Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia hii sekta ya uzalishaji, moja ya sekta ambazo nimeziishi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo manne ya kusisitiza kabla ya sijazungumza. Mafanikio katika hii Wizara, katika Serikali yanaonekana, tumeona ongezeko la uzalishaji, tumeona ongezeko na bei nzuri ya mazao, ninashauri kwamba tuongeze zaidi uzalishaji tukilenga zaidi kwenye kuongeza tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika kwamba wengi tumepata mavuno makubwa lakini siyo kila sehemu tumetumia tija kubwa. Suala la pili unapokuwa umeongeza bei, wananchi wanafurahia zao lile, tuongeze mazao zaidi wananchi waepuke kutegemea zao moja wawe na portfolio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwetu Kagera tuliwahi kutegemea kahawa ilipoanguka kilikua kizaazaa na ni historia mpaka watu wakakata mibuni yao tumekuja kuamka leo. Tuwekeze katika kutafuta masoko, Mheshimiwa Waziri wekeza katika kufuta masoko. Watu wanapofurahia kilimo unapowahimiza kulima wanapozalisha mazao lazima tuwape assurance ya kufuta masoko. Nichukue fursa kuishukuru Serikali na kipekee Mheshimiwa Rais katika hii diplomasia, diplomasia ya uchumi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina uzoefu katika masuala ya masoko, kuna masoko tulishindwa kuyaingia lakini sasa hivi masoko hayo yanatutafuta, hii ni diplomasia ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni maeneo ya kilimo. Nawapongeza Serikali kwa kujenga sekta za umwagiliaji na napongeza mpango wao wa kuja na umwagiliaji mdogo mdogo. Ninashauri maeneo madogo madogo yapewe kipaumbele kwa sababu matokeo yake yanakuja mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ya kulima kuna matumizi bora ya ardhi (land classifications). Unakuta mtu anapanda mazao katika eneo ambalo halipaswi kupandwa. Mfano rahisi ni kwetu, sisi kwenye land classifications - daraja one na two tumepanda miti na haipaswi, miti inapaswa kupandwa tabaka la sita ama la saba hata jangwani kwenye tabaka la nane nitalieleza zaidi, lakini kwetu Kagera tunalielewa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu katika maeneo ya kulima kuna kurejesha ardhi. Kuna maeneo leo hatulimi kwa sababu unakuta ni tambarare kama barabara, watu wameharibu mazingira. Lazima tutafute mbinu za haraka namna ya kutumia maeneo hayo kwa sababu eneo haliongezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namba tatu; nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa BBT ngazi ya Halmashauri; ninadhani hapa tumekubaliana na tofauti zetu sasa zimekwisha. Hii BBT ya Halmashauri ni dawa ya Kichina, Mchina ukiumwa jicho anapiga sindano kwenye jicho. Hii BBT ya Halmashauri inawafuata watu mahali walipo, hakuna haja ya kuzoea mazingira. Kama kwenu ni Moshi tunaku-BBT Moshi, kama ni Songea tunaku-BBT Songea na kwetu Makongora tumeshaanza kuwa-BBT vijana na Taifa letu linakwenda kuangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, marekebisho kwenye BBT ya Halmashauri; tusiwalenge vijana na wanawake tu, tuwalenge waliotayari. Wapo watu wana miaka 50 si vijana hawa ni wanaume, lakini wapo tayari kutumika. Wapeni hizo ruzuku, wawezeshe waweze kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais na nimshukuru. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri ile hadithi imefika mwisho, lakini ikafika mwanzo wa mwisho. Mradi wa Mto Ngono umefika mwisho sasa na tunaanza mwisho wa mwisho. Nimesikia taarifa yake wameshapima, unatafuta wakandarasi. Niwaombe wakandarasi wa dunia nzima ikiwemo Uyahudi, Argentina, (mabingwa wa irrigation), njoo mchangamkie utengenezaji wa hekta 16,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Waziri mtumishi wake wa umwagiliaji Kagera anastahili amwandikie hata barua. Jana lilipojibiwa swali langu hapa kuhusu mawanda ya Bonde la Mto Ngono, kijana yule baada ya saa mbili alikuwa site katika Kata ya Katoke, akiainisha eneo la kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyozungumza Mheshimiwa Profesa Muhongo, sisi umwagiliaji wa Kagera tunahusisha kilimo cha kahawa na nikipata nafasi nitazungumzia kwa nini tunakwenda kwenye coffee. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunahusisha mpunga lakini tunahusisha malisho ya mazao kwa sababu fursa ya Mkoa wa Kagera ni uwekezaji katika ufugaji hasa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na mbuzi (bidhaa ambazo zimepata soko kule duniani). Kwa hiyo, mazao kama Jongos, Napier, Usin, tunakwenda kuyalima. Hiyo ni katika kuongeza wigo (diversification) na kujenga portfolio ili mkulima asitegemee zao moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchangia. Nimezungumzia umwagiliaji wa kahawa. Sisi tunapanga mwaka kesho tuzalishe tani 85,000. Ninatambua juhudi za Serikali lakini hapa siyo tunapopaswa kuwa. Hatupaswi kuwa hapa. Mheshimiwa Kavejuru jana amezungumza hatupaswi kuwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nchi ya Uganda ambayo eneo lake la kulima kahawa ni sawa na Mkoa wa Kagera, mwaka jana wamepata 1.5 billion US Dollar. Sisi tunalima tani 85,000 wao wapo kwenye tani karibu 380,000; haikubaliki. Nikushukuru Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri aliniita tukakaa chini akasema tufanye nini? (Makofi)
 Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ni kuongeza tija, lakini pia kuweza kufanya irrigation kama ambavyo tumeamua sisi tunaanza kufanya irrigation. Sisi maamuzi ya Mkoa wa Kagera chini ya Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, RC Fatma Mwasa ni kwamba anatafuta ekari 10,000 Mkoa mzima wa Kagera, lakini ukifika Muleba Kituo cha Basi, swali la kwanza unaulizwa nioneshe unapolima na kama hulimi mibuni, haujalima chochocte kwa Kagera. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, the concept is, kama sisi Tanzania tunaweza kupata mazao export 3.54 billion na Uganda anaweza kupata 1.5 billion na sisi tunamzidi ardhi ukijumlisha eneo lote la Tanzania; hii maana yake ni kwamba tukiwekeza nguvu zetu na tunaweza. Ninatambua mikakati yako Mheshimiwa Waziri, tunaweza kupata Dola bilioni nne kwenye kahawa tu. Sasa, haya mazao mengine yakasindikiza, unakuta haraka kuna leap frog na kwenda kwenye Dola bilioni 10 kutoka kwenye mazao tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo tena mazao mengine niliyochagua suala la mpunga au mchele. Afrika tunatumia tani milioni 60 za mchele, lakini Tanzania tunayo potential ya kuzalisha tani 14,000. Sasa, ufanye mahesabu utaona kwa nini mimi ninawatabiria kwamba tunaweza kwenda kwenye uwezo mkubwa wa kuleta fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni zao la kakao. Kakao ina bei kubwa lakini tasnia ya chocolate ambayo inategemea kakao ni Dola milioni 110 duniani na kakao yenyewe ni Dola bilioni 17. Sasa Mheshimiwa hapa tunachopaswa kufanya katika vipaumbele vyangu vile katika uangalizi kwamba tutambue maeneo Tanzania ambako tunaweza kulima kakao, tulime kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kufanya, Kiwanda cha Kakao sio muujiza. Nguvu ya kakao ni industry ya chocolate. Sasa kutengeneza chocolate siyo sawa na kutengeneza satellite ya kwenda mwezini. Tuwakamate Watanzania hawa, tuwafundishe kuanzia viwanda vidogovidogo, viwanda vya kati, kusudi wawekeze kwenye kakao na chocolate tuweze kuuza chocolate, Tanzania, Afrika Mashariki na Dunia nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la horticulture. Horticulture inavutia, tuwapatie nguvu watu wa maparachichi. Ninamwambia Waziri watu wanasema mazingira ya biashara ya Tanzania, haimhusu yeye ni Serikali nzima, si mazuri. Mtu anatoka Njombe na gunia lake la avocado kupeleka sample tani 100, anasimamishwa na watu 1,000, kila mtu anamdai ribora. Kwa hiyo, mazingira (the ease of doing business) haijawa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la sukari. Potential ya Tanzania kwenye sukari ni tani 2,000,000. Hili suala ninalijua na nimelifanyia kazi. Kwa hiyo, tuhimize watu na namna ya kuhimiza ni kuhimiza kwenye viwanda vidogo, ili ile import ya industrial sugar tu-refine Tanzania sugar yetu, lakini tuweze ku-satisfy soko letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa faida ya muda, ninaomba kuunga mkono hoja. Safari imeanza na ni safari ya uhakika. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais. Tunakwenda. (Makofi)