Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa muda huu. Nianze kwa kumpongeza Waziri wetu wa Kilimo pamoja na watendaji wake wote kwa kazi nzuri ambazo wamefanya. Mimi nimekuwa kwenye Sekta ya Kilimo tangu nikiwa kijana mdogo, kuanzia mwaka wa 1975 mpaka mwaka wa 2020 nilivyostaafu na kuja kwenye siasa. Nimeona mambo mengi sana, nikiwa kama mtumishi katika Wizara ya Kilimo na niseme ukweli nimepitia Marais wote ambao wameiongoza nchi hii, kuanzia Hayati Mwalimu Nyerere mpaka kwa Dkt. Mama Samia hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa viongozi wetu hawa walikuwa na utashi mzuri wa kisiasa wa kukiendeleza kilimo na kumwondolea mkulima umaskini, lakini Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na utashi wa kisiasa alikuwa na kitu cha ziada na anacho, anafanya kwa matendo. Ninasema hivyo kwa sababu, Rais wetu huyu ameongeza bajeti ya Wizara hii kutoka kule ilikokuwa aliposhika madaraka, mpaka ikafikia 1.2 trillion. Hiki ni kitu kikubwa amefanya Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amemteua pia Waziri ambaye yuko makini kimatendo, anafanya kazi na zinaonekana. Ninaona hapa wamejiandikisha watu 65 kuchangia na ninajua wengine wamekatwa; kila mtu alitaka aseme kitu kuhusu Wizara ya Kilimo na utendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha tatu, amemteua mshauri wake mkubwa kabisa wa kilimo, mtoto wa mkulima, Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda, anamshauri mambo ya kilimo nchi hii. Ameteua Wenyeviti wa Bodi na ma-CEO ambao wanafanya kazi na tunaona mambo yanakwenda. Sisi tumpe Rais wetu maua yake kwa haya matendo makubwa ambayo ameifanyia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna nukuu moja ametoa, ambayo imeugusa moyo wangu na mioyo ya Watanzania wote. Ninaomba nimnukuu: “Hatuwezi kuuondoa umaskini, kama hatuwezi kuwaondoa wakulima wadogo kwenye umaskini”. Hili ni jambo kubwa na ndiyo commitment ya hii Wizara, Waziri wetu na wasaidizi wake kwenye kuondoa umaskini katika nchi hii. Niendelee kumwomba Waziri, kamata hapohapo tumsaidie mkulima mdogo aondokane na umaskini, fadhila zake atazipata kule juu mbinguni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kabla sijaanza kuchangia nimpe ombi Mheshimiwa Waziri. Kwenye jimbo langu nina Skimu ya Umwagiliaji ya Mabogini pale, ilijengwa miaka ya nyuma, imeshachoka sana, inahitaji iboreshwe watu wapate maji mengi na tuendelee kuzalisha mpunga kwa uhakika. Hii ni skimu ya uhakika ya mfano hapa nchini, imechoka tunamwomba aje atusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Mandakamnono, ninashukuru inaendelea. Tukazanie ujenzi ili iishe, wale wakulima waanze kuzalisha mpunga pamoja na kuboresha ile Skimu ya Makeresho. Tunaomba waendelee kutusaidia, ikiwepo ile Skimu ya Arusha Chini, ambayo Waziri alishatuma wataalam wakaja kule, lakini bado haijaingia kwenye mpango. Ninamwomba chonde chonde tusaidiane, ikiwa ni pamoja na kuboresha mifereji ya asili na kupatiwa miche ya ruzuku ya kahawa. Bado wakulima wa Mkoa wa Kilimanjaro wanahitaji miche ya kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya ombi nianze kutoa ushauri. Ninataka nichangie tu ni nini kifanyike, ili Sekta ya Kilimo iweze kumwondolea mkulima umaskini. Tuweke mkazo kwenye vitu vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, nitasema bajeti iongezeke. Ninakubaliana na Profesa Muhongo kabisa kwamba, Malabo walipokaa Viongozi wa Nchi mwaka 2003 na Maputo 2014, tulikubaliana chini kabisa iwe 10%. Sasa hebu tujiulize, tukimpa Mheshimiwa Bashe na jeshi lake 10% ya bajeti, ambayo ni karibu shilingi trilioni 5.5 na siyo kwamba tunashindwa, ni nini kitatokea nchi hii kwenye Sekta ya Kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa kuwa, Rais wetu ana utashi wa kimatendo pamoja na wa kisiasa kumsaidia mkulima, hii bajeti iongezwe. Nitatoa mfano, kule Israeli walipopata tu uhuru, 30% ya bajeti yao ilikuwa kwenye kilimo na leo tunaona Israeli ni Taifa kubwa linalolima kwa wingi, pamoja na kwamba, nchi ya Israel inaingia mara 42, Israel 42 ndiyo Tanzania yetu, lakini ni giant wa kilimo duniani kwa sababu, waliwekeza vizuri kwenye kilimo. Kwa hiyo, niiombe Serikali itafakari na kuiongezea hii Wizara pesa. Bado hii shilingi 1.2 trillion haitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, ni kuimarisha ushirika. Ushirika ni component muhimu sana. Hata kule Israeli walipokuwa wameanza kuboresha kilimo waliunda vyama vya ushirika vya wakulima au wakawaunganisha wakulima wadogowadogo na wale wakubwa, wakawawezesha wapate nguvu ya kuzalisha pamoja kwa wingi na nguvu ya kwenda sokoni ku-negotiate bei; ninajua tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano BBT; vile vikundi vyote tuviboreshe, tuviweke kwenye ushirika na yale mazao ambayo bado hayajaingia kwenye ushirika. Tuwaweke pamoja, waweze kuuza mpunga pamoja, mahindi pamoja, maharage pamoja, kama ilivyo kwenye kahawa, korosho, tumbaku na kadhalika. Tukifanya hivyo tutakuwa tumewasaidia sana wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya kusema hilo ninaomba niseme, Mrajisi wa Ushirika na yule Mkaguzi wa Ushirika waongezewe pesa. Bado wana kazi kubwa ya kufanya kuisaidia Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa tatu ni, kuna pembe tatu maalum, ishara inayofahamika. Ninaomba waniangalie vizuri; hapa katikati iko Serikali, pale juu yuko mkulima, ambaye ndiye tunamhudumia, huku kuna utafiti, pembe ya chini huku kulia kuna utafiti, pembe ya kushoto kuna ugani. Sasa, hiki kitu Serikali ikiwaangalia watafiti vizuri, wakawekeza vizuri kwamba, watafiti wazalishe teknolojia, halafu watu wa ugani, kama alivyoongea Mheshimiwa Lusinde, wakawa chini yako uwe unawaangalia mwenyewe wapeleke teknolojia huku juu kwa wakulima, huo mzunguko tutafanikisha vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba tuendelee kuwekeza kwenye utafiti. Ugani umejitahidi, japokuwa hawako kwa Mheshimiwa Waziri, lakini amewapa hata pikipiki na vitu vingine, ili wafanye vizuri waweze kusaidia kupeleka teknolojia kutoka kwa watafiti kwenda kwa mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho ni, Msaada wa Kimataifa; tukipata pesa tupeleke kwenye umwagiliaji, Israeli walifanya hivyo. Ninatoa mfano wa Israeli kwa sababu, ni nchi ndogo na imefanikiwa sana. Waliwekeza kwenye maji, wakajenga bomba la urefu wa kilometa 250 kutoka Galilaya mpaka kwenda kule Kusini kwenye jangwa. Baada ya watu kupata maji kule, Israeli, ndiyo tunaona mafanikio yaliyopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, pamoja na kazi nzuri wanayofanya kui-support Tume ya Umwagiliaji, bado pesa ya ni ndogo, tuwaongezee pesa. Tuna mtendaji mzuri sana na Mwenyekiti wake wa Bodi, mzuri. Ni hakika tukifanya hivyo mambo yatatunyookea, mkulima umaskini utamwondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninawapongeza sana. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)