Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb.), Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel (Mb.), Katibu Mkuu - Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe, Naibu Katibu Mkuu - Ndugu Ismail Abdallah Rumatila, Mganga Mkuu wa Serikali - Dkt. Grace Elias Magembe, wataalamu wa Wizara na wadau wa afya kutoka sekta binafsi kwa kazi nzuri wanazofanya kwenye kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia kuhusu changamoto mbalimbali zinazoathiri huduma za afya hapa nchini na nitapendekeza namna ya kukabiliana nazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za afya ni mojawapo ya haki za msingi za binadamu na ni kipengele muhimu katika kuhakikisha tunakuwa na jamii yenye afya bora. Katika kitabu kitakatifu ninachokiamini, kuna mistari 108 ya Biblia kuhusu afya ya kimwili, jambo ambalo linatakiwa kupewa kipaumbeke na mamlaka zilizowekwa kutuongaza na Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mathayo 15:30 - watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya. Mathayo 9:35 - Yesu alitembelea miji yote na vijiji, akafundisha katika masunagogi yao akihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila namna bila kulipua gharama yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma bora za afya zinahitaji kuwa na upatikanaji wa vifaa, wataalamu wa afya, miundombinu bora na usimamizi thabiti. Hata hivyo, huduma za afya hapa Tanzania zinakabiliwa na changamoto nyingi zinazopunguza ubora na upatikanaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hizo ni kama zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Watanzania wanatofautiana sana kwa uwezo wa kifedha. Kuna watu wa kipato cha juu ambao ni wachache sana kwenye jamii na watu wa kipato cha chini ambao ndio wengi. Kiuhalisia, huduma za afya ni za gharama kubwa ambazo watu wa kipato cha chini hasa wanaoishi vijijini hushindwa kuzimudu. Kama mwananchi hana bima ya afya ya gharama anayomudu hii huwafanya watu wengi wa kipato cha chini kushindwa kugharamia huduma za matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nchi yetu ina upungufu wa wataalamu wa afya katika nyanja mbalimbali. Wataalamu wa afya kama vile madaktari, wauguzi na mafundi sanifu wa vifaa tiba, ni changamoto kubwa katika sekta ya afya hapa Tanzania. Katika maeneo mengi yanayotoa huduma za afya hasa vijijini kwenye vituo vya afya na zahanati, idadi ya wataalamu wa afya haitoshelezi mahitaji ya wagonjwa. Hili husababisha mzigo mkubwa wa kazi kwa wataalamu wachache waliopo. Wataalamu wengi wa afya wanakosa muda wa kuhudumia wagonjwa kwa ufanisi, jambo linalosababisha msongamano katika vituo vya afya na kupunguza ubora wa huduma. Upungufu huu huongeza muda wa kusubiri kwa wagonjwa na mara nyingi husababisha wagonjwa kukosa huduma muhimu.
 Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, katika maeneo mengi hasa yale ya vijijini (vituo vya afya), kuna changamoto ya ukosefu wa miundombinu bora na vifaa tiba. Katika maeneo haya, vituo vya kutoa tiba vinakosa vifaa muhimu kama vitanda vya wagonjwa, majokofu ya kuhifadhi dawa/maiti, vifaa vya uchunguzi kama skana, ultra sound machines na mashine za kisasa za upasuaji. Pia kuna ukosefu wa magari ya kubeba wagonjwa kwa mfano, Hospitali ya Wilaya ya Mabogini iliyoko Jimbo la Moshi Vijijini haina gari la wagonjwa (ambulance). Ukosefu wa vifaa tiba unaathiri uwezo wa vituo hivi kutoa huduma bora kwa wagonjwa, jambo linalosababisha baadhi ya wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, pamoja na Serikali kupitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, lakini bado kuna changamoto ya watu kujiunga na Mfuko wa Bima wa Afya. Kwa watu wa kipato cha chini na wasio na ajira, ukosefu wa bima ya afya ni changamoto inayowazuia kupata matibabu kwa gharama nafuu. Wengi wanakosa bima ya afya kutokana na gharama kubwa za bima au kukosa mwamko kuhusu umuhimu wa bima ya afya. Kwa mfano, kifurushi cha bima ya afya cha bei ya chini cha Ngorongoro Afya kwa mtu mmoja mwenye miaka kati ya 18 hadi 35 ni shilingi 432,000. Bei hii ni kubwa kwa kundi la watu hawa wenye kipato kidogo. Ukosefu wa bima ya afya kunawafanya watu kushindwa kulipia matibabu yanayotokea kwa dharura bila kujipanga au huduma nyingine za afya kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia, wataalamu wengi wa afya wana ari ndogo ya kufanya kazi maeneo ya vijijini. Hii ni kutokana na mazingira magumu ya kazi na ukosefu wa miundombinu muhimu huko vijijini. Vijijini kuna shida ya nyumba za kupanga, maji na umeme. Madaktari wengi na wataalamu wengine wa afya wanapendelea kufanya kazi mijini ambako kuna miundombinu bora na fursa zaidi za maendeleo. Hali hii inasababisha ukosefu wa huduma za afya za karibu kwa watu wa vijijini. Kutokana na hali hii, wananchi hulazimika kutafuta huduma za tiba mijini na kuongeza mzigo wa kifedha kwao na familia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika baadhi ya zahanati za Serikali, kuna changamoto ya ukosefu wa dawa muhimu, chanjo za watoto, vifaa tiba kama gloves za kutoa huduma kwa akina mama wanaojifungua, sindano na mashine za kupimia matatizo mbalimbali ya kiafya. Uhaba wa vitu hivi huathiri huduma za afya katika maeneo mengi vijijini. Katika baadhi ya zahanati, wagonjwa hupewa dawa zisizo kamili au hutakiwa kununua dawa kwa gharama zao. Akina mama wanaojifungua hulazimika kununua baadhi ya vitu kama gloves na sindano. Mambo yote haya huishia kuweka mzigo mkubwa wa kifedha kwa wagonjwa na huathiri sana familia maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika baadhi ya magonjwa, nchi yetu imekosa sera na mipango thabiti ya kupambana nayo. Kwa mfano, magonjwa yanayotesa raia wetu na yenye gharama kubwa za tiba kama yale ya figo, selimundu, upungufu wa damu na kansa hayana sera inayoelekeza namna ya kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kifedha kukabiliana nayo. Sera na mipango thabiti ya Serikali kukabiliana na magonjwa haya ni muhimu ili kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wanaokabiliana na magonjwa haya. Kutokuwepo na mipango madhubuti ya kutibu magonjwa haya kunafanya wananchi maskini kufa kwani tiba za haya magonjwa ni za gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupambana na changamoto hizi, ninaishauri Serikali ifanye yafuatayo:-
(i)	Serikali iongeze bajeti ya sekta ya afya ili isaidie kuboresha huduma za afya na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi wote na kuokoa maisha ya raia.
(ii)	Serikali ifanyie mapitio na kuweka kifurushi cha gharama ndogo cha bima ya afya kwa watu wa kipato cha chini. Hii itawasaidia watu wa kipato cha chini kupata huduma za afya kwa gharama nafuu na kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia maskini.
(iii)	Changamoto ya uchache wa wataalamu, ninaishauri Serikali ipeleke wataalamu wa afya wa kutosha katika maeneo yenye uhitaji, hasa huko vijijini. Mafunzo ya mara kwa mara yanahitajika ili kuhakikisha kwamba wataalamu wa afya wanaendelea kuwa na ujuzi wa kisasa na uwezo wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
(iv)	Serikali ipeleke vifaa muhimu kama vitanda vya wagonjwa, vifaa vya uchunguzi kama scanner na mashine za kisasa za upasuaji katika vituo vyote vya afya na hasa vile vilivyopo vijijini. Pale panapohitajika gari la wagonjwa, Serikali ipeleke ambulance.
(v)	Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kama viongozi wa dini na Wabunge wahamasishe wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya. Elimu hii inaweza kutolewa kwenye mikutano ya dini, siasa, mashuleni, vyuoni, ili kuwafikia watu wengi zaidi na kuwasaidia kujua umuhimu wa kuwa na bima ya afya. Kampeni za uhamasishaji zinaweza kuwasaidia watu kuelewa umuhimu wa bima ya afya na kusaidia kuongeza idadi ya watu wanaopata bima ya afya.
(vi)	Kutokana na mazingira magumu ya kazi na ukosefu wa miundombinu muhimu huko vijijini, Serikali itoe motisha maalumu ya kifedha kwa wafanyakazi wa afya wanaofanya kazi katika mazingira magumu vijijini.
(vii)	Kuhusu uhaba wa dawa na vifaa tiba maalumu, ninaishauri Serikali itoe ruzuku ya dawa na vifaa tiba muhimu ili kuhakikisha wagonjwa wanapata dawa wanazohitaji. Ruzuku hii itasaidia kupunguza gharama kwa wagonjwa na kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu.
(viii)	Serikali iwe na sera inayoelekeza namna ya kukabiliana na kutibu magonjwa yanayotesa raia wetu na yenye gharama kubwa za tiba kama figo, selimundu, upungufu wa damu na kansa ambayo tiba yake ni gharama kubwa. Serikali ije na mipango madhubuti ya kitaifa ya kusaidia wagonjwa hawa na kuweka mifumo ya kufuatilia wagonjwa hawa popote pale walipo kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba changamoto za huduma za afya zinahitaji juhudi za pamoja na mipango thabiti ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.