Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kunisemea na kuisemea Wizara yetu. Nianze kwa kumshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kweli yote ambayo mmeyasema hapa na yote ambayo yanaonekana yamefanyika vizuri kwenye sekta ya afya yanatokana na juhudi yake yeye mwenyewe Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru kwa kuendelea kuniamini kwa miaka mitano na sasa tunaelekea ukingoni. Pia niwashukuru wananchi wa Siha kwa kuendelea kuniamini wakati wote na kunipa ushirikiano na niwaambie ninakuja tena kwa nguvu sana na kwa wale ambao wananyemelea kama kawaida yetu tutaenda kuwapiga na kimsingi wanaenda kufilisika, kwa hiyo, thelathini hawatarudi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Waziri wangu Mheshimiwa Jenista Mhagama. Sisi sote ni mashahidi hasa Naibu Mawaziri wenzangu kama ambavyo amekuwa kiranja wetu wakati wote hapa na watu hawajajua wakati mwingine alikuwa anachezea namba ambayo unacheza miguu yote unachezea Wizara zote na ameweza kufanya. Kwa hiyo, sasa alipo Wizara ya Afya ni caterpillar limeletwa kulima bustani na bustani itavurugwa kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongee na wananchi wa Peramiho kwa kweli sisi watu wa Wizara ya Afya na madaktari wazuri waliozungumziwa hapa, watumishi wote wa Wizara ya Afya wanawaomba watu wa Peramiho waturudishie Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa sababu kwa kweli tumeletewa ndiyo tunaanza ku-enjoy utamu wake wakati tunaenda kulimaliza Bunge kuanza uchaguzi, tunamwomba tena arudi ili aweze kuendelea kuiongoza hii sekta yetu ya afya na tunaomba Rais kwa kweli huyu tunampenda na anafanya kazi nzuri na ameiunganisha Wizara yetu ya Afya na kazi inakwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waheshimiwa Wabunge wenzangu mmesema sifa zetu nyingi za Mheshimiwa Waziri, lakini hata na mimi mkisema tumetibu wagonjwa, tumefanya nini, lakini ninataka niwaambie ukweli sifa hizo siyo za kwangu mimi wala siyo za Waziri kwa kweli ni watendaji walioko hapa nyuma. Kwa sababu kazi yetu sisi ukitupigia simu tunachukua simu tunapiga simu dakika tatu. Pia kuna mwingine ambaye kama alikuwa amelala na mke wake au mume wake anaondoka masaa matatu kwenda kuhakikisha huduma inayotakiwa kutekelezwa inaenda kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwapongeze Wakurugenzi wetu wa Hospitali yetu ya Jakaya Kaka yangu Dkt. Kisenge, kaka yetu Profesa Janabi; MOI kaka yetu Dkt. Ulisubya, lakini Dkt. Makubi wa Benjamin Mkapa, viongozi wetu wa hospitali zote za kanda nchini na mikoa tunawashukuru sana. Mmeona sasa matokeo ya kazi ambayo tumekuwa tukiwapigia kuwaomba kuwasaidia Wabunge katika maeneo mbalimbali na mmeona matokeo yake katika siku hii ya leo tukipitisha bajeti yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao wanakuwa background mara nyingi hawatajwi. Ninaomba tu niseme Wabunge mmesema mambo mengi hapa, kama mimi nimepokea simu zenu 100 ninataka kuwaambia kuna mtu amepokea 70 kati ya hizo 100 na siyo mwingine ni ambaye sasa ni msaidizi wa Waziri ambaye alikuwa msaidizi wangu na siyo mwingine ni Daniel Pyuza ambaye amesaidia sana na amewasaidia ninyi Wabunge mliopo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilisema nitumie hii fursa wakati tunaenda kumaliza Bunge kwa kwenda kwenye uchaguzi nimwambie Daniel Pyuza ahsante sana kwa kunisaidia na hata ndiyo maana umefanya kazi nzuri. Watu walipofikiri jembe kama Mheshimiwa Jenista Mhagama nani atembee naye kwa sababu ni caterpillar limekuja kulima bustani alionekana yeye pamoja kuwa ni mfamasia, hajasoma utawala, lakini ameonekana yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna afisa wetu wa Bunge, Alpha Cholobi tunakupongeza sana, tumejaa makaratasi hapa, lakini umekuwa ukihangaika na Katibu Mkuu kufanya mambo yote haya. Pia nimalizie kwa heroes wetu; dada yangu amesema vizuri, dada yangu Mheshimiwa Esther Matiko kuhusu daktari aliyegundua roboti, sitaki kulirudia hilo limefika na limeingia vizuri kama ambavyo nilitamani liingie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye la innovations ma-nurse wamekuja juu sana na wamekuwa kila tukihudhuria mikutano yao unaona kwenye innovations katika maeneo mbalimbali. Kuna mmoja anaitwa Wilson Fungameza walishindana watu 500 duniani na akashika namba tano kwenye innovation na akaenda Uingereza na akachukua nishani na akairudisha Tanzania hao ndiyo vijana wetu wanaotusaidia kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kuna wengi wameandika vitabu na wamefanya vitu mbalimbali lakini ninaomba nimtaje mmoja atayewasilisha heroes wanaofanya mambo makubwa kwenye hii. Kuna nurse mmoja anaitwa Stella Ndogwisango, nurse huyu amemwokota mtoto mwenye ulemavu wa viungo na tundu kwenye moyo aliyetupwa uwanjani, lakini sasa amemtibu huyo mtoto. Pia ameendelea kumjali kama mtoto wake na yuko naye hapa, amekuja naye hapa. Mtoto huyo ana miaka miwili sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nurse huyo hajaishia hapo, ndiyo maana ninawaambia Waheshimiwa Wabunge mmetuambia matatizo mengi sana hapa yanayotakiwa kutatuliwa ambayo ni kwenye majimbo yenu na maeneo mbalimbali. Ninachotaka kuwaambia Wizara ya Afya ina watumishi wazuri wa kutatua hayo matatizo, lakini pia Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kama amefanya haya makubwa ambayo ninyi mmekuwa mkiyasema hapa haya mengine mliyoyasema kwa kipindi hiki kifupi ni madogo sana hata tusipowajibu ninaombeni mwende kuamini kwamba yanaenda kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa nurse huyo amekwenda alikuwa wodini amelazwa na mtoto wake, kuna ajali ya basi la Sabena lilitokea Shinyanga, halafu walipokuwa wamelezwa majeruhi wakaletwa wodini kukawepo na mtoto wamekaa naye mwezi mzima hakuna ndugu yeyote aliyewatembelea wakati wagonjwa wengine wamelazwa na ni mtoto ana miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati anaondoka yule mtoto akawa anamlilia, kutafuta ndugu na marafiki haikuwezekana kupatikana, akaamua kumchukua kumfanya mtoto wake. Huyo nurse alivyompeleka huyo mtoto kumfanya ndugu yake nyumbani, wakati anaenda nyumbani, mtoto yule kila akiona gari linapita analia anasema gari linakuja kutugonga. Anasema tunakufa, ndiyo mwisho wakarudi kuanza kuangalia list za wagonjwa wakagundua mama yake aliumia kichwa na yuko Bugando anatibiwa na amefungwa mikono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo mtoto alipopitishwa pembeni ya mama yake, mama yake aliweza kujigusa na kumtambua mtoto wake. Baada ya hapo pamoja na huyo mama kukaa wodini miezi mitano, lakini mama huyo akaanza kupata nafuu. Huyo mama alikuwa ni Mkenya na yuko Kenya kwenye nchi yao anaendelea na mtoto wake. Hayo ndiyo mambo ambayo yanawatokea watu wetu wodini, nimesema nitumie hayo leo kuonesha kwamba tunatambua mambo makubwa yanayofanyika na wataalam na watu wetu kutoka chini mpaka kule chini wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmetuambia mambo mengi, mmetuambia matatizo mengi, mmeeleza mambo mengi ambayo nikiangalia mliyoyasema ni zaidi ya makaratasi mengi na yote haya hamjatuambia sisi mnamwambia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia sisi. Hata hivyo, wakati mnamwambia msisahau Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan huyo ndiye yeye ambaye kwenye sekta ya afya amewaletea nishani ya Goalkeepers Award ambayo ni kwa Marais wa Afrika yeye ndiye pekee aliyewahi kupata. Ametuingiza katika list ya Marais saba duniani waliowahi kupata nishani hiyo na haijatokea kwa bahati mbaya, imetokea kutokana na huu uwekezaji mkubwa aliouwekeza kwenye sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia huyo ndiye huyo aliyeifanya Tanzania sasa imeingia kwenye nchi ya pili kwa Afrika Mashariki kuwa na PET/CT scan. Ametuingiza kwenye nchi ya tatu kuwa na PET scan kwenye nchi za SADC na nchi ya tisa kwa kuwa na PET scan kwenye nchi tisa ambazo zipo Afrika. Maana yake ukiona ni nchi tisa ukilinganisha na nchi nyingi zilizo Afrika siyo jambo rahisi kuwa nalo. Huyo Rais ambaye leo mmetuambia matatizo yenu tumpelekee, hapa ninaombeni mtuamini tumeyachukua, tumeya-record huyu huyu ndiye sasa tunampelekea ili aende kuyatatua. Kwa hiyo, haya yote yanatatulika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jiulize kwamba leo ukipanga ambulance 727 ukaleta hapa Dodoma ukazipanga ni kazi kubwa kiasi gani imefanyika? Huyo ndiye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tunayemzungumzia na ndiyo maana watu wanamlaumu Tundu Lissu kwa kukimbia uchaguzi, hata wewe ungekuwa Tundu Lissu ungekimbia, hata mimi ningekuwa Tundu Lissu ningekimbia. Ningefanya drama zote ambazo Tundu Lissu anafanya na wale wote wanaomwonea huruma tungefanya hizo drama kwa sababu hamna namna nyingine ya mwanasiasa kukimbia zaidi ya kutengeneza drama na uzuri wake mimi nimeshakaa huko kila nikiwatazama ninajua hii ni drama, mimi ninajua hii ni drama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo huyu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Rais ambaye ameifanya leo Tanzania siyo tu kwamba amewekeza ndani ya sekta ya afya ikatatua matatizo ya afya yaliyoko ndani ya Tanzania, alichowekeza kimebubujika na kikaenda kwenye mataifa mengine leo tunapozungumza hapa mataifa 15 yanaleta wagonjwa ndani ya Tanzania kutibiwa. Maana yake ni nini? Uwekezaji wa Dkt. Samia kwenye sekta ya afya haujagusa tu sekta ya afya ndani ya Tanzania, umewapunguzia gharama nchi kumi na tano zinatotuzunguka sasa wanakuja hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Tundu Lissu akiangalia vyombo vya habari CHADEMA na wapinzani wengine wakiangalia wanakuta watu kule Comoro, wanakuta watu kule Zambia na kwingine wanapanga foleni wanawasikiliza madaktari wetu. Wakirudi huku ambao hawatatibiwa na teknolojia iliyopo huko wanaletwa ndani ya Tanzania wanakuja kutibiwa. Wakiangalia hayo wanafikiria na impact ya kutoka taifani mpaka inapofika kijijini na wanachokijua Watanzania wanaona kwenye huu mchezo hatuwezi kuingia, wanaamua kukimbia na ndiyo maana unaona hata kuna wengine ambao ni Wana-CCM wenzetu wameanza kuugua ugonjwa wa kifafa, wanakimbiakimbia na kusema mambo mengi ambayo wanataka kutuvuruga, sitaki kutaja majina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninataka kuwaambia, shetani ukivaa kola ya madhabahuni, ukifanya mambo ya kishetani tutakufuata madhabahuni, utanyooshwa na utawekwa sawa ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kubaki kuwa salama. Mambo ya msingi kama haya makubwa ambayo Rais wetu anayazungumzia hatutaki mtu yeyote kusahaulisha Watanzania mambo makubwa yaliyofanyika. Leo katika hii nchi yetu ya Tanzania ilikuwa ukitaka kutibiwa bila kufungua kifua inabidi uende India, Ulaya au Marekani; leo unatibiwa ndani ya Tanzania na siyo sisi tu tunatibiwa ndani ya Tanzania wanakuja majirani zetu wa nchi zingine wanakuja kutibiwa ndani ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Tanzania hii tunaambiwa watu wanapata matatizo mbalimbali ya ubongo wanayotakiwa wafunguliwe ubongo, lakini leo ndani ya Tanzania hii kwa kutumia tu mawimbi ya sauti mtu anatibiwa bila kupasuliwa ubongo. Huyo ndiyo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tunayemzungumzia na ndiyo maana tunasema kwa wivu mkubwa Watanzania wanaungana. Ndiyo maana wenzetu walipoona kwamba wakiingia kwenye uchaguzi wanaenda kuvunja rekodi ambayo haijawahi kuvunjwa na CHADEMA katika kushindwa, wakaona hawako tayari kuvunja hiyo rekodi, wameanza comedy na kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali nchi hii kudanganya na Watanzania wanajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunakaa hapa kuna watu kutoka nchi za mbalimbali, kwenye mwaka huu tu zaidi ya watu 12,180 wametibiwa. Leo tunakaa hapa watu 2,770 wamefuatwa nchini kwao na madaktari wetu, watu wakiangalia wanaona Samia Aid inakuja watu wa nchi nyingine ndani ya nchi yao wanapanga foleni kutibiwa na madaktari wa Tanzania waliotumwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ndani ya Benjamin Mkapa Hospital ya kwetu hapa kuna magari ambayo ni hospitali kamili inatembea hapa na zimekwenda Burundi, zimekwenda nchi jirani wamekwenda na wakienda wakipaki gari la Mheshimiwa Dkt. Samia na limeandikwa Dr. Samia Service limekaa hapo watu wa Taifa lingine wanakuja wanapanga mstari wanapokea huduma kutoka kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hayo ndiyo tunataka dunia ijue kwamba Rais huyu tu siyo kwamba ameleta suluhu za afya ndani ya Tanzania, ameleta suluhu za afya kwa Afrika Mashariki na Kati na majirani zetu waliotuzunguka… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Mollel, ahsante sana…

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimalizie kwa kuwaomba wananchi wa Peramiho kwamba hili jembe tumeanza ku-enjoy utamu wake waendelee kutuletea kwa sababu tunampenda sana na watumishi wa afya watafurahi sana, ni mtu mwenye emotional intelligence ya kutisha tena ya kuzaliwa nayo, siyo ya kusomea darasani ahsante sana. (Makofi)