Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia. Waheshimiwa Wabunge niwaombe kwamba hii bajeti ambayo kila mtu anasema ni nzuri tuipitishe, lakini niwakumbushe kwamba makubaliano ya viongozi wa nchi huru za Afrika yaliyofanyika Malabo mwaka 2014, Malabo ni kule Equatorial Guinea, viongozi walikubaliana kwamba bajeti za Wizara za Kilimo za nchi zote za Afrika ikiwa chini kabisa iwe 10% ya bajeti ya Taifa hilo. Kwa hiyo, hapa tunachopaswa kufanya kwanza toka 2014 walisema tulikuwa kwenye bilioni 294 tuko trilioni 1.2, kwa hiyo tutoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwamba tunaelekea. Kwa hiyo, kila mtu ajue bajeti ya mwaka huu ni kiasi gani, halafu apige hesabu kwenye ten percent tuko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili sisi watu wa Jimbo la Musoma Vijijini tuna furaha kubwa sana kwenye hii bajeti, hii ni kwa sababu tunayo mabonde mawili makubwa, Bonde la Mto Suguti na Bonde la Bugwema, mabonde yote mawili yamefanyiwa tathmini na yanafaa kwa umwagiliaji mkubwa na ambalo limepitishwa sasa ni hili Bonde la Bugwema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa shukrani Mheshimiwa Rais alivyokuwa Jimboni kwangu sikuomba vitu vingi nilimwomba viwili tu, bonde hili na barabara na yote tumepata. Tunampa shukrani nyingi sana na Jimbo la uhakika ambalo anajua ana kura nyingi ni la Musoma Vijijini kuzidi yote hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Bonde la Bugwema tumepata, mkandarasi amepatikana. Hili ndugu zangu kwa nini ninamsifia Mheshimiwa Rais ni kwa sababu mwalimu alianza kulijenga mwaka 1974, kwa zaidi ya miaka 50 Mheshimiwa Rais amefufua tena huu mradi sisi watu wa Musoma Vijijini tuna furaha kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu ni kwamba huyu Mkandarasi ambaye atakabidhiwa hivi karibuni malengo ya mwalimu ya miaka ya 1970 kwamba asaidie wakulima wadogo yapo pale pale, kwa hiyo, hili ni bonde kwa ajili ya wakulima wadogo na wakulima wakubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hatubahatishi tumeshapanga na mazao yatakayolimwa humu, kwanza ni mpunga, pili ni mahindi, tatu ni alizeti. Halafu tunachukua mazao haya yanayofanana fanana yaani mbaazi, dengu, choroko na maharage vilevile tutalima pamba. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Bashe kwa kazi nzuri unazozifanya usishawishike Bonde la Bugwema kuanza kulima miwa, hesabu na mimi nipo kwenye Kamati ya Kilimo hesabu tuliyonayo ni kwamba kuanzia mwakani tutakuwa na sukari ya kutosha kwa hiyo Watanzania kila mabonde yote yasigeuke kuwa mabonde ya miwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni biashara, mazao tuliyoyachagua ni kwa sababu tutafanya biashara ya ndani mwaka huu tuko watu milioni 70.5, mwaka 2050 wakati tunatimiza dira yetu tutakuwa watu karibu milioni 140. Kwa hiyo, soko la ndani limo ndiyo maana tunataka kilimo kikubwa kwenye Bonde la Bugwema halafu soko la nje ni nchi za Kiafrika tuna mikataba mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Afrika tuko watu bilioni 1.5 tukifika mwaka 2050 tutakuwa bilioni 2.5 wote hawa wanataka chakula na wote hawa huenda wataanza kununua kutoka kwenye Bonde letu la Bugwema. Sasa ninatoa umuhimu wa kilimo ni biashara. Mpunga tunataka kuulima kwa sababu duniani ambapo sasa hivi kuna watu bilioni 8.2 zaidi ya 50% wanatumia mchele, wali au mpunga kama chakula kikuu 50% kwa hiyo hatutofanya kosa sisi kulima mpunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile soko la mpunga miaka mitatu inayokuja duniani ukubwa wake kibiashara utakuwa wa bilioni 350 na sisi tunataka tunyemelee hilo soko. Mahindi yanamatumizi matatu kama chakula kwa binadamu kwa mifugo halafu viwandani yanatumika kutengeneza ethanol, kwa hiyo tukipata mengi sana tunaweza kufikiria mambo ya ethanol.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaazi tunazichagua kwa sababu biashara yake sasa hivi duniani ni bilioni 68 na ikifika mwaka 2030 itakuwa ya bilioni 75 kwa hiyo Mheshimiwa Bashe uko sahihi kusema ‘Kilimo ni Biashara’ na sisi Musoma Vijijini tunaenda mbali tunataka viwanda. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge isiwe tu kwamba kilimo ni biashara lakini kilimo vilevile ni viwanda, kwa hiyo sisi tunataka mazao yatakayolimwa kule Bugwema kwenye bonde kubwa kabisa, yatakuwa yanachakatwa na humo na tunaongezea thamani ya mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunalima pamba ombi letu ni kwamba ile ginnery ya Mgango, Waziri Bashe ile ginnery unafahamu na Waziri wa Viwanda lazima ile ginnery ifufuke halafu pamba tunayoilima tunataka kuanza kiwanda kipya pale majirani zangu Musoma Mjini wawe na kiwanda. Huko Bugwema kuna wafugaji sana, tunataka kufufua viwanda vyetu vya maziwa vya Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara na Musoma Vijijini tumeanza uvuvi wa vizimba na huko Musoma Vijijini mimi nimepanga ndani ya miaka minne ama mitano tuwe na Kiwanda cha Samaki Musoma Vijijini. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuende na kilimo ni biashara tuende na kilimo ni viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuwaeleza kidogo kuhusu maji ya Ziwa Victoria, maana tunataka kuyatumia sisi binadamu, mifugo yetu inataka kutumia maji ya Ziwa Victoria na sasa tumeingia ukulima mkubwa wa umwagiliaji wa kutumia maji ya Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaenda kujadiliana na nchi zingine ambazo zinatumia maji ya Ziwa Victoria ninaomba jamani mjaribu kutumia watu wa Musoma Vijijini ambao wana historia nzuri ya Ziwa Victoria. Ziwa Victoria siyo la zamani sana umri wake ni miaka laki nne tu siyo la zamani sana. Kwa hiyo wale wenzetu wa Kaskazini na hii point ni muhimu sana, watakaokuwa wanaenda kwenye discussions na nchi za Kaskazini tunasema Lake Victoria is four hundred thousand years old, lakini Mto Nile wanasayansi zamani walipiga mahesabu wakadhani Mto Nile umri wake ni miaka milioni tano, lakini juzi mahesabu yamepigwa upya tena Mto Nile unaonekana umri wake ni miaka milioni thelathini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mtu akija kusema msitumie maji ya Ziwa Victoria kwa kuwa yataisha kwenye Mto Nile lazima ufanye majadiliano ya kisayansi, kwamba Mto Nile ulikuwepo kabla ya Ziwa Victoria kuwepo na maji ya Mto Nile tutaongea siku nyingine huwa yanatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Ziwa Victoria nalo tulitumie kwa umakini mbali ya kuwa na umri wa miaka laki nne Ziwa Victoria limewahi kukauka mara kadhaa, lakini msiogope, limewahi kukauka mara kadhaa, mara ya mwisho kumbukumbu zetu huku kwa wanasayansi huku ndiyo zinakuwa kumbukumbu tu, pengine Daktari zipo? Haya. Kumbukumbu zetu ni kwamba mara ya mwisho lilikauka ilikuwa ni miaka 17,000 iliyopita, kwa hiyo ni siku nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna haki ya kutumia maji wa Ziwa Victoria kwa sababu 49% ya Ziwa Victoria iko Tanzania, Uganda ina 45%, Kenya wana asilimia sita. Kwa hiyo, kama tunatumia kwa uwiano tuna haki ya kufanya kilimo kikubwa cha umwagiliaji kwa kutumia maji ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mto Nile ambao mnaweza kuanza kuwa na wasiwasi, nimewaeleza ni wa umri wa miaka zaidi ya milioni 30, halafu hesabu imepigwa discharge yake yale maji yanayotembea Mto Nile mle ndani, discharge yake kwa sekunde moja ni lita milioni 3.5 yaani ile average discharge ni 3.1 million liters per second. Kwa hiyo, ukichukua maji yanayoweza kutunzwa kwenye Mto Nile na Maziwa yake na mito yake storage capacity yake kwa mwaka ni cubic meter bilioni 180 ambazo ukipiga mahesabu ni sawasawa na cubic kilometer 180. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujazo wa Ziwa Victoria, ni cubic meter 2,760, ukipiga hiyo ratio ni less than ten percent, kwa hiyo ndugu zangu Watanzania tuna haki ya kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa binadamu kwa mifugo na bado kwa umwagiliaji na siku tutakavyoitwa kwenye huo mjadala nimesema kodisheni majeshi kutoka Musoma Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa upande wa umwagiliaji kwa nini lazima tufanye umwagiliaji? Siyo kitu kigeni sisi tumechelewa, mambo ya umwagiliaji yalianza kabla hata ya Jesus Christ, inajulikana kwamba miaka 6,000 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo. Mambo ya umwagiliaji yalikuwa yanafanyika kwenye kule Middle East, nchi hizo zamani zilikuwa zinaitwa Mesopotamia kwenye Mto wa Tigris na Euphrates. Kwa hiyo jamani sisi tumechelewa kufanya kilimo cha umwagiliaji na ninaomba niunge hoja kwa sababu niliambiwa ni dakika tano kumbe wameniongeza dakika, tayari zimekwisha? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya nimalizie na Mheshimiwa Musukuma ame-support haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jamani namalizia kwa kusema kwamba tunachoiomba Serikali kwenye mpango wa maendeleo, kwenye ile draft wale wa mpango wa maendeleo lazima hili suala la umwagiliaji waweke kipaumbele kikubwa, kwa sababu uchumi mkubwa na watu wengi walioajiriwa ni kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)