Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kunipatia nafasi ya kuzungumza ili niseme machache kuhusu Wizara nyeti kabisa katika nchi yetu, Wizara ya Kilimo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, mzee wa speed 120 Mwijage ametoka kumaliza sasa hivi, ameonesha kwamba; katika nchi ambazo kuna gap kubwa kati ya matajiri na maskini na maskini wengi wakilengwa kuwa ni wakulima, ni muhimu speed ya Wizara ya Kilimo ikawa ndio matarajio yetu ya ku-close gap kati ya maskini na matajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama namna ambavyo Mheshimiwa Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara wamejipanga unaona wamechechemua kilimo chetu, sasa tunajadili kilimo cha biashara kutoka kilimo cha kujikimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeiona katika kilimo. Kwa Mkoa kama Dodoma ambapo tuna tatizo la kuwa na mito inayotiririka maji muda wote, hututegemei kuingia kwenye kilimo cha umwagiliaji bila kutujengea mabwawa, kwa sababu Mkoa wetu sisi mito yetu inatiririka na kuondosha maji moja kwa moja. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namna pekee ya kutufanya tuingie kwenye ushindani wa soko la umwagiliaji ni kutengeneza mabwawa makubwa ambayo tutatunza maji halafu maji hayo tutayatumia katika kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, niwe na shukrani kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Mvumi kwa ajili ya Serikali kukubali kuanza kutujengea mabwawa mawili makubwa pale Kata ya Manda na Mpwayungu. Hii itakuza uchumi wa eneo lote la Wilaya ya Chamwino. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tumemwona akifanya vitu ambavyo si vya kawaida. Kwa mfano, wote tulikuwepo hapa wakati wa sakata la sukari na bei ya sukari tukafikiria itaishia kwenye shilingi 5,000 mpaka 6,000 lakini kwa kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe na timu yake, leo sukari ipo shilingi 2,500. Kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri maana yake Watanzania kama ingebaki ile ile, leo shutuma zote zingekuwa kwake. Ila kwa namna ambavyo wamepambana, wamefikisha mahali ambapo baadhi ya watu hawaamini macho yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tumeona Wizara ikiagiza mitambo ya kuchimbia visima vikubwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Tumwombe tu Mheshimiwa Waziri mitambo ile itakapozinduliwa na Mheshimiwa Rais na kuanza kufanya kazi basi na sisi wa Jimbo la Mvumi watukumbuke, ili tuweze kupata visima vikubwa. Maji yapo chini, kama tumeyakosa maji ya juu basi tupate haya maji ya chini ya ardhi, ili yaweze kutusaidia katika kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tumeona akipambana kuhusu mbolea. Tuna kiwanda cha ndani hapa Dodoma; kiwanda pekee cha mbolea kinatengeneza mbolea ya kukuzia, mbolea ya kupandia, mbolea ya kunenepesha mazao. Hiki kiwanda kimekuwa na tatizo la madai ya ruzuku yao. Kwa hiyo, tumwombe Mheshimiwa Waziri awasaidie wawekezaji wa ndani wanahitaji kulindwa. Hawa watu wanaajiri watu wengi, wanatusaidia mno, mbolea yao inafika kwa wakati. Kwa hiyo, ni vyema akawawekea ulinzi maalum wa kupatiwa fedha zao ili waweze kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaendelea kuwatia moyo Mawaziri pamoja na Katibu Mkuu na wenzake wote, kazi wanayoifanya ni kazi nzuri. Hii BBT ambayo imezungumzwa hapa, nimwombe Mheshimiwa Waziri, si kazi yake kujenga barabara lakini pale Ndogoye ambapo yeye ananielewa nikisema hivyo, kuelekea kwenye shamba lake kubwa pale watutengenezee barabara pale. Siku Mheshimiwa Rais atataka kwenda kule, mbadala watatumia helicopter kumbe wanakimbia kwenye ule mlima. Hebu nimwombe atazame ule mlima, aone namna bora ya kushirikiana yeye na TAMISEMI kuweza kuuweka vizuri ili mazao yetu yaweze kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la muhimu kabisa nimwombe Mheshimiwa Waziri atusaidie wakati akijibu hapa, wamefikia wapi kutengeneza ile Wakala ya Ugani ambayo Mheshimiwa Rais ameiagiza. Tunaomba tupate majibu, tuone hatua ambazo wamezifikia ili kuweza kuongeza speed ya usimamizi wa wafanyakazi hasa Maafisa Ugani ambao wanasimamia kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kuhusu stakabadhi ghalani. Kwetu sisi hapa panahitaji elimu. Watu wakielewa, wakaona wananufaika, watasimamia wenyewe. Ukiona mahali watu wanakataa kitu, siyo wanakataa kitu kizuri kwa sababu ya ujinga, wanakataa kwa sababu hawakifahamu. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tufahamisheni na sisi siku moja tusimame tuzungumzie kama Mtwara wanavyozungumza, tuzungumze kama Lindi wanavyozungumza na sisi tuwatoe wakulima wetu kutoka Kata ya Manda, Mpwayungu, Makamo waende wakajifunze namna ambavyo wenzetu wananufaika na hiyo stakabadhi ghalani, lakini kutueleza tu kwamba kuna stakabadhi ya ghala bila watu kujua manufaa yake hii nayo inaleta tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ninawatakia kila la kheri. Ahsanteni sana. (Makofi)