Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Nami nichukue nafasi hii kupongeza sana Wizara ya Kilimo, watoto wa mjini wamesema kwa kweli sasa hivi Kilimo kumechangamka. Kumechangamka kwa sababu Waziri mnafanya kazi vizuri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu rafiki yangu anafanya kazi vizuri na Wakurugenzi wote, yaani kunaonekana kila Mkurugenzi anafanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana sana kwenye hili eneo la mbolea, Mheshimiwa Bashe anakumbuka ilikuwa shida, nikawa ninakwambia kabisa kwamba Kijiji cha Mdundualo wakanunue mbolea Songea Mjini; walikuwa wanapigwa na kuna wanawake wengine hadi waliugua; lakini leo hii tunavyozungumza vijiji vinapata mbolea. Kwa mfano Kijiji cha Mdundualo yaani wakala yupo pale kijijini, kwa hiyo hakuna tena kusafiri, hiyo ni pongezi kubwa sana. Kama kuna kijiji cha Mheshimiwa Kunti kule basi ni vichache; wawasaidie na wao wapate mbolea kama wanavyopata vijiji vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia ile juhudi ya kupeleka pikipiki kwa wale Maafisa Ugani. Hata hivyo nimwambie Mheshimiwa Bashe, kwamba zile pikipiki haziwafikii wakulima. Ukipiga simu au mkulima anamhitaji yule afisa, anakuuliza una mafuta? Utaniwekea hela? Sasa ninafikiri wajipange kwa utaratibu. Gari anazotaka kupeleka na hizo pikipiki waziratibu vizuri na ikiwezekana sijui kuwe na wakala, otherwise watapeleka gari lakini haziwafikii wakulima. Vijana wanapiga race mitaani na zile pikipiki. Hilo ninamwambia Mheshimiwa Bashe. Yeye ni rafiki yangu, lakini lazima nimwambie ukweli. Suala la pikipiki lile ninakwambia limebuma, waangalie vizuri, waweke mwongozo kwenye pikipiki, zinafanya kazi namna gani. Walisema watakuwa wanawafuatilia, hakuna kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema kwa sababu mimi nikiwaita pia wananiambia. Sisemi kama mimi ni Mbunge, ninasema tu kama mkulima ninahitaji, lakini wanakwambia tuwekee fedha ili tuweke mafuta. Kwa hiyo, ninataka kusema mkulima wa chini kupata huduma na wale maafisa ni shida kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo alituahidi, nimwambie Mheshimiwa Bashe, sijui walitoa mwongozo, maana nilitafuta trekta kulima kule sikupata. Safari hii ninaomba atupangie vizuri mwongozo; tunakwenda wapi sisi wakulima wa chini ili tupate matrekta, tulime kwa hiyo bei. Nimesikia mwenzangu mmoja anasema hapa ni shilingi 35,000, lakini ninakumbuka walituambia 40,000. Sasa which is which, ninaomba watueleze vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena kusema, kwamba huyu jamaa anayeshughulika na mbolea anastahili maua yake. Nimwombe sasa, Mheshimiwa Bashe ni rafiki yangu, nilimweleza kuwa kuna bonde kule block farm kubwa sana. Kwa nini hataki kwenda kutuchimbia kule mabwawa. Block farm, lakini si ni mkoa wake ule. Ninaomba, nina ramani hapa nitamrushia Mheshimiwa Bashe, atupelekee bwawa kule ili tulime Mpunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka kuwa pia walituahidi watatupelekea skimu hizo nane Nyasa; hazipo mpaka leo, hakuna mpaka leo; lakini watu wanafikiria Ruvuma hatuhitaji mabwawa kwa sababu kuna mvua na tulikuwa tunalima sana. Sasa hivi kutokana na hizi tabianchi kubadilika tunahitaji na sisi mabwawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anipelekee bwawa Mdundualo kule. Aliniletea wataalam, ninamshukuru sana; waende Mdundualo ili lile bwawa sasa likafufuke. Sehemu inaitwa Likingu waende kule na sisi tuone mabwawa maana watu wanayasikia tu. Sisi tunayahitaji hayo mabwawa ili tuanze kulima kwa kutumia Irrigation scheme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndiyo nianze kuchangia. Nimshukuru sana Mheshimiwa Bashe, anapambana na bei za kahawa pamoja na korosho. Sasa ile bei waliyotuambia ya 4,000 kilo yaani ile ilikuwa mara moja na ndio ikazima. Asimamia palepale hawa wanunuzi wasishushe bei, korosho haiozi. Ile ya shilingi 4,000 tulifurahi sana, lakini ikashuka, ikashuka, hadi ikafika huko kwenye elfu mbili na ushee. Asimamie hizi bei zipande pale; tena awatishie kwamba, kama mnasema zipunguzwe siwauzii korosho, lakini korosho watazinunua tu. Kwa hiyo tunaomba ile bei ibaki shilingi 4,000 kwa kilo; ilifanyika mara moja tu, hiyo nimwambie na Mheshimiwa Bashe analijua hilo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, sasa nakuja kwenye utafiti. Niseme hivi, nipongeze sana kazi inayofanywa na TARI na hasa pale Naliendele. Kwenye hii fedha nyingi aliyoipata kwenye bajeti ya safari hii aipeleke bajeti nyingi kwenye utafiti. Wakafanye utafiti kwenye mbegu ili tusipate mbegu fake. Zile kampuni zinazouza mbegu fake zifungiwe; na kampuni zinazouza mbegu nzuri tutangaziwe ili wakulima wajue kuwa kampuni hii ina mbegu nzuri ya mahindi; zitangazwe zile mbegu nzuri zote na kampuni zao; lakini na wale matapeli watangazwe pia ili mkulima ajue kuwa, nikiona kampuni hii nisinunue mbegu yake. Asiwaonee huruma; mimi ninakwambia wakulima watafurahia sana. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Dkt. Jeradina aliyeko kule Naliendele. Kuna mbegu kule ya karanga, nikasema hivi mbegu hii ya karanga ambayo na mimi nilipanda, je, kule Tabora Kaliua wanaijua? Nachingwea wanaijua? Ruvuma yote wanaijua? Kuna mbegu nzuri mno. Mimi mwenyewe nilishangaa, nimelima kaeneo kadogo tu. Kwa hiyo ile mbegu ninaomba Mheshimiwa Bashe awasambazie mikoa yote wanaolima karanga, watafurahi sana, ipelekwe kule. Vilevile kuna SUA, Nelson Mandela, UD na Tumbi; hizi ni Centre zinazofanya tafiti, hawa wameomba wasaidiwe. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliongea na mkuu wa chuo fulani akasema: “Tunaomba watushirikishe sana katika tafiti.” Leo hii kuna huu utafiti wa tissue culture ya ndizi; hebu wasaidiwe hii tissue culture ya ndizi pale Nelson Mandela ili iweze kuwasaidia. Kwanza wao Nelson watapata fedha na vilevile watasaidia ku-train na nchi nyingine na hivyo watapata fedha. (Makofi)  
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tissue culture ya ndizi ni biashara nzuri mno. Mheshimiwa Bashe aweke nguvu zake hapa, awasaidie SUA, awasaidie na wale Nelson Mandela na UD pamoja na Tumbi kwa kuwa wanafanya kazi nzuri. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa RAS Tabora, Tumbi kuna zinaitwa pingiri, aliniambia huyu Maige, sijui ni Kiswahili; zinaitwa pingiri, zile za mihogo. Tumbi wana mbegu nzuri za mihogo. Tunaomba; walianza production kidogo, lakini tunaomba, wataalam wanisikilize hapo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba zile mbegu Mheshimiwa Waziri azisambaze kwenye mikoa inayolima mihogo ili kuzuia ile bleach, sijui inaitwa bleach sijui inaitwa nini. Wanatoa mbegu ambayo ipo very resistant to disease. Tusaidieni Ruvuma tunalima mihogo, Tabora wanalima mihogo, hata Kyela kule wanalima mihogo. Kwa hiyo, ile species muisambaze. Mimi kuagiza mbegu kutoka kule kupeleka huko kusini ninaweza; lakini mkulima wa kawaida, ninaomba wasambaze hiyo mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninataka nimwambie Mheshimiwa Bashe, yeye ni rafiki yangu, lakini hili lazima nimwambie, Mheshimiwa Bashe nimemwambia mara nyingi zao la tumbaku linawafaa wakulima wakubwa. Wakulima wadogo kwanza wanachelewa kuwalipa, wakulima wadogo wanakopa sana wengine mpaka wanakimbia nyumba zao. Ninafurahi ananiangalia, anisikilize. Ameniambia kwamba wameweza kupata tani 160,000 sawa, wanapata sijui fedha za nje zinawasaidiaje wakulima wa chini Mheshimiwa Bashe? Nyumba zao mbovu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie hivi, wakishapata zile hela waende wakatengeneze programu ya kuwasaidia wakulima wadogo. Wakulima wadogo afya zao mgogoro, hali zao na nyumba zao mgogoro unazing’ang’ania, amwachie Mheshimiwa Cherehani alime tumbaku, lakini wakulima wadogo wawape mazao mengine mbona yapo Mheshimiwa Bashe, hili zao wanaling’ang’ania kwa nini? Mimi hapo kwa kweli wewe hautakuwa rafiki yangu, urafiki utapungua kwenye hilo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo basi mimi nikushukuru sana, lakini nimemwambia ukweli. Ninafikiri atakuja na majibu ya kuliondoa taratibu hilo zao la tumbaku. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninawashukuru sana. (Makofi)