Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa tena fursa ya kuja kusimama hapa mbele ya Bunge lako Tukufu ili kuweza kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa sababu na minajali ya muda ambao nimepewa, hoja zenu ambazo kwa bahati mbaya ama kwa namna moja ama nyingine tutashindwa kuzifikia ninaomba mridhie tutazijibu kwa maandishi na tutaziwasilisha kwenu kabla Bunge hili halijahitimishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa dhati ya moyo wangu niinue moyo tena wa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu na kwa sekta zote ikiwemo sekta hii ya afya. Tuko katika kipindi ambacho kwangu mimi Waziri wa Afya baada ya kupata jukumu la kumsaidia Mheshimiwa Rais nimeona katika sekta ya afya ulimwenguni tunapita katika mabadiliko na mageuzi makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulimwengu huu kwa sasa tuko katika karne ya 21. Sasa katika karne hii ya 21 ukiangalia na Mheshimiwa Waziri kaka yangu Profesa Kitila amekuwa akisema sana haya, kwenye karne hii ya 21 mabadiliko ya uchumi yamekwenda kwa kasi na ukisoma taarifa mbalimbali katika majalada mbalimbali ni kama vile GDP katika nchi ama ulimwengu mzima imeongezeka karibu mara tatu ya viwango ambavyo vilikuwa huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maendeleo haya na ongezeko la uchumi kukua kwa GDP katika nchi mbalimbali kuna maanisha nini katika sekta ya afya? Kunamaanisha mambo yafuatayo:- (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza upande mmoja maendeleo haya yanaendana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wote. Sasa mabadiliko ya sayansi na teknolojia ni favour kubwa katika maendeleo ya sekta ya afya ulimwenguni.

Vilevile, maendeleo haya ambayo tunasema GDP imeongezeka, uchumi umekuwa katika ulimwengu mzima yanatupelekea kuongeza shughuli zinazoendana na maisha ya kila siku ya binadamu. Miji yetu imekuwa mikubwa sana na population katika miji yetu imeongezeka. Pamoja na kuongezeka kwa population kwenye miji yetu, maisha ambayo tuliyazoea huko nyuma yamebadilika, kwa hiyo, mila, desturi na tamaduni za ulimwengu kwenye mataifa mbalimbali zimebadilika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu sasa wanaishi kwa kimitizamo ya miji zaidi, ninataka kusema nini, baada ya kubadilika kwa mila, desturi, tamaduni zetu za maisha huko nyuma hapo ndipo tunakutana na tabia za wananchi na za jamii ambazo zimepoteza asilia yake na kujiingiza kwenye mageuzi haya makubwa ambayo yaendana na mtazamo wa kiuchumi kwa sasa na ndiyo watu wengi wamesema na mdogo wangu Mheshimiwa Esther hapa amesema. Kwa hiyo, hata zile tabia bwete za kutokufanya mazoezi ni kwa sababu ya mabadiliko haya ya kiuchumi, mitazamo ya kimaisha na namna tunavyoishi kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu wa mazingira, ni kwa sababu ya ongezeko la watu, lakini mabadiliko ya mtazamo mzima wa mwenendo wa maisha ulimwenguni na mabadiliko haya ya kiuchumi. Uwepo wa viwanda hiyo pia ni maendeleo makubwa, lakini kwenye sekta ya afya yanaathari kubwa kwa sababu ongezeko la moshi linaathari kubwa kwa maisha ya binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukataji wa miti na mazingira unasababisha mwingiliano kati ya binadamu na wanyama na matokeo yake ndiyo haya magonjwa ya mlipuko kama m-pox, ebola na mambo mengine ya namna hii haya marburg. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa tunakabiliana na changamoto za namna moja ama nyingine. Huku tuna maendeleo makubwa, huku tuna maendeleo kweli yanayo-affect sekta ya afya, lakini output ya hayo maendeleo inaathari pia na inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumefika katika ulimwengu ambao maendeleo hayo ya kisayansi yanatuambia sasa hivi sayansi ndiyo afya na afya ni sayansi. Bila sayansi hakuna afya na bila afya hakuna sayansi, ndipo mahali ambapo tumefika kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tupo tena kwenye hali ambayo ni lazima hata sisi kama Watanzania na nitasema hapa karibuni wakati ninapitia majibu ya maswali yenu. Tunasema maendeleo haya ya sayansi ni mabadiliko ya teknolojia na vifaa tiba na namna ya uchunguzi kwenye magonjwa. Kukua kwa hii sayansi uwepo wa chanjo ili kufanya prevention ya magonjwa tunayoyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine yapo makundi ambayo hayaamini pia katika maendeleo haya ya sayansi na teknolojia katika vifaatiba na chanjo ambazo zinatumika katika ulimwengu kwa sasa. Tuna kazi kubwa na ninaomba niseme katika Taifa letu la Tanzania kama tusingekuwa na daktari bingwa mbobezi number one Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwenendo huu wa ulimwengu kwenye sekta ya afya tungeweza kujikuta tupo mahali ambapo panatutatanisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sifa alizonazo ambazo zimesaidia sekta ya afya kuendelea kuwa himilivu kukua na kufika katika viwango ambavyo leo Waheshimiwa Wabunge ninawapongeza sana kwa kutambua mchango huo mkubwa wa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais huyu ana maono makubwa kwenye sekta ya afya, makubwa sana. Mheshimiwa Rais huyu amefanya maamuzi mazito tena yenye uthubutu mkubwa katika kuleta ustawi wa afya za wananchi. Mnakumbuka wakati wa Covid alipofanya maamuzi ya kuhakikisha Watanzania tunachanjwa ili tuweze kuokoa maisha yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ana vipaumbele katika sekta ya afya nami wakati ninawasilisha hotuba yangu nimewaambia vile vipaumbele kumi. Vipaumbele vyote vile kumi vinajibu hoja za Waheshimiwa Wabunge ambazo zimesemwa hapa na kipekee ninamshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati yangu na Wajumbe wa Kamati kwa kazi kubwa waliyoifanya. Hivi vipaumbele tumevifikia kwa sababu ya maono ya Mheshimiwa Rais na ushauri mkubwa tulioupata kwenye Kamati yetu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI. Kwa hiyo, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwahakikishie Mheshimiwa Rais ni jasiri katika kuhakikisha maamuzi tunayoyafanya kwenye sekta ya afya yanaleta ustawi ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yaliyozugumzwa leo na Wabunge yanagusa maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza, ni jinsi Taifa letu lilivyojikuta kwa sasa na siyo sisi peke yetu kwa sababu siyo kisiwa, ulimwengu wote, magonjwa yasiyoambukiza yameendelea kuongezeka kwa kiasi kikubwa. Kila mahali utakutana na kesi hizi kwa mtazamo mmoja ama mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia eneo la pili; ni magonjwa ya mlipuko ambayo nimesema yanatokana na mageuzi haya ya ndani ya ulimwengu yanayosababisha pia uharibifu wa mazingira, tabia ya nchi kubadilika, mienendo, mitizamo, tamaduni na desturi zetu kuwa zimebadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo pia magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Nimesema hapa wapo Watanzania ambao wameokolewa vifo kutokana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kama mabusha, matende na magonjwa mengine ya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile yapo magonjwa yale yanayoambukiza na Mheshimiwa Shigongo ameeleza sana kuhusu masuala ya Hepatitis B, lakini tumezungumza masuala ya HIV, ya TB na masuala ya malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba bajeti ambayo Mheshimiwa Rais na Bunge lako tukufu itakapoipitisha leo ambayo tumeomba shilingi 1,618,191,235,000 itakwenda kujibu hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge mlitupatia katika michango yenu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza, Waheshimiwa Wabunge mmezungumza sana kuhusu kiwango kidogo cha utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo katika sekta ya afya. Waheshimiwa Wabunge, tunalipokea jambo hili kwa mikono miwili na tutakwenda kulifanyia kazi, lakini ninaomba muungane na mimi kukubali kwamba Mheshimiwa Rais wetu huyu jemedari na mimi ndio ninasema yeye ndio daktari bingwa na mbobezi. Katika kipindi kifupi cha miaka minne amefanya mageuzi makubwa sana ya kuhakikisha fedha na rasilimali katika sekta ya afya zinapatikana. Sisi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mifano michache; mwaka 2015/2016 bajeti yetu na hasa katika eneo la maendeleo ilikuwa ni shilingi bilioni 8.3; mwaka 2021/2022 ilikuwa ni shilingi bilioni 278.4. Waheshimiwa Wabunge, mwaka 2024/2025 bajeti imefika shilingi bilioni 501.1. Kwa hiyo, ni lazima tuone nia, dhamira na utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha anaimarisha sekta hii ya afya na ninaomba tumpigie makofi mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, nitazungumza vizuri hapo mbele kama muda utanitosha. Hapa katikati tumepata mabadiliko ya sera za kimataifa kuhusu uchangiaji wa gharama kwenye sekta ya afya.

Waheshimiwa Wabunge, ninaomba niwaambie zipo nchi zimetetereka baada ya mabadiliko hayo ya kisera ya kimataifa. Hata dawa kwa ajili ya kuhudumia magojwa msonge ikiwemo HIV, TB, Malaria pamoja na hata hii Hepatitis. Dawa hizo ni tatizo, lakini wakati ninasoma hotuba yangu jana nimewaambia Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ilijipanga na ikaja kujipanga tena na imetoa na fedha nyingine, tuna uhakika na dawa hizi mpaka mwaka 2026 bila kutetereka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni kweli ipo baadhi ya miradi fedha hazijapatikana, lakini unapokuwa na bunduki unataka kuua adui, unaweza utumie risasi moja ikafanikiwa, unaweza kutumia zaidi ya risasi mbili ama tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye sekta ya afya ili kufanya isimame ni mambo mengi na ndiyo maana tunasema ajenda ya universal health coverage ukiitazama kama lengo endelevu la kidunia lina mambo mengi ndani yake, ni pamoja na hii miundombinu ambayo mmenikumbusha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninadhani Serikali tupo hapa na ninafurahi kumuona Waziri wa Fedha yupo hapa. Tunaendelea kufanya kazi na Waziri wa Fedha kwa karibu kuhakikisha kila bajeti inapopatikana tutaendelea kuimarisha, lakini tunamshukuru Rais kwa ile miradi ambayo tumeshaikamilisha na ninyi Waheshimiwa Wabunge mmempongeza Rais hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi hiyo tumewaambia ni pamoja na vifaa tiba na tumeeleza ni kwa namna gani tumeweza kununua vifaatiba. Waheshimiwa Wabunge ngoja niwape mfano mmoja, ukiacha mbali hii miundombinu ya ujenzi, tumezungumza sana tatizo la cancer (saratani).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwekeza kwenye matibabu ya magonjwa haya ambayo hayaambukizi ni jambo muhimu sana. Ninaomba niwapatie picha tu kidogo, ujenzi wa bunker moja ya kuweka mashine ya mionzi kwa ajili ya kutibu saratani unatumia wastani wa shilingi bilioni 5.5 kwa bunker moja. Ununuzi wa mashine moja ya kisasa toleo la sasa hivi maarufu kama LINAC, mashine hiyo inauzwa shilingi bilioni 7.8 kwa mashine moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ununuzi wa mashine nyingine ambayo ni maarufu kwa jina la COBAT yenyewe siyo chini ya shilingi bilioni 1.9. Hata hivyo ukiangalia CT-Scan the same 1.8 billion shillings. Ukiangalia ile PET scan machine niliyowaambia iliyofungwa pale Ocean Road ni shilingi bilioni 18.8. Ndiyo maana sisi kwa East Africa ni nchi mbili tu tumeweza kuwa na hiyo mashine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, MRI ni zaidi ya shilingi bilioni 2.8; ninataka kusema nini Waheshimiwa Wabunge? Mmeona na mmeshuhudia dhamira ya Mheshimiwa Rais kuwekeza kwenye majengo, mmeona tumefika zaidi ya miundombinu ya kutolea huduma za afya zaidi ya 12,000. Kwa hiyo, tutaendelea kukamilisha majengo hayo yaliyobakia na tutaendelea kuweka vifaa hivi vinavyotumia teknolojia ya kisasa na hali ya juu. Afya kwa Rais wetu ni jambo namba moja ili kuokoa maisha ya wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza Waheshimiwa Wabunge suala la ukosefu wa rasilimali watu. Ninamuona hapa Mheshimiwa Waziri mwenzangu wa Utumishi yupo hapa. Tunajadiliana kila siku tunatokaje? Mheshimiwa Profesa Muhongo ame-provide data hapa jana nzuri za kutosha za namna ambavyo tunatakiwa kuendana na mikataba ya kimataifa. Ile rationale kati ya daktari na mgonjwa inatakiwa iweje? Mheshimiwa Profesa ametuambia aidha daktari mmoja kwa wagonjwa 4,000, aidha daktari mmoja kwa wagonjwa 1,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme kupitia mashirikiano na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora jambo hili tumewaeleza, kwenye taarifa zetu tumepambana na leo tunahesbu watumishi 171,711. Tumepunguza gap, lakini tunakubali kwamba tunatakiwa kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwape tu taarifa ndogo Waheshimiwa Wabunge, sisi kwa mujibu wa taarifa ambazo tumeshirikiana na taasisi na mabaraza ambayo yapo ndani ya sekta ya afya nchini, uwiano wa daktari bingwa kwa sasa umefikia moja kwa 4,000, lakini zipo nchi zinazotuzunguka na sitataka kuzitaja, wenzetu bado wapo kwa daktari mmoja kwa wagonjwa 25,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa ni lazima tuone Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ya kupunguza tatizo hili la watumishi na kama tungepata nafasi ya kutosha Mheshimiwa Waziri wa Utumishi angetoa maelezo hapa, hakika Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuna kila sababu ya kumpongeza, lakini tunapokea hiyo changamoto, ni lazima tuendelee kuongeza watumishi kadri inavyowekezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeniambia na Profesa alisema tunatakiwa kuwa na wataalam wa Telemedicine, Teleradiology na Eco. Ninakubali kabisa na ninamkubalia Mheshimiwa Profesa Muhongo, Mbunge mbobezi kwa mchango wake na ninaomba niseme yafuatayo; kwa idadi ndogo hii ya watumishi ni nini ambacho tumekifanya ndani ya Wizara kwa kushirikiana na wenzetu wa Utumishi. Kwanza tulichoamua, nimesema ndani ya utangulizi, ni lazima twende katika mifumo ya uwekezaji wa sekta ya afya unaotumia sayansi na teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukiweza kufika madaktari bingwa bobezi labda niseme tukifika madaktari 10,000 lakini tukawa na mifumo mizuri ya telemedicine ina maana madaktari wale wana uwezo wa kutusaidia kuwasiliana na vituo vyetu vya afya nchini, zile referral ambazo labda zitaanzia kwenye ngazi ya wilaya kuja kwenye ngazi ya mkoa na ukamuweka mtaalam kwenye ngazi ya mkoa akawasiliana na wataalam waliopo kwenye kata, zahanati kama mtu amefanyiwa kipimo labda cha CT-scan, x-ray ama ultrasound. Kwa uchache huo huo wa wataalam tukienda kwenye sayansi ya teknolojia ya sasa na hasa artificial intelligence na tukaendelea kusimama kwenye telemedicine. Wakati tunaelekea katika matakwa hayo mengine ya kimataifa, lakini tutakuwa tumeokoa maisha ya Watanzania wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mtu anapata kipimo cha x-ray wakati yupo kwenye Hospitali ya Kanda labda Mbeya, anakwenda likizo kwa mume wake Dar es Salaam, anapata ugonjwa au shida kiafya anaenda labda pale MOI kupatiwa matibabu, lakini kwa sababu hatuna hiyo mifumo inayosomana, anaambiwa aanze tena kufanya vipimo vilevile kwa mara ya pili na kwa gharama hizo hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hatuwezi kuvuka wala kufika, ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais na ninaomba niwaambie kwa Hospitali zote za Kanda na Mwenyekiti wa Kamati amelisema sana. Mifumo yote sasa hivi inasomana na hata leo, jana na juzi tumekutana Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa mifumo inasomana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka sasa tuondoke kwenye mifumo kusomana kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa ikasomane kwenye Kanda mpaka Taifa, lakini tushuke mpaka kwenye wilaya na vituo vya afya mpaka kwenye zahanati. Tukiweza kufika hapo tutakuwa tumeitendea haki sana sekta hii ya afya na tutakuwa tumefanikiwa sana kwanza kupunguza gharama za wananchi wa Tanzania katika mfumo mzima wa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani umetoka Songea umepimwa, unafika Njombe unapimwa, unafika Mbeya unapimwa, unafika Dar es Salaam unapimwa kitu ambacho kingeweza kurahisishwa kwa mifumo kusomana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea ushauri huu kwa unyenyekevu na ninawahakikishia kwamba ni maelekezo ya Serikali tutapambana usiku na mchana kuhakikisha mifumo inakuwa ni solution ya uhaba wa watumishi na kupunguza gharama za matibabu katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea hapa hoja nzito kuhusu MSD. Ni lazima tuitazame MSD na Waziri wa Fedha nipo naye hapa atakuwa ni shahidi nimefanya naye vikao vingapi, tumekaa kwa ajili ya kuifanya MSD ifanye kazi vizuri. MSD iliwasilisha maombi ya shilingi bilioni 561.

Waheshimiwa Wabunge, toka MSD hii imeanza ni kwa mara ya kwanza mwaka jana (2024) wamepewa shilingi bilioni 100. Ninaposimama hapa ninaomba niwaambie fedha hiyo whether ni deni ama mtaji wameshaongezewa shilingi bilioni 50 na mpaka sasa wana shilingi bilioni 150, ukiacha mbali juhudi zao wanazozifanya za kuwekeza ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ukiachia mtaji na deni Serikali imeendelea kutoa zaidi ya shilingi bilioni 42 kwa ajili ya kujenga maghala ya kuhifadhia bidhaa zetu za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa mwaka huu wa fedha taarifa ya Kamati ilizungumza madeni ya bidhaa msonge ambayo yamezidi kuifanya MSD iendelee kunyong’onyea katika utendaji wake. Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga tena shilingi bilioni 48.2 kwa ajili ya ugomboaji wa bidhaa za miradi msonge ili kuifanya MSD iendelee kuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iliona hiyo haitoshi, kwa kuwasiliana na wenzetu wa China tunakwenda kupokea fedha ambayo ni grant na siyo mkopo wa dola za Kimarekani ambazo ni sana na shilingi bilioni 119 na fedha hizo zitatusaidia pia kuongeza kwa MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madeni ya TAMISEMI, ninamshukuru Waziri wa TAMISEMI jana wamekutana na MSD wameweka utaratibu wa kuyalipa, madeni ambayo yako kwenye Fungu 52 na mimi mwenyewe Waziri wa Fungu 52 tumeshaweka mkataba na taasisi zote zilipe madeni ya MSD haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, deni la NHIF ninamshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu - Waziri wa Fedha, tumekubaliana kutoa hati fungani ambayo itasaidia kubeba mzigo huo na taratibu zote zimekamilika. Waziri wa Fedha atakapokuja kwenye bajeti yake hili ni eneo ambalo atalitolea tena ufafanuzi wa kina ili tuweze kuiokoa pia NHIF. Lengo la NHIF ku-provide hiyo fedha kwa ajii ya ustawi wa sekta ya afya lilikuwa zuri, lakini tunaamini kwamba kulikuwa na kila sababu ya kuhakikisha tunalipa hayo madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba bajeti ya mwaka 2025/2026 tunakwenda kuanza Bima ya Afya kwa Wote. Lengo la Bima ya Afya kwa Wote ni nini? Ni kuhakikisha uwekezaji uliofanywa na Serikali yetu kila mwananchi wa Tanzania aweze kunufaika na uwekezaji huo. Akitaka matibabu kwenye wilaya, kwenye mkoa, kwenye zone, kwenye taasisi, kwenye hospitali yetu ya Taifa aweze kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umesema vizuri, vifurushi tulivyonavyo vya bima ya afya sivyo vifurushi vya bima ya afya kwa wote. Waheshimiwa Wabunge, kaeni sawa sawa, tutakuja na Bima ya Afya kwa Wote ili iweze kuwasaidia wananchi wote na lengo letu ni kupunguza vifo na kuwafanya wananchi wetu wawe salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli muda ni mfupi lakini ngoja niguseguse tu yote. Mheshimiwa Profesa Muhongo alitu-challenge hapa kama tunaangalia mwenendo wetu unaendana na Sustainable Development Goals na hasa goal namba tatu. Naomba nimhakikishie Profesa tunakwenda sambamba na goal hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kuiangalia goal namba tatu ambayo inahusu sekta ya afya, inatutataka tupunguze vifo vya akinamama na watoto. Waheshimiwa Wabunge, tumpigie makofi Rais, goal hiyo vifo vya akinamama na watoto tumevipunguza. Inataka tupunguze vifo vya watoto under five, tumetoka 67 mpaka 43. Sasa hapo Waheshimiwa Wabunge kama mmenifuatilia kwenye bajeti yangu, hapo hatujafanya vizuri sana, tumeweza kutengeneza uzazi wa dharura, tumetoa watoto tumeweza kuwaweka pembeni, lakini tunahitaji kuwa na Neonatal Intensive Care Unit za kuokoa maisha ya watoto katika vituo vyote vinavyotolea huduma zetu, tumejipanga vituo 100 tutavipa vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu Mheshimiwa Engineer Ulenge alisema jana nakushukuru sana. Hata vile vifaa vya utambuzi wa kusikia tunakwenda kuvinunua na kuviweka kwenye vituo vyetu hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, goal hii namba tatu inaendana pia na goal namba moja ya kupunguza umaskini. Waziri wa Fedha atakapokuja atawaeleza ni kwa kiasi gani Serikali yetu imeweza kupunguza umaskini. Kwa hiyo, goal namba tatu inategemeana na umaskini, goal namba moja inategemeana na goal namba sita kama nitakumbuka vizuri ya uwepo wa maji safi na salama. Kwa hiyo, jambo hilo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Profesa tunakwenda nalo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepambana kuhusu magonjwa haya yanayoambukiza, nilikuwa nafuatilia mchango wa kaka yangu Mheshimiwa Shigongo. Naomba nimhakikishie kwamba kwa sasa kwa kweli tumeshajitahidi kiasi cha kutosha na tumeshafanya kazi ya kutosha. Homa ya hepatitis tumeiingiza kwenye Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Magonjwa Yanayoambukiza. Kwa hiyo, sasa hivi tunakwenda na magonjwa ya ngono, HIV na Hepatitis. Tunapambana nayo yote kwa pamoja na imetusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tumetoka uambukizo wa asilimia 4.3 tumefika uambukizo wa asilimia 3.5; tumpongeze sana Mheshimiwa Rais. Nimekwenda kufuatilia kwa kina, suppliers wetu ambao wamepewa jukumu la kuleta chanjo la hepatitis nchini, kumbe Mheshimiwa Shigongo baada ya kutushauri tulishaachana na ile monopoly ya mtu mmoja, sasa hivi wako wanne na wanafanya kazi hiyo na tumeshaanza kuona kuna dalili za bei kuanza kushuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kujipanga na pale ambapo Serikali itakuwa na uwezo, basi tutafanya kazi ya kuwachanja wananchi kwa kuzingatia utaratibu wa chanjo nchini, kwa sababu ya muda, basi ninaomba tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge Tabasam habari ya Serengeti tumeipata, lakini nimhakikishie Mbunge Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati tutakwenda kuangalia uwekezaji uliofanywa na mwekezaji wetu kule Iringa. Nilisema wakati wa hotuba hapa tunawashukuru pia Ubaya Ubwela kupitia MO Foundation, naye anatusaidia sana sekta ya afya. Tunashukuru sana Wananchi kupitia GSM na wao wanatusaidia sana kwenye sekta ya afya zikiwemo taasisi nyingine za dini, benki zetu na mashirika mbalimbali ambayo yanatusaidia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi kwa kuwa kengele imenigongea na bado nilikuwa na mambo mengi, lakini tutayaleta yote kwa maandishi. Kwa heshima kubwa ya juhudi iliyofanywa na daktari bingwa mbobezi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ninaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kumuunga mkono na kumtia moyo kwa kiasi kikubwa kwa jinsi anavyofanya vizuri kwenye sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapotaka kutoa hoja nitaomba pia nije kuleta mabadiliko wakati nahitimisha vifungu vyangu. Nitaleta mabadiliko ya maneno katika hotuba yangu, ile hotuba kuu ambayo niliisoma mbele yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Waheshimiwa Wabunge ninawashukuru sana kwa michango yenu. Ninawaombea kila la kheri kwa Mwenyezi Mungu mwezi wa 11 tukutane sura hivi hivi tukitazamana humu ndani. Niwahakikishie wananchi wa Tanzania, kama tumefaidi huduma za afya ni kwa sababu Wabunge hawa wameupiga mwingi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumekwenda kwa hatua hizo kubwa tukiongozwa na Mheshimiwa Rais, bajeti hizi humu ndani Wabunge hawa walizipitisha kwa umakini hawakukataa na ndizo ambazo zimekuja kuleta ustawi wa jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, ninaomba niahidi majibu yote nitayaweka kwenye makaratasi na kuyawasilisha kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)