Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kabla sijaendelea na mchango wangu ninaomba ni-quote maneno ya Baba wa Taifa, Baba wa Taifa anasema maeneo yafuatayo kwenye kilimo: “Hatupaswi kusahau kwamba kilimo ni kazi ya heshima tunapaswa kuwathamini wakulima na kuwaunga mkono ili waweze kufanya kazi yao vizuri.” Maneno ya Baba wa Taifa, Mwasisi wa Taifa hili ambaye aliamini na kuheshimu kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya ya Baba wa Taifa, ninaomba nitumie fursa hii adhimu kuipongeza na kuishukuru sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia ambaye ni Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi amekitendea haki chama chetu, amewatendea haki Watanzania kwa kuonesha na kuyaishi maneno halisi ya Baba wa Taifa kwamba kilimo siyo kazi ya kudharaulika, kilimo ni kazi ya kuheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ninaomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kuendelea kuwahudumia wakulima wote nchini kwetu na kwa kweli tumeona faraja kwa wakulima. Kipekee ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Bashe katika kipindi cha Uwaziri wake amebahatika kufanya ziara kwenye Jimbo langu la Momba, ninamshukuru sana. Kwa hiyo, katika haya nitakayokuwa ninashauri ninajua atakuwa na picha halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, nitakuwa na ushauri kidogo tu kwenye Wizara yetu hii pendwa ili waendelee kuwahudumia wakulima. Mheshimiwa Waziri, katika vipaumbele vyake alivyokuwa amevisoma pamoja na ile mikakati ombi langu la kwanza, nimwombe kama ambavyo ameanzisha BBT ninaomba aanzishe kampeni ya kutokomeza Watanzania kulima kwa kutumia jembe la mkono ili tuanze kulima kidigiti. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, aah! Kaka mimi nitaomba taarifa usome baadaye, nishauri kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani kuona hizo takwimu alizokuwa anazisoma za miaka minne, kwamba miaka minne tumetoka hapa, tumepanda hapa, tumezalisha tani hizi Mheshimiwa Waziri pamoja na jitihada zote hizo ambazo alizisoma hapo mbele zaidi ya Watanzania, 60% bado wanalima kwa kutumia jembe la mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania watakapoanza kulima kisasa watatumia akili kubwa, nguvu kidogo lakini watatumia eneo dogo na watazalisha kwa kiwango kikubwa. Kwa hiyo, ninatarajia tutakaporudi kwenye Bunge la Kumi na Tatu anasoma bajeti kama sasa kama Mungu ataendelea kumpa kwenye hiyo nafasi au vinginevyo atapandishwa. Tunatamani atusomee takwimu kwamba alikuwa na Watanzania kadhaa ambao walikuwa wanatumia jembe la mkono na sasa hivi siyo tu kuwa wa pili kulima mahindi Afrika, tunatamani kuwa wa kwanza. Hiyo ni kampeni ambayo ninaomba Waziri aweke kwenye vile vipaumbele vyako Watanzania tutoke kulima kwenye jembe la mkono as we are speaking now hatuna hata matreka, hayawezi kufika 100 kwenye Jimbo la Momba, sijajua kwenye Majimbo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri, mbegu, sitataka kuongea sana kwenye hiki kipengele kwenye suala la mbegu, lakini pamoja na jitihada zote ambazo wamefanya, ninataka nimwachie tu homework. Kwa nini, watu wa Nyanda za Juu Kusini bado wanalima na kutumia mbegu ya mahindi kutoka Zambia, kwa nini? Hususan kwenye Mkoa wangu wa Songwe, mbegu zote za mahindi tunachukua Zambia, Zambia wametuzidi kitu gani? Pamoja na mazuri yote ambayo umefanya kwenye mbolea hiyo ni homework. Tunapaswa kuzalisha mbegu zetu wenyewe, sisi ndiyo tuwauzie Zambia na Mataifa mengine na yenyewe hiyo itakuwa ni chanzo kizuri cha mapato kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbolea, Mheshimiwa Waziri ninakiri na hata alipotembelea Jimboni kwangu Momba aliona. Kwa kweli hali ya upatikanaji wa mbolea ilikuwa ni changamoto sana na Watanzania wengine ambao wameongeza kipato kwa kutupatia ruzuku za mbolea, lakini Mheshimiwa Waziri kaka yangu kule Wilayani kwetu, sisi tunatoka Wilaya ambayo ipo mpakani, tunakiri vyombo vya dola vimefanya kazi yake vizuri sana ila bado wapo ndani kwako huko kuna shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifumo ya mbolea iwekwe vizuri mbolea bado inatoroshwa kwenda Zambia. Mimi ninatoka Jimbo ambalo pia lipo mpakani pale Tunduma bado kuna shida. Kwa hiyo, ile ruzuku ambayo wametuwekea ili inawezekana sasa hivi mbolea isingekuwa nyingine imevuja huko inawezekana mpaka tunavyoongea. Sasa tungekuwa sisi tumeongoza, tumekuwa wa kwanza katika zao la mahindi, lakini bado ipo mianya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kwamba wapo baadhi Watanzania ambao wanalima upande wa Zambia. Kwa hiyo, wanachukua mbolea yetu wanaenda kulimia upande wa Zambia lakini mbona inapokuja mbegu mbona wenyewe Watanzania wanaenda kununua Zambia kwa pesa kwa nini na wenyewe wasifuate? Kama upo utaratibu wa kuwauzia mbolea kama nchi ili iende ikatumike kwao, lakini siyo mbolea yetu ya ruzuku ambayo Mheshimiwa Rais ameamua kutoa thamani ndiyo iende ikafanye Zambia. Bado kuna matobo, hukohuko ndani kwako, mwone namna ya kuangalia hili jambo lisiendelee tena, lakini nia ya Serikali na nia yako ilikuwa ni njema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mikakati yake Mheshimiwa Waziri, vitu ambavyo vingine amevitaja kwamba ni kipaumbele ni pamoja na masoko kwa wananchi kuwatafutia masoko. Mheshimiwa Waziri mwaka jana tulikuwa tunaogopa hata kuonana usoni nikija unasema Condester, ninajua kule kwake changamoto ya stakabadhi ghala. Mimi kama Mbunge kijana nikaamua nichukue hili jukumu nikaenda na yule DG wa Waziri anaitwa Bangu, tukazunguka Jimbo zima la Momba kuwaelimisha wananchi umuhimu wa stakabadhi ghalani na kwa kauli yake amekuwa akisema stakabadhi ghalani mkulima anajipangia bei. Sasa Mheshimiwa Waziri Wanamomba wakaitika wakakubali na nikawaambia limeni poleni kwa changamoto ambazo zimewapata tukae kwenye muda wa kujifunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wanamomba wamelima sana ufuta na kwa bahati mbaya kwa sababu mvua zilikuwa ni kidogo mazao ambayo yanakubali mvua kama mpunga hatujapata, wakapata ufuta. Sasa Mheshimiwa Waziri ikiwa bei ya mwisho mwaka jana ilikuwa 4,000 tunapoongea sasa juzi kulikuwa kuna mnada 2,800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitaomba Waziri atakapokuja kuhitimisha leo jioni atuambie ile hamasa aliyotupa tukubali stakabadhi ghalani, nikaamua kubeba mzigo mwingine wa Waziri mwenye dhamana, ilibidi aje kutoa tamko Wanamomba wakaelewa, sasa hivi Wanamomba wanalia. Wanataka wauze huo ufuta ili waweze kununua mahindi, ili waweze kununua mpunga bei zipo chini unatuambiaje? Wanamomba hawajui mambo ya demand and supply huko duniani, yeye ndiye Waziri mwenye dhamana anatusaidiaje bei za ufuta zipo chini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu skimu za uwagiliaji, ninakushukuru nimepitia taarifa yako yote kwenye mabondeni yote hapa ya kwetu. Bondeni la Kasinde amesema upembuzi umeshakamilika lina hekta 15,000 kwamba upo kwenye manunuzi, kwenye Bwawa la Kamsamba ambalo lina huo ujazo wa cubic meter 62,920, Bwawa la Kasinde pia cubic meter 88 umesema vyote hivi vimekamilika. Kwa dhati ya moyo wangu pamoja na Wanamomba tunakushukuru sana ukamilishaji huu unasema tupo kwenye manunuzi. Tunaomba kweli tuone kwenye vitendo, tunaomba kweli tuone kwenye vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazalisha; pamoja wanalima kwa kutumia jembe la mkono utakapotuletea mambo mazuri kama haya siyo tu kwetu sisi Wanamomba, lakini ni faida pia kwa Taifa. Nimwambie ukweli mpunga ambao anaona unaenda mwingi pale DRC na Zambia, mimi si nipo hapo maeneo Jirani, unalimwa na hawa wanaolima kwa jembe la mkono hapo Momba. Kwa hiyo, tunaomba hili jambo likamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaona Skimu ya Uwagiliaji Naming’ongo, Mheshimiwa Waziri alikuja pale tukamtembeza akapigwa na picha vizuri na Wanamomba akili yao bado inakukumbuka. Sasa hivi utekelezaji ametupa pesa 41%. Tunamwomba basi kaka atumalizie hii pesa maana yake ndiyo skimu ambayo kwa sasa hivi inategemewa hakuna skimu yoyote ya uwagiliaji kwenye Jimbo la Momba. Hii tu hizi nyingine zote ndiyo tunakusudia tuweze kuzifanya, umeona ni hii tu 41%. Kwa hiyo, sasa hivi ukiona mpunga ambao utakuwa umetoka Momba ni kwenye hii skimu hii hapa. Kwa hiyo, tunaomba tumaliziwe pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa umuhimu wake, Waziri mwenyewe akiendelea kusema anayaunga mkono maneno ya Mheshimiwa Rais kwamba sisi tunataka tujitosheleze ndani, lakini pia tuweze kuilisha Afrika. Mheshimiwa Waziri siyo makosa ya Mheshimiwa Rais, siyo makosa ya Chama Cha Mapinduzi, siyo makosa ya Waziri, kulikuwa kuna mabadiliko ya tabianchi Tanzania kwingi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya maeneo ambayo yanategemea mazao yenye mvua wamekosa mazao. Mfano kule kwetu Momba hatujapata mpunga kwa sababu hata hii skimu yenyewe si haukutuletea pesa, sasa tungemwagiliaje? Maana yake skimu ni mbovu. Kwa hiyo, tulikuwa tunategemea mvua ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, yale mazao kama mpunga hatujapata. Ninataka kumwambia nini? Ninataka kukumbusha kule 2022 maana yake hatuna mazao ya kutosha ya chakula. Sasa kama jana Waziri ametusomea kwenye hizo taarifa zake kwamba sisi tumekuwa ni wazalishaji wa pili wa mahindi na Mheshimiwa Rais anasema tujitosheleze sisi nchini kwetu na tuweze kuwahudumia Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi tunaomba kuanzia angalau mwezi Julai watu wamalizie kuvuna, atakuwa ameshafanya tathmini, ameshapata. Tunaomba NFRA kwa atakavyojua kwa sababu wapo chini yake, waanze kuwauzia wananchi mahindi kwa sababu lengo la kupeleka ruzuku, lengo la kufanya mambo yote hayo, lengo la Wabunge sisi kuendelea kuishauri Serikali kwamba tuongeze bajeti ni kuona kwamba hatupaswi kununua chakula kwa bei ghali kwa sababu tumelima tuweze kujitosheleza sisi wenyewe na sisi tunalo ghala la NFRA. Kwa hiyo, tusingependa mahindi yanatoka, yanaeenda Zambia na DRC wakati sisi wenyewe tunalolitunza ghala na tumewa-host vizuri na kuna wakati NFRA wanachelewa kutulipa. Kwa hiyo, wakiwa wanachelewa kutulipa tunatunza mahindi yetu. Tunaomba tuanze kupata mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kuendelea kutukumbuka wakulima na sisi tunaamini watawatendea haki wakulima. Ahsante sana. (Makofi)