Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami ili niweze kuchangia bajeti hii ya wakulima, bajeti hii ya wananchi. Nianze kwa kuunga mkono hoja bajeti hii nzuri ambayo inakwenda kugusa maisha ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuja Kigoma alisema anakwenda kuufungua Mkoa wa Kigoma, amekwenda kuufungua Mkoa wa Kigoma kwa kupitia kilimo ambapo wananchi sasa wa Jimbo la Muhambwe wanafurahia kufunguliwa kwa jimbo lao kwa kupelekewa mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote ni mashahidi, tumepata mbolea ya ruzuku ambayo imefikia wakulima kwa wakati na kwa urahisi.  Hapa niwapongeze mawakala wetu ambao walijiongeza zaidi na kusogeza karibu zaidi huduma hii ya mbolea kwenye vijiji vyetu ili wananchi waweze kupata mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea hii ya ruzuku imeleta tija sana kwa wakulima wetu kwa sababu bei imepungua, lakini wanaipata kwa wakati na kwa urahisi. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Bashe, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kazi nzuri sana wanazozifanya katika Wizara hii ya Kilimo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tumeshuhudia tangu jana mapka leo tunawapa maua yao kwa kazi nzuri kwa sababu wote tunafahamu wamegusa maisha ya wananchi wengi huko kwenye jamii zetu. Wengi wamesema, wananchi sasa wanapenda kulima, lakini wameiamini Serikali, Wizara ya Kilimo kwa sababu imefanya mambo yanayoonekana. Hongera sana kaka yangu Mheshimiwa Bashe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye Hotuba ya Waziri kwamba tunavyo viwanda vya ndani ambavyo vinahudumia nchi yetu, hivi vimerahisisha upatikanaji wa mbolea ikiwemo Minjingu Phosphate na Itracom hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa mbolea umerahisika kwa sababu ya viwanda hivi, sasa ninadhani ni muda muafaka sasa wa viwanda hivi kupelekewa ruzuku kwa ajili ya mbolea ili mbolea itoke kule kiwandani ikiwa tayari ina ruzuku. Hii italeta multiple effect, kwa nini? Kwanza tutavijengea uwezo viwanda vya ndani kama ilivyo sera kwa nchi yetu kwamba tuwalinde watengenezaji wa ndani. 
Mheshimiwa Mweyekiti, tutaongeza pia ajira kwa vijana wetu kwa sababu kama vitazalisha sana, vijana wetu wataajiriwa zaidi, pia viwanda hivi vitaweza kusafirisha mbolea nje ya nchi. Kwa hiyo, tutapata export levy kwa sababu, wakizalisha ndani zaidi mahitaji yakitosha watapeleka nchi jirani na nchi itajipatia mapato zaidi. Niombe Serikali ifikirie kuvipatia viwanda hivi ruzuku ili viweze kufanya kazi vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umwagiliaji; kwanza niishukuru Serikali nimeona kupitia ukurasa wa 144 umeweka mikakati ya kuendelea kujenga miundombinu ya umwagiliaji. Hapa nimpongeze Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji kaka yangu Raymond alifika Jimbo la Muhambwe, alifika katika Skimu za Lumpungu, Nyendara, Kigina, Kumgondogondo na Kahambe.  Wananchi wa Muhambwe wanamshukuru sana. Leo nimeona kwenye bajeti imeelezea jinsi gani wanakwenda kufanya ukarabati wa skimu zile za Jimbo la Muhambwe ili wananchi wa Muhambwe nao waweze kufaidika kwa kilimo cha umwagiliaji waweze kulima kwa mwaka mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, Serikali ipeleke pesa za kutosha Tume ya Umwagiliaji hizi skimu ziishe pia ambazo zimemalizika kufanyika upembuzi yakinifu ikiwemo za Jimbo la Muhambwe ziweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kipekee Tume ya Umwagiliaji kwa kujenga uzio kwenye Skimu ya Nyendara, kama nilivyoisema hapa Bungeni kuwa ilikuwa inasababisha maafa na mkandarasi sasa yupo site, wananchi wa Jimbo la Mhambwe wanaishukuru Serikali sana ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu sasa skimu ile italeta matokeo na haitaleta maafa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 107 imeongelewa jinsi gani tutakwenda kushirikiana na Serikali katika kuendeleza Skimu ya Lumpungu, wananchi wa Lumpungu wapo tayari, wanaisubiri kwa hamu, wamefurahia uwekezaji huo kwa sababu kipo kipengele ambacho wananchi watapata 20% na wao kuweza kufanya kazi, na tumeshaandaa hati ya pamoja kushirikiana na Serikali ili scheme hiyo ifanye kazi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka wa kuhakikisha utekeleza hii mipango mizuri ambayo Wizara ya Kilimo imefanya, kwa Wizara ya Fedha kupeleka pesa za kutosha. Bila fedha hatutaweza kufanya haya mambo ambayo yamepangwa vizuri sana na Mheshimiwa Waziri Bashe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuja na mpango mzuri wa kujenga miundombinu ya masoko ya mazao ya kilimo kwa ajili ya wakulima katika halmashauri zetu. Nami nimetajwa pale kwenye ukurasa wa 107, Jimbo la Muhambwe tunalima muhogo na muhogo umeporomoka sana.  Kufuatia kilio changu kwa Mheshimiwa Kaka Bashe ninashukuru sasa Serikali imetuona, inakwenda kujenga soko la muhogo, itakuwa three in one, tutakausha muhogo, tutauza muhogo, lakini tutaweka na maghala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaandaa eneo katika Kata ya Nyarioba, tulitakiwa hekta 50 lakini sisi tumeandaa 55 na wananchi wametoa eneo lile bila kuhitaji fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaiomba Serikali, soko hili la muhogo lina manufaa sana kwa wananchi wa Kibondo kwa sababu bei ya muhogo imeporomoka sana kutoka shilingi 800 mpaka shilingi 200, mabenki yamewapatia wafanyabiashara pesa lakini hawawezi kulipa kwa sababu soko la muhogo limeporomoka sana.  Niiombe Serikali mpango huu ulioweka kwenye bajeti, basi pesa iletwe ili wananchi wa Jimbo la Muhambwe waweze kuuza huu muhogo kwenye masoko yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo imeona umuhimu wa kumkopesha mkulima wa Tanzania. Niyapongeze mabenki yote ambayo yanafanya kazi na wakulima, CRDB, NMB, NBC, lakini kipekee hapa niipongeze Benki ya Maendeleo ya Kilimo kupitia Mkurugenzi wake kaka yetu Frank, anafanya kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunakumbuka mwaka jana 2024 wakati benki inaonekana haitaweza kufanya kazi vizuri, Serikali na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi ya dhati na ujasiri aliingiza pesa pale ili kuwaongezea mitaji.  Benki hii kikubwa ilichofanya nimeona kwenye taarifa imetoa bilioni 137 kwa ajili ya wakulima wadogo.  Niiombe Serikali iendelee kuiongezea benki hii pesa, lakini waendelee kushuka kwa mkulima mdogo wa Muhambwe wa Kijijini kule Kigina - Rugogwe ambaye hawezi kufika kwenye mabenki makubwa ili na yeye aweze kunifaika na huu mkopo wa single digit. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo inafanya vizuri katika mazao mengi, tumeona tumbaku ya pili Afrika, tumeona mahindi, Mheshimiwa Bashe amefanya kazi nzuri na Serikali imefanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, wapo mawakala wachache wanunuzi wa mazao kwa wakulima ambao ni wajanja wajanja na hapa nitamtaja JESPAN ni wakala aliyenunua tumbaku katika Jimbo la Muhambwe, AMCOS zangu za Jimbo la Muhambwe bado hawajalipa, mauzo ya mwaka 2020/2021. Ninamwomba kaka yangu Mheshimiwa Bashe, JESPAN awalipe wakulima hawa ambao wanalima kwa shida sana, wanalima kwa jembe la mkono, lakini wanauza tumbaku halafu mtu hawalipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Bashe wasaidie wakulima wa Jimbo la Muhambwe ambao walilima tumbaku lakini wakala wake JESPAN hajaweza kuwalipa.  Hapa nimpongeze DG wa Mamlaka ya Tumbaku, kwa kweli amenipa ushirikiano sana kuhusiana na deni hili, wamelipwa kidogo lakini sasa ni muda wa kumaliza hii pesa yote ili hawa wananchi waweze kupata pesa yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Muhambwe wapo tayari kupiga kura, wakiangalia yale maghala aliyojenga Mheshimiwa Bashe kule Kagezi, Rubongwe, wananchi wa Muhambwe wapo tayari kwenda kupiga kura. Wananchi wa Muhambwe wapo tayari kupiga kura wakiangalia mbolea ambayo imewasaidia kuweza kupata mazao mengi, ikuvuna kwa kiasi kikubwa. Wanasema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hawana cha kumlipa zaidi ya kumpatia kura za kishindo za kutosha itakapofika mwezi wa kumi, kwa nini? Tulijiandaa kwa muda mrefu ndiyo maana sasa tupo tayari kwenda kupiga kura kumchagua Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Wizara ya Kilimo imefanya mambo mazuri makubwa sana, lakini kama Serikali haitaingiza hizi pesa, kama wenzangu wanavyosema, Azimio la Maputo hatujafikia hiyo 10%, hata hiyo asilimia tunayoipanga haiendi kwa wakati na haiendi kwa ukamilifu. Malengo haya mazuri ya Waziri Bashe, malengo haya mazuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hatutaweza kuyafikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu ambao wamesisitiza kwamba tunaiomba Serikali ipeleke pesa za kutosha kwenye Wizara ya Kilimo ili wananchi wetu waweze kufaidika ili Skimu za Muhambwe ziweze kujengwa, soko la muhogo liweze kujengwa, mikopo kwa wananchi iweze kupelekwa na wananchi waweze kufaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo niliyoyachangia, ninaomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja bajeti hii ya wakulima, ya Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)