Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa fursa ya kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. Nianze kwa kusema kwamba ninaunga mkono hoja; na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa ambayo ameyafanya katika sekta hii ya kilimo, mageuzi ambayo yanatambulika ndani na nje ya nchi. Halikadhalika ninampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Waziri Bashe, Mheshimiwa Naibu Waziri kaka Silinde, Katibu Mkuu na viongozi wote wa wizara hii kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuhakikisha kwamba tunaleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo ambayo ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kuipongeza sana Serikali chini ya Wizara ya Kilimo kwa kutambua mbegu za asili, ambayo imekuwa ni moja ya hoja zangu katika Bunge hili. Ninapongeza pia uamuzi wa kujenga seed bank kubwa, kwa maana ya gene bank hapa Tanzania, ambapo Tanzania itaungana na nchi kama za Norway ambazo zina gene bank kubwa duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi ninaomba niishauri Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunayo sheria ya mbegu ambayo kwa bahati mbaya inatoa haki ya wauzaji wa mbegu wakubwa; hivyo kuna haja kwa sheria hii kufanyiwa mapitio ili kuhakikisha kwamba sheria hii inatoa pia fursa na itambue umiliki na usimamizi wa mbegu za asili, kwa maana ya mbegu ambazo zinamilikiwa na wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika tunahitaji sera ya mbegu; sera hii ya mbegu ifanyiwe maboresho ili iweze kutambua namna ambavyo mbegu za asili zitasimamiwa na zitalindwa; na pia namna ambavyo hazitafifishwa kutokana na mikataba ya kimataifa iliyopo, ambayo inatoa upendeleo zaidi kwa mbegu za kisasa zinazozalishwa na wazalishaji wa nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ikamilishe mchakato wa NPGRFA ambao umeanza kutoka mwaka 2007, kwani kwa kufanya hivyo tutaweza kulinda haki za wakulima na pia tutaweza kulinda haki za mbegu za asili. Kwa kufanya hivyo Tanzania tutakuwa tunatekeleza mikataba ya kimataifa ambayo tumeridhia ambayo inalenga kulinda haki za wakulima ambayo ipo chini ya UNDROP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Serikali itajenga seed bank kubwa, kwa maana ya gene bank, nitumie fursa hii kuisisitiza sana Serikali chini ya Wizara ya Kilimo, kwamba ni lazima itenge fedha ili iwekeze na tuhakikishe kuwa tunakuwa na seed bank katika ngazi ya vijiji, kwa sababu ni muhimu sana kulinda mbegu za asili ngazi za vijiji. Tayari tumeshaona mifano mizuri kupitia wadau wa SWISS AID wako na seed bank ambazo wameanzisha pale Lindi, wadau wa Iles de Paix (IDP) ambao wameanzisha seed bank pale Arusha pamoja na Mkoa wa Manyara. Hivyo, nitumie fursa hii kusisitiza sana Wizara ya Kilimo, pamoja na kwamba tutajenga seed bank kubwa ya kitaifa ni lazima tuwekeze pia katika kujenga hizi benki za mbegu za asili kwa kuanzia walau kila mkoa uwe una mbegu za asili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kusema, kwamba mbegu hizi za asili zina uwezo mkubwa sana wa kuhimili ukame, zina uwezo mkubwa sana wa kuhimili magojwa. Hivyo tutakavyozidi kuhakikisha tunatumia na tunalinda mbegu zetu za asili tutaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; jambo ambalo litaendelea kuwaweka wakulima wetu salama, lakini pia litapunguza utegemezi wetu kwenye mbegu za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu suala la mbegu ni suala pia la kidiplomasia, suala la mbegu pia linaweza likatumika katika kuleta athari ya usalama wa kitaifa. Kwa hiyo ni muhimu sana niendelee kusisitiza tuzilinde mbegu zetu za asili na tuhakikishe kwamba wakulima wetu wanalindwa na kunakuwa kuna nguvu ya ziada katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na hizi benki za mbegu za asili katika mikoa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo mbegu hizi za asili zina mchango mkubwa sana katika kuchangia kupunguza matatizo ya lishe, kwa sababu tafiti zimeshathibitisha kuwa mbegu za asili zina madini joto mengi, zina madini chuma mengi, zina protini nyingi pamoja na vitamini mbalimbali tofauti na mbegu za aina nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaendelea kuishukuru sana Serikali kwa kutambua na kuweka ulinzi juu ya mbegu za asili. Hata hivyo, niendelee kusisitiza, kwamba ni lazima sheria zifanyiwe maboresho kama ambavyo nimeshaeleza, lakini pia lazima tuwe tuna benki za mbegu za asili kwenye mikoa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijahitimisha nigusie hoja yangu nyingine ya kudumu katika Bunge hili kuhusiana na zao la vanila. Ninatambua kuwa Serikali chini ya Wizara ya Kilimo imefanya jitihada kubwa sana katika soko hili la vanila; lakini nikiwa ninatokea Mkoa wa Kagera bado wakulima wetu wa zao la vanila Mkoa wa Kagera bado wanahitaji Serikali iangalie zao hilo kwa jicho la kipekee kutokana na fursa ya rasilimali fedha inayoweza kuleta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii kuiomba sana Wizara ya Kilimo kupitia mamlaka yetu ya COPRA isimamie vizuri zao hili la vanila ili tuweze kupata soko. Wakulima wetu kilio kikubwa ni soko. Ninatambua kuwa chini ya dada yangu Irene zipo jitihada kubwa ambazo zinafanyika za kuhakikisha kwamba tunapata soko la vanila nchini Japan pamoja na China.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mitano hii nimekuwa nikiongelea zao la vanila; bado hatujafikia kuliona hilo soko. Niombe sana tuweke kipaumbele katika zao hili la vanila ili wakulima wa zao hilo Mkoa wa Kagera waweze kunufaika na zao hili ambalo litakuwa na mchango mkubwa sana katika kuchangia fedha ambazo zitatokana na mchango wa sekta hii ya kilimo.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa inatokea wapi? Mheshimiwa Saashisha Mafuwe.

TAARIFA

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninataka kumpa taarifa Mheshimiwa ambaye anachangia vizuri kuhusu zao la vanila. Zao hili kuna kipindi lilifika kilo moja 120,000; lakini kutokana na kwamba mazao ya vanila mengi yanaingizwa kutoka nje ya nchi bei hapa kwetu imeshuka. Kwa hiyo nilikuwa ninampa taarifa tu kwamba, mchango wake ni mzuri, asisitize kwamba tuzuie mazao ya vanila yanayoingizwa nchini ili vanila yetu ipande bei.

MWENYEKITI: Unaipokea taarifa hiyo Mheshimiwa Neema?

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Saashisha. Ninaendelea kusisitiza Serikali iweke jitihada kubwa kwenye zao la vanila kwa sababu hili ni zao la kimkakati. Ninatambua namna ambavyo kaka yangu Mheshimiwa Waziri Bashe anaendesha shughuli zake, ni mzee wa vitendo ni kaka wa vitendo. Hivyo basi hata na sisi katika zao la vanila tuone vitendo hivyo kupitia matokeo chanya kwa kaka yangu Bashe ili tupate soko la uhakika la vanila. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe pia kwa kusisitiza, tunapoongelea maendeleo ya sekta ya kilimo hatuwezi kuacha watafiti wetu, wanasayansi wetu katika kukuza sekta hii ya kilimo. Watafiti wana nafasi kubwa sana, hivyo niombe sana... (Makofi)

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa. Hapa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Olelekaita.

TAARIFA

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimpe dada yangu, taarifa hapa. Anavyozungumza habari ya watafiti, Profesa Patrick Ndakidemi, kwenye journal ya watafiti wanaoheshimika duniani ni namba mbili Tanzania; lakini inapokuja kwenye wataalam wa kilimo nchi hii ni namba moja ana point 56 na anayemfuata ana 41. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea sana taarifa hiyo na ninaomba nichukue fursa hii kumpongeza sana mzee wangu, baba yangu Mheshimiwa Profesa Ndakidemi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pale ambapo nilipokuwa nimeishia; pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanyika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ni lazima iwekeze fedha za kutosha katika tafiti ili wanasayansi wetu waendelee kufanya kazi iliyobora, ambayo pia itajumuisha kutafiti hizi mbegu za kisasa ambazo tunaletewa, kwamba zinakuwa zina madhara au zinakuwa zinatija pamoja na kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nirejee tena kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya, nirejee tena kumpongeza kaka Bashe kwa kazi kubwa anayofanya na nisisitize umuhimu wa kuwa na benki za mbegu za asili katika mikoa yetu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)