Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Afya, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.” 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Afya, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Awamu ya Sita, Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetekeleza miradi mingi ya miundombinu ya afya. Katika kutambua ufanyaji kazi mzuri wa Wizara ya Afya, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepokea tuzo ya heshima ya The Gates Goalkeepers Award kutambua juhudi zake za kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa 80%, kuboresha upatikanaji huduma za afya na kukuza usawa wa kijinsia katika sekta hiyo. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kiongozi huyo anakuwa wa saba duniani na wa kwanza Afrika kutunukiwa tuzo hiyo ambayo hutolewa kwa viongozi waliowezesha nchi zao kuharakisha maendeleo kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG). 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na kwa kushirikiana na TAMISEMI, imeendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya Hospitali ya Wilaya na vituo sita vya afya vya Kata za Ikukwa, Ilembo, Santilya, Ilungu, Swaya na Utengule Usongwe. Vituo vyote sita vinaendelea kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa hasa huduma ya watoto na akina mama. Hospitali ya Wilaya pamoja na vituo vya afya vimekamilika na maandalizi ya vifaa tiba vya nyongeza yapo katika hatua za mwisho ili vianze kutoa huduma kwa ukamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki tunapopambana na majanga, magonjwa ya mlipuko ikiwemo la corona virus (covid-19), tumejifunza umuhimu wa utayari wa huduma ya afya hasa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali na hivyo Serikali iongeze msukumo wa kupeleka vifaa tiba na kumalizia vituo vya afya na zahanati zilizojengwa kwa nguvu za wananchi. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wananchi wa Kata za Igoma, Isuto wamejenga vituo vya afya na kuna maendeleo mazuri ya kukamilisha na pia katika Mji Mdogo wa Mbalizi wenye wakazi zaidi ya 150,000 kuna uhitaji wa ujenzi wa Hospitali ya Mji wa Mbalizi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo napendekeza Serikali kutoa kipaumbele katika bajeti hii kwa vituo vya afya hivi ili kukamilisha vifaa tiba na watalaamu ili vitoe huduma kikamilifu. Pamoja na Vituo vya Afya vya Ilungu, Igoma, Isuto na Ulenje, napendekeza kukamilisha zahanati zote ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maboresho ya miundombinu ya hospitali na vituo vya afya, Serikali ihakikishe bajeti ya mwaka huu inaendelea kujielekeza zaidi kwenye ajira ya madaktari na watumishi wa afya kwa ujumla. Pamoja na maboresho hayo ya miundombinu, vifaatiba na ajira kwa watumishi, napendekeza Serikali ikamilishe mpango kabambe na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na hasa kwa wazee na wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali iangalie jinsi ya kuboresha Bohari ya Dawa (MSD) ikiwa ni pamoja na Serikali kuhakisha inaongeza mtaji wa MSD na kuboresha muundo wa shirika ili uendane na jukumu kubwa la kutoa huduma kwa tija na ufanisi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki ambapo Serikali inaangalia kuanzisha Bima ya Afya kwa Wote, kipaumbele kielekezwe kwenye maboresho ya upatikanaji wa dawa pamoja na kuwezesha huduma ya hospitali zetu kutoa huduma bora zaidi kwa ukanda huu wa Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.