Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Kabla sijaanza kuchangia napenda ku-declare, mimi ni mkulima wa parachichi. Zao la parachichi; maji, mbolea na miche ya uhakika; bajeti ya mwaka jana walituambia watatoa ruzuku ya miche, nimeiona lakini siyo kihivyo. Wakulima wadogo wa parachichi wanahitaji maji ya uhakika, ili waweze kupanga msimu wao wenyewe wa mavuno. Tunahitaji pack house wakulima wa parachichi; ninazungumzia wa Njombe hapa na mimi ni mkulima mdogo tu wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaanza kuchangia. Nimewasikiliza Wabunge wengi wakichangia hapa. Ni kweli kabisa hawa vijana wawili, mimi ninawaita wazazi, wanafanya kazi nzuri na wametengeneza confidence kwa wakulima. Kama ambavyo humu ndani sasa hivi hatusikii kelele za kwenye madini kwa sababu, msingi wake Mheshimiwa Dkt. Biteko alitengeneza hiyo confidence, lakini mbali na mipango hii mizuri hapa waliyonayo, mbali na bajeti ya Kilimo kutoka shilingi bilioni 200 mpaka shilingi trilioni 1.2, pesa hazitoki zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, simwoni Waziri wa Fedha hapa! Kazi yetu sisi ni kuibana Wizara ya Fedha kupeleka pesa kwenye maeneo nyeti yanayogusa watu wengi. Leo bajeti ya mwaka huu 2025 tusingezungumzia tena shilingi trilioni 1.2, ingetoka yote tungewaza kuongeza iende ikasaidie Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipitisha, mwaka jana 2024, shilingi trilioni 1.2, imetoka shilingi bilioni 664, sawa na 33%. Kwa nini sasa miradi ya umwagiliaji utekelezaji wake isiwe 27% sijui 28%? Kwa nini miradi mingi ya kilimo isikwame kwa sababu, hakuna pesa za kutosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ambayo yanagusa watu wengi kwenye nchi hii. Kilimo, tunasema kinaajiri zaidi ya 70% ya Watanzania, huko tunatakiwa tuweke pesa za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia Wizara ya Afya, pesa zake zinatakiwa ziende vya kutosha. Unapozungumzia Wizara ya Maji pesa zinatakiwa ziende za kutosha. Kuna maeneo ya kimkakati yanamgusa Mtanzania mdogo, lazima tuweke pesa za kutosha. Haya, leo wao wana ndoto ya kumsaidia mkulima mdogo, hatuwapelekei pesa, hiyo ndoto itatekelezeka vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira njema kabisa na ni kweli, ndiyo Wizara ambayo inafanya nchi itulie, Wizara ambayo inalisha Taifa. Hatuipelekei pesa Wizara ambayo inaajiri, inatengeneza ajira, hatuipelekei pesa! Tunapeleka 53%! Serious? Si bora hata ingefika 70% au 80%? 53%, kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ninaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, lazima tuibane Wizara ya Fedha, ili haya malengo mazuri, ambayo yamewekwa na hii Wizara yatimie, ili hao akinamama ambao wanasomesha watoto kupitia kilimo wafanikiwe. Haya yote yanadhihirika, pale kwangu Bunda, waliahidi kutuchimbia visima 150, lakini wameweka kwenye mpango Kisima kimoja tu cha Misisi, Kata ya Sazira, vingine vimekwama. Siwalaumu, hawana hela, lakini lazima niwadai kwa sababu, wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini wamenituma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Bwawa la Bitaraguru linahitaji ukarabati. Wakilikarabati lile bwawa ambalo linahitaji shilingi milioni 150, kuna project ya Kilimo cha Bustani ekari zaidi ya 200, zinazofanya kazi ni ekari 50 tu, haya ni lazima tuyaseme. Dhamira ni njema, ndiyo maana wakatutengea hivi, lakini pesa haziendi, watafanyaje kazi? Lazima tuhakikishe Wizara ya Fedha inapeleka pesa kwenye maeneo nyeti ili Watanzania wawe na uhakika na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimezungumzia hapohapo visima 150, nimezungumzia Bwawa la Bitaraguru, lakini Wizara ilienda kufanya research kwenye Kata ya Wariku kwa sababu ya kuwekeza, lile eneo ni potential kwenye miradi ya umwagiliaji. Umepita mwaka mzima hakuna kinachoendelea. Kata zangu saba zile za vijiji watu wanajihusisha na kilimo na wao wametambua, tunaomba utekelezaji wake tuuone kwenye Jimbo la Bunda Mjini, ili wananchi waweze kutumia kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mabwawa mengi tu yanahitaji ukarabati; kuna Bwawa la Kisangwa, Bwawa la Gushigwamara na Bwawa la Kinyambwiga, haya yote yakikarabatiwa wananchi wa Bunda watanufaika na kilimo cha umwagiliaji. Mheshimiwa Bashe anajua, Bunda pale tuna ginnery tano, zinazofanya kazi ni ginnery mbili tu, nyingine zote zimekufa. Hizi zikifufuliwa zitasaidia ajira kwa vijana na akinamama wa Jimbo la Bunda Mjini, mwanzo zilikuwa zinafanya kazi. Tunaomba watufufulie ginnery hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa nilizonazo Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Mara kiliomba mkopo wa shilingi bilioni 3.7, kwa ajili ya kufufua Ginnery ya Ushashi, lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni, Mheshimiwa Bashe, tuna AMCOS tatu; ya Butakale, ya Kinyambwiga na vilevile ya Kinyambiga, hizi zote hazina maghala. Kikifika kipindi cha mavuno wanakodi, unaweza ukakuta mtu anakodi ghala kwa shilingi laki tatu/nne wakati amepata mavuno ya shilingi milioni ya pamba. Tunaomba AMCOS hizi zipate maghala, ili ziepukane na hasara ya kwenda kukodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia Mheshimiwa Butondo, zao la pamba limeporomoka, wakulima wa pamba hawaridhiki na hii bei elekezi. Kuna kipindi tulifika shilingi 3,000 leo ni 1,100. Wakulima wa pamba wanatumia gharama kubwa kwenye maandalizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia pamba; Mheshimiwa Bashe, ametoka Kanda ya Ziwa, anaelewa; na mzazi mwingine Silinde hapo hata kama hawalimi pamba, yeye yupo wizarani, tunaomba watusaidie zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna chuo pale cha wanyamakazi kipo Serengeti Kata ya Mcharo ni chakavu, kina ekari kama 25 hivi. Kile chuo wakikiboresha kitakuwa na uwezo wakutoa mafunzo kwa wataalam zaidi ya 20,000 kwa mwaka waweze kujifunza ni namna gani wataweza kutoa mafunzo kwa wakulima kulima kilimo cha kisasa. Chuo ni chakavu sana, sana. Wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini tunaomba sana wakarabati hiki chuo na sisi wakulima wa Jimbo la Bunda Mjini wapewe elimu ya kulima kilimo cha kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Maafisa Kilimo Wizara yangu; I mean idara yangu ya kilimo wana uhaba wa vitendea kazi. Ili waweze kutimiza majukumu yao mazuri tunaomba visima, miradi ya umwagiliaji; nimesema hapa kuhusu ukarabati wa Chuo cha Wanyamakazi, ukarabati wa mabwawa Bunda Mjini na maghala kwenye AMCOS. Ginnery zifanye kazi ili uchumi kupitia sekta ya kilimo kwa wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini uimarike, na sisi tuone kilimo kuwa ni sawa na kazi zingine. Kwa kweli wanafanya kazi kuna mzazi nyuma hapa ameninong’oneza, anasema anashukuru sasa hivi lile wazo lake la BBT linakwenda vizuri. Ninakushukuru. (Makofi/Kicheko)