Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana ambayo ina jumla ya kiasi cha fedha trilioni 1.24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo kwa kweli Taifa letu limekuwa likisonga mbele pakubwa sana katika maendeleo hasa katika Sekta hii ya Kilimo kwa sababu imekuwa ikipewa kipaumbele sana katika hii Awamu ya Sita na hasa kwa kutengewa fedha nyingi za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukishuhudia performance kubwa sana katika eneo la kilimo na hasa katika hii Miradi mikubwa ya BBT ambayo kwa kweli tumekuwa tukizalisha vijana wengi ambao sasa wameanza kusaidia katika Sekta ya Kilimo, hasa huko wilayani ngazi za chini sana; wamekuwa msaada mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu kwa kweli tunaamini kama utasimamiwa vizuri; na ninampongeza na kumsisitiza Mheshimiwa Waziri kwamba aongeze juhudi ya kuhakikisha uzalishaji wa vijana hawa uendelee kwa sababu ndiyo msingi mkubwa wa mafanikio katika sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri Bashe, Naibu Waziri Mheshimiwa Silinde, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watumishi wote ambao kwa kweli kimsingi wamekuwa pamoja kabisa kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwanza kuzungumzia eneo la pamba. Mimi ninatoka Mkoa wa Shinyanga ambao ni mkoa wa pili katika uzalishaji wa pamba. Kimsingi unapozungumza Shinyanga uzalishaji wa pamba unazungumzia Wilaya ya Kishapu. Pamba yote inayozalishwa katika Mkoa wa Shinyanga 75% inatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu. Kwa hiyo, unapozungumza pamba Shinyanga maana yake unazungumzia Wilaya ya Kishapu ambayo ni Jimbo la kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka tu niseme zipo changamoto hasa katika masuala ya pembejeo, lakini kwa bahati mbaya sana ni utaratibu tu. Pembejeo inatoka lakini inatoka katika utaratibu wakati mwingine si mzuri na hasa viuatilifu (dawa za kuua wale wadudu na mbegu kwa ajili ya kilimo) na mbegu kwa ajili ya kilimo zinafika si katika wakati mzuri. Mbegu zinatakiwa zifike mapema kuanzia mwezi Agosti katika msimu wa pamba kwa sababu msimu wa kilimo unaanza mwezi Oktoba, ndipo tunapoanza maeneo ya kwetu huko Kishapu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri mbegu ziwe zinafika mwezi Julai na mwezi Agosti uwe ni mwezi wa mwisho. Pia, mbegu zile zitolewe kwa mujibu wa ile allocation iliyotolewa katika kila eneo kulingana na takwimu za idadi ya wakulima na ukubwa wa maeneo ya mashamba kwa sababu napo pamekuwa na tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukifika mahali mbegu zenyewe inabidi tena uombe ombi maalum la kuomba maeneo ya kata kadhaa ziongezewe mbegu, as if kama hakuna takwimu katika Idara ya Kilimo. Kwa hiyo, eneo hili ninafikiri wawe smart zaidi ilimradi mbegu ziwe za kutosha kuanzia mwanzo wa msimu mpaka mwisho wa msimu. Kwa hiyo, eneo hili ninaomba lizingatiwe sana ilimradi tuwasaidie wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa viuatilifu kumekuwa na tatizo kubwa sana. Kuna wakati pamekuwa pakitokea upungufu mkubwa wa dawa hizi kwa ajili ya kupulizia wadudu waharibifu. Kwa hiyo, hili jambo linatakiwa na lenyewe lisimamiwe, dawa ziwe za kutosha na ziwafikie wakulima kwa usahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita hasa kupitia Mheshimiwa Waziri kwa usimamizi mzuri sana wa hii Wizara ya Kilimo kwa namna ambavyo kwa kweli udhibiti sasa umekuwa mzuri. Dawa zinafika za kutosha isipokuwa ule wakati, ninaomba sasa jitihada hizi ziendelee kwa sababu wakulima wameanza kuona manufaa makubwa. Sisi tunasema ruzuku ambayo imekuwa ikitolewa katika dawa na mbegu inasaidia sana kuongeza ari ya wakulima kuendelea kulima zao la pamba. Kwa hiyo, hili nilitaka nilisisitize sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nilitaka nizungumzie suala zima la bei ya mkulima wa pamba. Bei hii siyo nzuri, tupo shilingi 1,100 na 1,200. Bei hii siyo nzuri. Zao la pamba lina mchakato mrefu sana katika kuliandaa kwenye kilimo kuanzia kuandaa shamba, kuja kupalilia, kuna masuala ya kunyunyuzia dawa, kuna masuala ya mavuno, ni gharama kubwa sana. Mheshimiwa Bashe wewe bahati nzuri unatoka kanda ambayo tunalima pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ekari moja tunapata kiasi kidogo sana cha fedha, lakini huwezi ukaamini ni kwa nini Serikali yetu tumekuwa tukilizungumza suala zima la kutengeneza kwanza, mjengeko wa bei na pia kuhakikisha kwamba tunatengeneza namna ya kulinda bei ya zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishasema kwamba tutaanzisha Mfuko wa Kulinda Zao la Pamba, lakini jambo hili limekuwa halitendeki. Mwaka kila mwaka tukizungumza halitekelezeki. Ninakumbuka yeye mwenyewe wakati hajawa hata Waziri moja kati ya jitihada zake ambazo alikuwa anazizungumzia ni suala zima la kumlinda mkulima kwa kutengeneza namna nzima ya kulinda bei ya zao la pamba, lakini jambo hili halifanyiki. Ninaomba sana jambo hili lifanyike haraka. Wachakate, wafanye utaratibu wa namna yoyote ambayo itasaidia sana kuhakikisha kwamba, stabilization ya price ya zao la pamba inakuwepo, kwa maana ya kuhakikisha kwamba tunalilinda hili zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nilitaka nilizungumzie ni suala zima la ginnery. Tuna ginnery ya Mhunze ambayo ni ya muhimu sana. Mheshimiwa Waziri aliahidi mwaka wa fedha uliopita kwamba, angetusaidia fedha upande wa SHIRECU ilimradi ginnery hii tuiponeshe, tuweze kusaidia pamba inayovunwa katika eneo la Kishapu izalishwe pale. Kiwanda hiki kinaenda kusaidia hata masuala ya ajira kwa watu wetu wa Mji wa Mhunze na kuuchangamsha Mji wa Mhunze pamoja na kupunguza tatizo la ajira katika Wilaya yetu. Ninaomba sana eneo hili alitazame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake kwa kweli ninamsifia sana Mheshimiwa Waziri, alizungumzia mambo mengi sana. Sisi tunasema katika Wilaya Kishapu tumefanikiwa pakubwa sana. Alituletea matrekta 22 na yametusaidia sana katika Wilaya yetu katika kuhakikisha kwamba kilimo cha pamba kinakwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pia amemsaidia sana mkulima. Tunampongeza sana na kwa kweli Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hatutaweza kuisahau katika Wilaya ya Kishapu kwa sababu sasa tunalima pamba kwa bei ya shilingi 35,000 kutoka shilingi 70,000. Tumpe nini Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunasema 2025, mwaka huu, majibu watakwenda kuyaona katika Wilaya ya Kishapu. Tunaomba tu, Mheshimiwa Waziri, matrekta haya yaendelee kubaki kusaidia katika kusukuma uzalishaji wa zao la pamba katika Wilaya yetu ya Kishapu. Mheshimiwa Waziri, nilikuwa ninataka nizungumzie, nimekusikia katika suala zima la uuzaji wa godown la SHIRECU, ambalo liko kule Kurasini, Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili godown kwa mwaka mmoja linatusaidia karibu shilingi milioni 900 kwa kodi tunazopata kutokana na ukodishaji kwa mwaka mzima. Zaidi ya shilingi milioni 900 ambazo zimesaidia SHIRECU kutembea, walau kuwa na uhai kwa sababu, hatuzalishi pamba. Sasa kwa sababu, nimesikia katika hotuba ya Waziri ameweka utaratibu wa kutaka kuuza godown lile, basi baadaye fedha zile zisaidie upande wa SHIRECU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, kwanza ushirikishwaji ufanyike ilimradi tuweze kutoa tafsiri nzuri kwa sababu, maneno ni mengi. Tuko Wabunge tunaotoka Mkoa wa Shinyanga, nina hakika akituhusisha tunaweza kusaidia na hasa eneo lile linalozalisha pamba. Pia, ninafikiri tathmini ifanyike vizuri kwa sababu, godown lile tunaweza tukapata fedha nyingi sana, kama kweli litauzwa. Maana evaluation report ikishakuwa imetoka, tuone kama faida ipo ama haipo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu zile zizingatiwe katika suala zima la uuzaji wa mali ya wakulima kwa sababu, lazima Mkutano Mkuu wa Wanachama uridhie na ukubaliane kwamba, kuna haja ya kuuza, baada ya maelezo na sababu za msingi zitakazokuwa zimetokea. Vinginevyo ninaona ni godown ambalo limekuwa likitupa fedha nyingi sana, zaidi ya shilingi milioni 900 na ninadhani kwa mwaka unaokuja 2026 tutakwenda kuwa tunapata, kwa kodi tu, shilingi bilioni moja kwa mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninafikiri tutapata wakati mzuri wa kutueleza hata sisi wawakilishi kujua umuhimu wa kuuza godown lile ilimradi lilete manufaa kwa mambo mengine. Vinginevyo tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, katika hotuba yako nimeona kuna magari 44 unaenda kuyatoa; ninashauri sana Wilaya ya Kishapu kwa sababu, ni wilaya ya kimkoa katika uzalishaji, kama inabeba 75%, ninaomba katika suala zima la ku-allocate hayo magari Wilaya ya Kishapu ipate gari moja kwa sababu, ni eneo kubwa sana lile la uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Vyama vya Msingi 88 sasa, si jambo dogo. Kwa hiyo, ninaomba katika yale magari kwa kweli, Waziri aelekeze Wilaya ya Kishapu, ilimradi kuongeza nguvu ya uzalishaji wa zao la pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka ...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, nikutakie kila la heri Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri. Ninaunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)