Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata nafasi niweze kuchangia kwenye bajeti hii muhimu sana ambayo inawagusa Watanzania wengi, ambapo Watanzania wengi sana wanajihusisha na kilimo hasa kilimo kile kidogokidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yote ya Wizara kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya kuhakikisha kwamba kilimo cha nchi yetu kinaendelea kuwa mkombozi kwa Watanzania wetu, lakini kilimo hiki kinaendelea kuwakomboa kiuchumi sisi watu ambao tunatoka maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kupongeza kwa bajeti ambayo imeendelea kukua mwaka hadi mwaka. Tunafahamu kwamba tumetoka toka kwenye shilingi bilioni 294 mpaka shilingi trilioni 1.2 mwaka jana na mwaka huu imeendelea hivyo. Hii yote ni juhudi kubwa ambayo inafanywa na Wizara. Pia, tumpongeze mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa mkulima namba moja champion kuhakikisha kwamba anawajali wakulima, anakijali kilimo na kuhakikisha kwamba Watanzania waendelee kunufaika na kilimo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoenda kupongeza kwa kuongezeka kwa bajeti pia tu ninaendelea kupongeza kwa mipango mizuri waliyokuwa nayo. Namna ambavyo sisi ambao tunatoka maeneo ya kilimo hasa ambacho tunatoka kwenye kilimo cha tumbaku mipango yao mizuri kwenye Wizara, mipango yao mizuri kuhakikisha kwamba kilimo hiki kinazidi kukua, tumeweza kuona namna ambavyo zao letu la tumbaku limeweza kukua kutoka 2021/2022. Sisi Mkoa wa kitumbaku wa Chunya tulikuwa tunazalisha tani 15,000,000, lakini mwaka huu tunategemea kuzalisha tani 25,000,000 Mkoa wa Kitumbaku wa Chunya. Haya ni mafanikio makubwa sana tunawapongeza kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaambie nitapingana kidogo na mama yangu Mheshimiwa Dkt. Thea, kwamba uchumi wa wakulima wa tumbaku umeweza kukua na umeongezeka kwa kiasi kikubwa sana. Sisi leo wastani wa juu wa zao la tumbaku ni dola 3.4 hii haijawahi kutokea kwa kipindi kirefu sana toka mama Mheshimiwa Dkt. Samia ameweza kuingia. Haya kwetu ni mafanikio makubwa sana. Hivyo, pato la Halmashauri yangu ya Wilaya ya Chunya kupitia zao la tumbaku mwaka uliopita tulipata shilingi bilioni 3.8 ambayo imetokana na ruzuku kutoka zao la tumbaku. Kwa hiyo, sisi kwetu zao hili ni mkombozi kwa wakulima, lakini pia mkombozi kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri haya ambayo yamefanyika kwenye zao la tumbaku lakini bado tunaendelea kuishauri Serikali iweze kuona namna bora na nzuri ya kuhakikisha kwamba zao hili kadri linavyoendelea kukua tuendelee kutunza mazingira. Mazingira yetu mengi tunayolima maeneo ya tumbaku yanaharibiwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wakulima wanakatwa fedha kwa ajili ya kupanda miti, lakini hiyo miti haionekani. kwa hivyo tulishauri Serikali ione namna iliyokuwa nzuri ya kuhakikisha kwamba wakulima wa kwetu wanawekewa utaratibu mzuri ili hii miti isiweze kuharibiwa kwa kiasi kikubwa kama ambavyo inaendelea kutokea sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wakulima wetu hawa kwenye zao la tumbaku pamoja na kutumia nguvu kubwa sana kulima, lakini changamoto ya majanga ya asili yameendelea kuwaletea hasara sana. Changamoto ya ukame kama mwaka huu ambavyo tumeona, mvua zimekuwa kidogo hivyo wakulima mazao yao yamekuwa machache. Pia kuna wakati mvua zinakuwa nyingi hasa mvua za mawe, majani yale yanaharibika na yakiharibika inakuwa ni hasara kwa mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri kwamba tuone namna ya kusisitiza ile bima ya wakulima tuhakikishe tunaipa nguvu ili wakulima hawa wasiweze kupata hasara kama ambavyo wanapata sasa hivi. Wanafanya kazi kubwa shambani lakini majanga ya asili ikiwemo mvua za mawe pamoja na ukame au mvua inapokuwa imezidi imeendelea kuwarudisha nyuma wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ili tuendelee kutoa elimu kwa wakulima wetu juu ya mabani yaliyokuwa mazuri na kisasa, wakulima wanafanya kazi kubwa sana shambani lakini kazi kubwa ile inakuja kuathiriwa wakati wa ukaushaji wa hii tumbaku kupitia kwenye mabani. Mabani mengi yanayojengwa yanakuwa hayana ubora wa kisasa, siyo makubwa kulingana na uhitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kazi kubwa iliyofanywa na wanakulima inaelekea kupotea katika hatua ya ukaushaji wa tumbaku. Wakulima wanashindwa kupata kile walichotarajia, kwani mavuno yao hayazai matokeo kama walivyotarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne tuendelee kutoa elimu juu ya kalenda ya upandaji wa zao la tumbaku. Tukifuata kalenda vizuri, wataalam wetu wakiwasisitiza hawa wakulima tutaweza kupata mazao mazuri na wakulima wetu wataona tija ya zao la tumbaku na bei ambayo ipo sasa hivi itaweza kuwanufaisha vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tunafahamu kwamba Watanzania wengi wanategemea sana kilimo kuendesha maisha yao hasa kule vijijini na kilimo ambacho sasa hivi tunatakiwa twende nacho na kila mmoja akizungumze hapa ni kilimo biashara. Kilimo biashara ndiyo mkombozi wa mkulima wetu wa Tanzania na soko letu la mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali iwekeze sana kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tunajua inafanya kazi kubwa, inaendelea kuchimba mabwawa, inaagiza magari ya kuchimba visima lakini hii kasi iweze kuongezeka. Tukiongeza hii kasi tunaamini kwamba wakulima wetu wataenda kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Wilaya ya Chunya hasa Tarafa ile ya Kipembawe yamegundulika mabonde mazuri yanayofaa kwa kujenga scheme za umwagiliaji. Kata ya Kambi Katoto, Kata ya Mafyeko, Kata ya Luwalaje pamoja na Kata ya Rupa maeneo Riyesero. Haya yamegundulika kwamba yanafaa kupitia wataalam wetu wa ndani na wataalam kutoka Wizarani kupitia Tume ya Umwagiliaji. Waliweza kufika Wilaya yetu ya Chunya wakayaahirisha wakayaona na sisi tukaweza kuomba, tumeandika barua kuomba angalau tuweze kupata usanifu wa kina, takribani kama milioni zisizopungua 500 hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha tukiweza kuzipata, ukafanyika usanifu wa kina angalau sasa tutaweza tukaanza kuyajenga maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji na sisi Wilaya ya Chunya tukapata skimu za umwagiliaji, hivyo kilimo chetu kitaweza kwenda mbele na wananchi wetu wa Tarafa ya Kipembawe wakanufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei yake, kuna scheme ya umwagiliaji ambayo ilianza kujengwa muda mrefu sana toka 2012 ambayo inaitwa scheme ya Ifumbo. Tulipata zaidi ya bilioni moja, lakini ilijengwa ndani ya mwaka mmoja ikasimama, zile fedha ni kama zimepotea. Hivyo, kwa kuwa Serikali nia na lengo lake ni kuhakikisha kwamba eneo lile ambalo linafaa kwa kilimo cha umwagiliaji liendelee ili lengo lake liweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara, tunafahamu ilikuja lakini iweze kufanya usanifu upya kulingana na mazingira ya sasa hivi, tupate fedha, usanifu wa kina ufanyike, scheme ile pale iweze kujengwa ili wananchi wa Kata ya Ifumbo na Wilaya ya Chunya tuweze kunufaika wakati hii tayari tunakuwa tumeshaanza nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya ambayo tumeweza kuyasema, mtakumbuka wizara ina mpango mzuri sana wa kesho iliyo bora maarufu kama BBT. Sisi Wilaya yetu ya Chunya tuna maeneo takribani hekta zisizopungua 600,000 ambayo Waziri alifika, tukayaainisha. Hata hivyo, tulitegemea kwamba angalau sasa hatua za mwanzo zile zilivyokuwa zisingeweza kuanza, pia mpaka sasa mradi huu bado haujaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, wananchi wangu wa Tarafa ya Kipembawe wanategemea yale mashamba pori wakiweza kuyaendeleza tutahakikisha kwamba uchumi wa wananchi wa Chunya kwa maana ya Tarafa ya Kipembawe utakua, ajira zitazalishwa, lakini kama nchi tutakuwa na uhakika wa chakula cha kutosha. Mlibebe hili ili pamoja na mradi unapokuwa unaendelea tuhakikishe kwamba na sisi Wilaya ya Chunya tunapewa kipaumbele pamoja na kwamba zao la tumbaku linaendelea, lakini na haya mazao mengine yaweze kwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi hii. Niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya yeye na wataalam wake, tunaamini kilimo siyo uti wa mgongo, kilimo ni biashara na kilimo ni fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)