Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Amb. Liberata Rutageruka Mulamula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BAL. LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi nichangie kwenye hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Afya. Ninaomba kwanza kabisa na mimi nitoe pongezi nyingi za dhati kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa hotuba nzuri na timu yake yote akiwemo Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia nimpongeze sana sana Profesa Janabi kwa ushindi wa kishindo na kuaminiwa kushika nafasi ya Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika. Profesa Janabi kama upo nakukaribisha kwenye uwanja wa diplomasia za kimataifa na kikanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia niungane na wenzangu kumshukuru sana, sana, sana Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel kwa msaada wake mkubwa. Kama wengine walivyosema, hata ikiwa usiku wa manane una dharura Mheshimiwa Dkt. Mollel atakusaidia pamoja na msaidizi wake Daniel Pyuza, kwa kweli wamekuwa msaada sana, sana, sana na hawachoki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba uniruhusu niwapongeze madaktari na wafanyakazi wote wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Mloganzila, Hospitali ya MOI, Jakaya Kikwete Cardiac Institute. Kwa namna ya pekee niwashukuru sana madaktari wa Mbeya Referral Hospital. Nimefurahi kumuona Mkurugenzi wa Mbeya Referral Hospital hapa ambaye niliunganishwa na Mheshimiwa Dkt. Mollel wakati nilikuwa na dharura ya kijana wetu alikuwa amepata ajali ya bodaboda. Kwa kweli wamefanya miujiza kuweza kumsaidia na akapona na hasa naomba kupitia kwa huyo Mkurugenzi kama bado yupo anifikishie shukrani zangu kwa daktari mtaalam wa neurosurgeon. Ni daktari kijana, anaitwa Dkt. Boazi; kwa kweli tunao madaktari. Katika kumsaidia huyu kijana ilikuwa kwa kweli ni medical miracle.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hizo hospitali nilizozitaja ikiwemo ya Benjamin Mkapa ninawashukuru sana, sana kwa customer service, yaani huduma zao ni ya viwango vya kimataifa. Ukienda kwa kweli unasema kumbe tunaweza. Maana kwa wale ambao wameenda Benjamin Mkapa siombei kwamba muende, lakini ikitokea umeenda ukifika tu utakuta wale vijana waliovaa uniform huko nyuma yameandikwa maandishi makubwa uliza nikusaidie na kweli wanatusaidia. Kwa hiyo, naomba kupongeza menejimenti ya hospitali hiyo kwa kweli mmeboresha sana huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa msemaji wa mwisho bahati nzuri ni kwamba mengi yamesemwa. Mimi ninaomba nijikite katika maeneo machache tu. Kwanza, kabisa ninaomba niungane na wenzangu nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali na Wizara kwa mikakati thabiti ambayo imeinua sana sana sekta ya afya na imeendelea kuboreka na upatikanaji wa huduma za afya kwa kweli umeimarishwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba uniruhusu niongelee kuhusu Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation. Nilibahatika kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hii na Mheshimiwa Msadifu wa Taasisi hii Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye ni Setra wa Taasisi hii. Ninaongelea kwa uchungu sana, ninaomba unisikilize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takribani miaka 19 taasisi hii imekuwa ikichangia sana kupunguza uhaba wa wataalam wa afya hususan katika maeneo yenye changamoto kubwa ya wataalam nchini kote. Kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na wadau wa maendeleo mpaka sasa taasisi hii imechangia ajira za wataalam wa afya wapatao 7,322 wakiwemo madaktari, wauguzi na kada nyingine mbalimbali nchini kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ninasema kwa masikitiko. Kufuatia tamko la Executive Order ya Rais Donald Trump, na kama mnavyofahamu, kufatia tamko hilo Shirika la Misaada la Marekani (USAID) lilisitisha na kufuta misaada kwa miradi ya afya takribani 17 iliyokuwa inatoa mchango mkubwa katika kutoa huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mradi huo mkubwa ni mradi uliojulikana kama “Afya Endelevu” uliokuwa unasimamiwa na taasisi ya Mkapa Foundation ambapo ulitoa ajira kwa wataalam wa afya 1,299 ambao walikuwa wanatoa huduma za afya katika hospitali na vituo vyote vya afya vya umma nchini, vituo 701 kwenye mikoa 22 yote ya Tanzania ikiwemo Mkoa wa Kagera, Kanda ya Ziwa na mikoa mitano ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusitishwa kwa ghafla kwa mradi huu adhimu kumesababisha kusitishwa kwa ajira ya watumishi hao 1,299. Hili limekuwa ni tishio na limeathiri kwa kiasi kikubwa kasi ya upatikanaji wa huduma za afya hasa za mama na mtoto, UKIMWI na kifua kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambayo imekuwa ikilifanyia kazi suala hili. Kulingana na udharura na umuhimu wa jambo hili kuna wengine ambao wamekuwa wanabeza wanasema kufungwa kwa miradi ni kwamba tulikuwa hatunufaiki, kwamba fedha zilikuwa zinarudi kule zilikotoka. Mimi ninataka kusisitiza hili, kwamba kwa kweli hapa napoongea wafanyakazi 1,299 katika sekta ya afya nchini kote wamesimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi napongeza juhudi zinazoendelea, Mheshimiwa Waziri Jenista anajua, nimekwishaongea naye kuhusu hili. Mimi ninaomba Mheshimiwa Waziri akija kutoa hitimisho tafadhali atueleze ni wapi tumefikia katika kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanabakizwa katika vituo husika na kuendelea kutoa huduma adhimu za afya kwa wananchi. Amesikia kilio cha Waheshimiwa Wabunge, kuna vituo vya afya, lakini havina wafanyakazi na hawa wafanyakazi tayari walikuwa kwenye ajira sasa wanakwenda mtaani. Kwa hiyo, nitashukuru sana kusikia tamko la Serikali kuhusu hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niongelee suala ambalo limeongelewa sana, suala la kuhusu gharama za matibabu ya dialysis nchini. Ninatambua gharama, hili ni kama janga kubwa sana. Nina ndugu yangu ambaye anakwenda mara tatu kwa wiki na kila akienda Muhimbili kupata hii dialysis analipia shilingi 150,000 na inabidi aende mara tatu. Kwa hiyo, kwa wiki wanalipa shilingi 450,000. Kwa hiyo, you can imagine, ni mtu gani ambaye ana uwezo huo? Na hii dialysis ikiendelea inaendelea maisha. Kwa hiyo, ninaomba hili liangaliwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna gharama pia ambazo zinaitwa catheter in session, Muhimbili zinauzwa hadi shilingi 2,000,000 kwa arteriovenous fistula na shilingi milioni 2.3 kwa permcath insertion, one PPM, najua madaktari wako wanaelewa kutegemea wanamwekea ipi. Je, ni wangapi wana uwezo huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi narudia kilio cha Wabunge wenzangu kuhusu hili suala, kwa kweli liangaliwe na Mkurugenzi wa NHIF mdogo wangu Irene analijua, ndugu zangu walikwishakwenda kumwona lakini akawaambia mikono yake imefungwa. Sasa sisi tufanyeje kwa kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho of course limeongelewa suala la mfuko wa afya, ninashukuru Mbunge mmoja ameongelea kuhusu wazee. Kwa kweli wazee katika nchi nyingine wanabebwa vizuri sana, lakini huku naona wazee wananyanyapaliwa. Mimi nina mama mkwe ana miaka 98 amenipigia simu ameenda kwa daktari ameandikiwa dawa za moyo wakamwambia kwamba kumbe hazimo tena kwenye hicho kifurushi na hakuwa na taarifa.

Kwa hiyo, mimi ninasema jamani ninaomba hiyo bima ya afya sijui itakuwa kwa wote, lakini na vifurushi angalau wazee nao wapewe priority na preference treatment.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naomba niunge mkono hoja, asilimia 100 kwa 100, ahsanteni sana. (Makofi)