Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Amandus Julius Chinguile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai, lakini niungane na Wabunge wenzangu kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba Mheshimiwa Rais ameonyesha kwa vitendo namna ambavyo anakwenda kufufua matumaini ya wakulima kote nchini. Tukiona tu hiyo bajeti ya mwaka 2021 na hii bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025, tunaona dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais kwenda kuinua kilimo cha Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili mwenye ubishi bila shaka ana matatizo na hapa hospitali ya afya ya akili ipo karibu Milembe, hawa watu tuwasaidie ili waone nia njema ya Mheshimiwa Rais namna Serikali ya Awamu ya Sita ilivyofanya kazi kuinua kilimo cha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Hussein Bashe na Naibu wake Mheshimiwa Silinde, Katibu Mkuu na Watendaji wote. Wabunge wenzangu wametoa sifa nyingi kwa Mheshimiwa Waziri na Timu yake, lakini ipo sifa ya ziada nitaisema. Mheshimiwa Waziri huyu ni mcha Mungu lakini pia ni mkweli, zaidi ya hayo Waziri huyu hata ukimpigia simu hata saa nane ya usiku anapokea na tabia hiyo amekwenda kuiambukiza kwa Naibu wake, lakini kwa Katibu Mkuu na Watendaji wote. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri, tunaona kazi yake kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze kwenye mchango wangu kwenye maeneo kadhaa. La kwanza kwenye scheme ya umwagiliaji na hapa Mheshimiwa Waziri ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa kabisa. Kwenye maswali yangu nilikuwa nimetoa maswali yanayohusu juu ya scheme hii ya umwagiliaji kwenye maeneo kadhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu yapo maeneo ambayo yana mabonde oevu, yapo mazuri kwa ajili ya kilimo hiki cha umwagiliaji. Na kwa kutambua maeneo haya ninaomba niyataje kwa ruhusa yako, yapo maeneo ya Namanga, Ruponda, Marambo, Chihola, Rupota, Mbondo na Matekwe. Haya maeneo ni mazuri na yana mabonde mazuri yaliyo oevu na kwenye majibu ya maswali niliyokuwa nayauliza walikuwa wanasema bado wanaendelea na utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri maeneo haya tukienda kuweka hizi scheme za umwagiliaji ni zaidi tunakwenda kupandisha sasa morali ya wakulima wetu na wataendelea kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Nachingwea lina Kata 36 na hapa nishukuru kata zote zinao Maafisa Ugani, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina vijiji 127 kwenye eneo hili, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tunao Maafisa Ugani kwenye maeneo haya 16, maana yake tunao upungufu wa Maafisa Ugani 111 na kwa sababu tunaona nia ya dhati ya Serikali kuinua kilimo ni wazi sasa Maafisa Ugani wanahitajika zaidi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anapata nafasi ya kuajiri hawa Maafisa Ugani, tukumbuke kule Nachingwea ili kazi iweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo, niipongeze Idara ya Kilimo Nachingwea inafanya kazi nzuri sana, hawa Maafisa Ugani kwa ngazi zote wamepata vyombo vya usafiri, lakini hapa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, Afisa Kilimo Wilaya, hana usafiri, ili aweze kusimamia vizuri kilimo ni lazima awe na usafiri wa kufaa unaokidhi haja kuwafikia watendaji wetu kule ngazi ya kata na vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Afisa Kilimo wetu Wilaya ya Nachingwea anaitwa Rafael Yusuph Ajetu anafanya kazi nzuri sana, anachapa kazi kweli na ndiyo maana kilimo Nachingwea kinaendelea kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linguine, nimesikia Wabunge wenzangu hapa wanashukuru kwa sababu ya matrekta. Hapa nitazungumza kwa unyenyekevu mkubwa sana. Kule kwetu sisi asilimia ya wananchi wengi wanatumia kilimo cha jembe la mkono. Matrekta haya tafadhali na sisi tunayahitaji, kwa kufanya hivi kilimo tutaendelea kukiinua zaidi, maeneo hayo kwa sasa wananchi wamehamasika sana juu ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka iliyopita kilimo ilikuwa inaonekana ni kazi ya hovyo na ni kazi ambayo wanakwenda kuifanya watu ambao wameshindwa maisha, lakini sasa kilimo hata wananchi wetu wameshagundua sasa kwamba kilimo ndiyo uchumi, kwa hiyo kwa kutuletea haya matrekta, sisi tunakwenda kuimarisha kilimo chetu, siyo tu Nachingwea hata Lindi kwa ujumla.


Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kuhitimisha hapa, ni vizuri aseme neno kuhusu gari ya hisa kilimo kule Wilaya ya Nachingwea na matrekta haya kwenye maeneo haya tutapata lini ili basi kule kazi iendelee na wenzetu waendelee kujipanga kwamba kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu jana hapa wako Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia juu ya ufufuaji wa zao la soya na karanga kule Nachingwea. Mheshimiwa Waziri, zao hili ndiyo lilikuwa maarufu enzi za wakoloni na tulipata reli pale ambayo ilikuwa inatoa karanga na soya kutoka Nachingwea kwenda Bandari ya Mtwara. Kwa sababu ambazo kwa kweli siwezi kuzijadili sasa ile reli iliondolewa, lakini pia na lile zao lilikufa. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye mipango ya Wizara kufufua mazao ya kimkakati twende tujielekeze kwenye zao hili la soya na karanga kwenye Jimbo langu la Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hata leo hapa Mheshimiwa dada yangu Dkt. Thea Ntara amelizungumzia pia, Mheshimiwa mama yangu pale jana, Mheshimiwa Lulida alilizungumzia. Kwa hiyo, ni jambo la muhimu, wakituletea hiyo basi tutaendelea kuongeza mazao ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Tawi la Kituo cha Utafiti Naliendele, kiko pale Nachingwea na hili ninalizungumza kwa unyenyekevu mkubwa, Mheshimiwa Waziri kile kituo kimechakaa. Kile kituo matrekta yote ni mabovu, wakati tunaendelea kuimarisha kilimo, twende tukifufue na kile kituo cha utafiti ili kiweze kufanya kazi kikiwa na zana za kisasa. Ninajua hilo Waziri analiweza, basi anaweza akasema neno hapa ili wataalam wangu kule waendelee kujua kwamba mambo yanakuja na kazi itaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anakuja ku-present hapa Mfumo wa Ununuzi wa Korosho (TMX) hatukumwelewa sana, lakini sasa tunamwelewa sana, tunamwelewa sana. Tunamwelewa sana Mheshimiwa Rais na nia yake njema na kwenye hili sisi kule Nachingwea, wananchi wangu wakati nawatembelea nakwenda kuwaambia nikaseme nini Dodoma? Waliniambia Mheshimiwa Mbunge ukipata nafasi mwambie Mheshimiwa Rais, wakati ukifika huku hana sababu ya kuja, sisi tumeshakubaliana, kura zote kwa Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo hata Liwale sauti ndiyo hiyo. Siyo tu Nachingwea na Liwale hata maeneo mengine ya Mkoa wa Lindi tumekubaliana kwamba, Mama Samia hata kama asije kuomba kura, sisi tumekubaliana kwa namna ambavyo ametufanyia mema kwenye Mkoa wetu wa Lindi, kule kazi inaendelea na sisi tutampa mitano tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ni vizuri nitambue kazi kubwa inayofanywa na Mkuu wangu wa Mkoa, Mama Zainab Telack, anafanya kazi kubwa sana ya kusimamia shughuli zinazoendelea ikiwemo kilimo, pia na Mkuu wangu wa Wilaya, Mheshimiwa Mohamed Moyo, naye anafanya kazi. Mkurugenzi wangu, Engineer Chionda Kawawa, wanafanya kazi ya kusimamia na kuona kwamba mambo yanakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niendelee kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)