Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii muhimu, bajeti ya wananchi na bajeti ya wakulima wa Tanzania. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na takwimu zilizopo ni kwamba, kilimo kinaajiri Watanzania wengi kuliko biashara au shughuli yoyote. Zaidi ya 75% ya Watanzania wanafanya kilimo, hata mtu akiwa mtumishi na yeye anafanya kilimo, kwa sababu kilimo ni sehemu ya majukumu ya kawaida. Kwa hiyo maana yake tukikiboresha kilimo basi tutakuwa tumegusa watu wengi zaidi. Ndiyo maana leo Serikali imeangalia kilimo katika umuhimu wake, imeweza kupandisha bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mpaka shilingi trilioni moja na milioni mia mbili arobaini na mbili kama ambavyo tumesomewa na Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kama ambavyo wamesema wengine kwamba, Azimio la Maputo lilizielekeza nchi zilizopo kwenye ukanda huu kuhakikisha kwamba 10% ya bajeti yake inakuwa ni bajeti ya kilimo kwa sababu, kilimo ndiyo kinazalisha malighafi za viwanda, kilimo ndiyo kinachozalisha chakula kwa maana ya usalama wa chakula, lakini kilimo ndiyo kinachosababisha hata viwanda vifanye kazi. Kwa hiyo maana yake, kilimo kikizingatiwa kinaweza kuchochea shughuli za uchumi kwenye sekta zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo baada ya maneno haya ya mwanzo, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ambayo ameionesha wazi kwa utekelezaji mbalimbali wa bajeti na mipango ya Serikali kwenye sehemu ya kilimo. Amefanya kazi hii kubwa sana ambayo leo tunaona imepandisha na kuleta hata ruzuku ya mbegu, ruzuku ya mbolea, imeongeza hekta za umwagiliaji, lakini na afya ya udongo ambayo huko nyuma tulikuwa tunapigia kelele kama Bunge.  Leo tumeanza kuona hata vifaa vya kuangalia afya ya udongo pia tumeongeza Maafisa Ugani. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani hawa wamewezeshwa hata usafiri katika maeneo yetu. Kwenye hili eneo ninaomba tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya utekelezaji wa shughuli za kilimo. Zaidi nimpongeze sana Ndugu yangu Mohamed Hussein Bashe kwa namna ambavyo ameisimamia sekta hii. Kwa kweli tunamwona ana passion ya kilimo, anafanya kazi nzuri, wakulima wa nchi hii wana imani na yeye na kwa hakika kile anachosema ndiyo anachotembea nacho. Amekuja mwaka huu ametupa tathmini na tunaona mwenendo mzuri wa kilimo. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na wenzake kwa maana ya Naibu Waziri Mheshimiwa Silinde, Katibu Mkuu Ndugu Mweli na wataalam wote walioko kwenye eneo hili, wanafanya kazi nzuri na Mungu aendelee kuwabariki sana. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maeneo haya, ninapongeza kwa upande wa Ikungi. Ikungi, nilisimama mwaka wa fedha 2022/2023 nikasema kwamba, miongoni mwa maeneo ambayo hatujafanya vizuri ni kutuwekea hata ruzuku ya kilimo katika eneo la zao la alizeti. Tukasema kama tunavyoweza kupata ruzuku kwenye pamba, kama tunaweza tukapata ruzuku kwenye korosho, kwa nini isiwe alizeti ambalo ni zao muhimu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafurahi kusema kwamba mwaka huu tunaoenda kuumaliza tumeweza kupata ruzuku ya mbegu ya alizeti tani 57.8, jambo hili ni kubwa ambalo sisi watu wa Ikungi tunashukuru sana. Kama haitoshi tumepata tani 710 ya mbolea ambayo imeenda kusaidia kuongeza uwezo wa uzalishaji wa mazao mbalimbali, tumeweza kupata hata mbegu ya mahindi ambayo huko nyuma ilikuwa haipo, tumepata tani 571 na hii jumla yake ilikuwa gharama ya shilingi trilioni mbili, bilioni mia nne thelathini na nane, mia tano sitini na nane. Katika hili Serikali imetuletea ruzuku ya shilingi trilioni moja, bilioni mia saba kumi na saba, sawa na 70%, Serikali imetuwekea fedha hii, tuseme nini? (Makofi) 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa kutuwezesha kutuletea ruzuku hii ambayo leo imewawezesha wakulima zaidi ya 63,000 ambao wameweza kufanya kazi hii nzuri. Kwa hiyo, ninaomba nihakikishe kwamba, itatusaidia kuongeza sana uzalishaji. Kwenye eneo hili la alizeti, ninaiomba sana Serikali iongeze uwezo wa mbegu ili uweze kusaidia wakulima kuzalisha zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; niweze kuchangia kwenye suala la mbolea. Tumekuwa na uwekezaji, wawekezaji wamevutiwa sana, Mheshimiwa Rais amewavutia wawekezaji na wamewekeza kwenye Sekta ya Mbolea. Tuna kiwanda ambacho kipo hapa Dodoma, ambacho kimeweza kufanya kazi nzuri ya uzalishaji. Kiwanda hiki cha ITRACOM ambacho kinazalisha mbolea hizi za FOMI, ambazo ni mbolea nzuri na ni mbolea tofauti na mbolea nyingine ambapo inaweza kukuza mazao, lakini pia inaweza kuboresha afya ya udongo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana wenzetu hawa waliowekeza waweze kulipwa fedha ya ruzuku, ili waweze kutoa mbolea kwa wingi na walipwe fedha ambazo wanadai Serikali ili wawe na muscles ya kuendelea ku-supply mbolea. Tukiwezesha vizuri eneo hili, tutasadia kuongeza tija ya kilimo na tutaongeza mazao mengi na zaidi, tutaenda kuwasaidia ajira Watanzania hawa. Hapa Dodoma kiwanda kipo kinazalisha ajira nyingi, tunaomba wawajali, wawaonyeshe na waweze kuwavutia wawekezaji wengine waje wawekeze katika sekta mbalimbali ambazo Mheshimiwa Rais ameendelea kuwavutia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi niombe sana maeneo mawili: eneo la kwanza ni suala la umwagiliaji. Minara ya skimu yangu Mheshimiwa Bashe anaijua ya pale Mang’onyi. Ninajua Naibu Waziri naye pia anajua, lakini amenielekeza kwa wataalam kazi nzuri inafanyika. Niombe sana zile fedha zitoke, Mkandarasi apatikane ili ile Skimu ya Umwagiliaji ya Mang’onyi iweze kuanza kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana mabwawa pia yaweze kuchimbwa maeneo ya Lighwa pale Msule kwa maana ya Misughaa pamoja na hapa Choda eneo ambalo lina ardhi nzuri sana, ili wakulima wawe na mazao mbadala kwa ajili ya kufanya hivyo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mwaka huu kumekuwa na tatizo la hali ya hewa, tabianchi imebadilika na mvua hazikuwa nzuri. Niombe sana mazao yatashuka, hivyo kazi nzuri iliyofanyika na NFRA mwaka juzi, ndugu yangu Komba yuko pale ninaomba na mwaka huu watuangalie katika hifadhi waweze kutuletea chakula kupunguza makali wakati tunaenda kujiandaa kwa ajili ya uvunaji upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja ili tukafanye kazi ya wakulima wa nchi hii ambayo Mheshimiwa Rais amewajali sana. Ahsante sana. (Makofi)