki cha afya kiko kijijini na kinahudumia kata karibu nne. Kwa hiyo, tukipata gari la ambulance itasaidia sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu tunaamini zile zilizoletwa zinahudumia katika vituo ambavyo tayari sasa hivi zinatoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika bima ya afya, niwapongeze sana watendaji wa hospitali hizi za Taifa kama Muhimbili, Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa na hizi za mikoa kwa huduma za kadi ya bima ya afya. Anapokwenda muhitaji, mgonjwa wa bima ya afya, wamemwandalia utaratibu mzuri sana, kwa maana anapokelewa, anahudumiwa, anapelekwa katika department mbalimbali kwa maana ya vitengo na baadaye anapatiwa huduma zake mpaka dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hospitali za miji na wilaya bado bima hii, baadhi ya dawa na baadhi ya huduma zinalipiwa. Mimi nilikuwa naomba kama inawezekana kwa Hospitali ya Mji wa Mbulu bado tuna tatizo kubwa la upungufu wa dawa. Huwa ninatembea wodini na kwenda kwenye wodi mbalimbali, ninazungumza na wagonjwa ninakuta mambo mengi, wagonjwa wengi wananunua dawa hizi na hasa kundi lile la mama na mtoto pamoja na wazee ambao kwenye sera yetu tumesema walau wapewe huduma ya afya bila malipo. Tukisema bure tunakwenda kinyume zaidi, tuseme bila malipo, kwa maana ya msamaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika eneo hili mimi ushauri wangu ni kwamba kwanza tutazame takwimu za wapokea huduma. Hospitali ya Mji wa Mbulu inahudumia iliyokuwa Halmashauri ya Mbulu ambayo sasa ni Halmashauri ya Karatu, kwa kuwa iko katikati inahudumia Halmashauri ya Babati, eneo la Magara na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu. Kwa kuwa ni hospitali yao kongwe ya zamani, basi watu wana imani kubwa kwenda hapo na mara nyingi wakienda wanategemea watapata huduma. Kwa hiyo, kuna mwingiliano wa takwimu ambazo haziko kwenye takwimu za Halmashauri ya Mji wa Mbulu kwa ajili ya wapokea huduma, akina mama wajawazito pia unakuta kuna wagonjwa kutoka hizo halmashauri zinazopakana kwa ajili ya ukaribu wanakwenda pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba walau niiombe Wizara ione namna, kwanza kuangalia zile takwimu halafu iongeze huduma ya dawa na vifaa tiba kwa ajili ya bajeti, kwa sababu inaonekana idadi ile ukiitazama ni takribani 30% kwa mwaka wanatoka katika halmashauri hizo zinazotuzunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili litahitaji sana, sana, sana, kutazamwa kwa sababu eneo la afya ni eneo sensitive na inategemewa na watu wengi. Namna pekee ninayoona ni kwamba kama tunaweza kuongeza ruzuku basi tuongeze ruzuku kwenye upatikanaji wa dawa na vifaatiba ili walau wale wananchi ambao hawana uwezo wa kulipia hizo gharama waweze kuhudumiwa na hasa kundi hili la akina mama kwa sababu ukizungumza gharama ya upasuaji shilingi 150,000 ama shilingi 120,000 kwa mama mjamzito unaweza kukuta familia hiyo haina huo uwezo.

Kwa hiyo, tunatakiwa kupunguza baadhi ya huduma kuzilipia. Tunajua zingine lazima wananchi walipie, Serikali kwa uwezo wake haiwezi kulipia gharama ya matibabu kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hizi bima za afya tunazozungumza zile package za mwisho zile za chini tunajua inahudumia kwenye ngazi fulani fulani za matibabu. Mimi ninadhani bado kwa matatizo ya magonjwa kuna wananchi wengi sana kule chini wanahitaji wapate huduma hizi za ngazi ya wilaya, ngazi ya mkoa na ngazi ya hospitali za rufaa. Tuitazame upya namna ambavyo huduma hii itatengamaa na itatoa huduma nzuri kwa makundi haya ya wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye eneo hili la pombe sitazungumza sana, lakini tutazame. Ninadhani alcohol hizi za viroba Mheshimiwa Waziri na Serikali kuna haja ya kwenda kuandaa vipimo maalum ili kuona athari zikoje na kwa namna gani tunaweza tukakabiliana nayo. Kwa nini nazungumza hivi, mimi pia ni mshiriki au mfanyabiashara wa baadhi ya pombe, lakini ninachojifunza ni kwamba pengine mwananchi anatumia chupa za mills 250 kama mbili au za mills 200 kama mbili tayari amelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, hii hali inakuwaje? Hatuoni kuwa yawezekana ukali wa hiyo pombe iko juu sana? Kuna haja ya kutazama na pia kuboresha eneo la kuzuia uingizaji wa bidhaa hizi au vyakula tunavyoingiza pamoja na dawa ili kuweza kuzuia badala ya zimeingia nchini tunakwenda kukagua, halafu tunakwenda kuteketeza kumbe tunaathiri uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, solution kubwa au jibu sahihi lililo kubwa ni namna ya kuzuia ili wasiingize nchini ama wasitengeneze kwa kadri ambavyo mamlaka zetu zikifanya uchunguzi na inaona kwamba kwa vyovyote vile haijaweza kufanikisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia eneo lingine ambalo nazungumzia ni kwamba kwa namna ya pekee Serikali iongeze bajeti ya Wizara ya Afya. Hii nchi tumekuwa wengi, yaani takwimu ya nchi ya watu milioni 61 mahitaji ya magonjwa mbalimbali yameibuka kiasi kwamba hata Serikali haiweze kukabiliana na hali hii kwa sababu bado ina deni kubwa na mapato yetu bado ni madogo. Ushauri wangu ni kwamba tutazame upya namna ambavyo bajeti hizi tunazitazama. Hata kama tuko zaidi ya trilioni moja pointi kadhaa basi tuangalie maeneo nyeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee pia kama inawezekana ruzuku ya wazee, kwa maana ya wazee katika bima yao ama kitambulisho kinachoonekana, lakini wakaongezewa. Nchi kama Tanzania tunaweka ruzuku kwenye mafuta, lakini mwenye gari ana uwezo kuliko maisha ya mtu ambaye ni Mtanzania, unapoweka ruzuku kwenye mafuta ya magari halafu huku kwenye afya tunaacha, hasa kwa makundi haya ya wazee pia kwa makundi haya ya mama na mtoto. Jambo hili hebu litazamwe namna gani tunaweza tukapata fedha mahali tukaboresha eneo hili na kuijengea uwezo MSD ili iweze kufanikisha jambo hili kwa namna ya pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uzuiaji au matumizi ya dawa hizi za kuzuia au kuangamiza mbu. Nchi zingine zinaagiza kwetu zinanunua, sisi kwetu msambazo umekuwa mdogo na namna ya kuzipata au kuzipunguza gharama ili tuweze kudhibiti mazalia ya mbu na namna ya kuyateketeza bado mwendo wetu ni mdogo. Tutazame namna gani tunaweza tukatekeleza programu ya kitaifa ya kuweza kuzuia ama kuangamiza mbu kwenye masalia na maeneo mbalimbali ili tuweze kufanikiwa kwa namna ya pekee ambapo itaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu huu kwa namna ya pekee niishukuru Serikali, niipongeze Serikali kwa kazi kubwa inayofanyika. Tuiombee nchi yetu kuelekea uchaguzi. Hao wanaotusema vibaya, wanaosema Serikali haijafanya kazi wanatembea kwenye barabara tulizojenga, wanapiga simu kwa mitandao tuliojenga, wanawasha umeme ambao Serikali imekwishatekeleza, pia wanapanda ndege na treni. Hawa tuwaache waendelee, Watanzania watawaelewa tu.
Sisi jukumu letu liwe kwenda mbele na kutekeleza na kuitakia nchi yetu uchaguzi mwema wa mafanikio. Bado Watanzania wana imani kubwa kwa chama chetu na kwa Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunisikiliza na kwa muda wako, ninashukuru sana, ninaunga mkono hoja kwa 100%. (Makofi)