Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya bajeti hii muhimu, Bajeti ya Kilimo. Kwanza ningependa kutoa pongezi kwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutuongoza vizuri kwa falsafa zake za 4R na vilevile, kwa kuhakikisha kwamba Wizara hii muhimu inapata bajeti ambayo inaashiria umuhimu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia bajeti hii ilivyopanda kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 ambayo ilikuwa ni shilingi bilioni 294 hadi leo ambapo tunaongelea bajeti hii inayoombwa ya mwaka wa fedha 2025/2026 ya shilingi trilioni 1.24. Hiki ni kiashirio kizuri cha lengo thabiti cha bajeti hii inalenga nini katika kumkomboa Mtanzania. Kwa kazi hii nzuri ya Rais, zawadi nzuri ambayo tunaweza kumpatia ni katika muda muafaka mwezi Oktoba, tuhakikishe kwamba anapata mitano mingine tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kutoa pongezi kwa Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe, ambaye anafanya kazi nzuri ya kuiongoza hii Wizara na vilevile, kwa kuisimamia vizuri Wizara hii ambayo ni muhimu inayohitaji usimamizi mkubwa pamoja na kwa kutuletea bajeti ambayo ina matumaini kwa wote. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kutoa pongezi kwa wasaidizi wa Waziri nikianza na Naibu Waziri wake Mheshimiwa David Silinde; Katibu Mkuu Gerald Mweli; na Naibu Makatibu Wakuu Dkt. Hussein Omar na Dkt. Stephen Nindi, ambapo inaonyesha wanatoa usaidizi mzuri kwa Waziri huyu ambaye ametuletea bajeti yenye kutia moyo. Ikiwezekana timu hii Mheshimiwa Waziri uitunze sana, kwani inaelekea inakusaidia sana. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa Mradi wa BBT. Mchango wangu karibu wote utajikita hapohapo kwenye huu Mradi wa BBT ambao kwangu mimi ninaona ni mpango mzuri sana, ambao umeazimia kutukomboa katika Sekta hii ya Kilimo. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mradi huu umelenga katika kuongeza ajira kwa vijana na wanawake ambao wanaweza kuitumia ardhi yetu ambayo tunayo tele nchi hii, lakini vilevile, tuna wateja wa kutosha wa mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi hii. Tunampongeza kwa kugeuza kilimo, kwa ile dhana ya “Kilimo, Biashara”. Kilimo kiwe ni biashara na biashara hii iweze kumfaidisha kila mtu kwa mafao yake kwamba siyo chakula tu, bali vilevile twende kukifanya kuwa ni biashara. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuuelezea huu mpango wa BBT kwamba, jinsi ulivyo na ulivyo mkubwa, tutarajie matunda yake yaonekane kwa hatua. Yaani hayawezi kuwa matunda ya ghafla, kwani ni mpango mkubwa sana. Ningependa kuuita kama gogo twende taratibu kwamba: “Bandubandu Humaliza Gogo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuigawanya katika vipengele mbalimbali. Nilivyopitia randama yake pamoja na hotuba yake nimeona kuna BBT Ugani, ambayo imejigawa katika mambo fulani; kuna BBT Mitaji, ambayo imejikita katika kutoa uwezeshaji wa kifedha kwa hawa wahusika; ina BBT Miche, ambayo imetoa miche kwa ajili ya Wakulima hao; lakini kuna BBT Visima, ambayo imejikita katika miundombinu ya kusaidia umwagiliaji katika mpango huo; kuna BBT Mashamba, ambayo imetoa mwelekeo mzuri katika upatikanaji wa ardhi ya hawa walimaji; lakini kuna BBT ya ngazi ya Halmashauri, ambayo inausogeza karibu zaidi mradi huu kwa wahusika wenyewe. Kwa hiyo ninampongeza Mheshimiwa Waziri, kwa huo mpango wake wa “Bandubandu Humaliza Gogo.” 
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumshauri Mheshimiwa Waziri kitu kimoja kwamba, katika makundi haya ambayo amelenga ya vijana na wanawake, kuna kundi moja kubwa ambalo lipo linaweza likakusaidia sana katika kuboresha mradi huu. Hili ni kundi ambalo nitaliita ni kundi la walio tayari. Hili kundi la walio tayari ambao wengi wao ni middle class (watu wenye kipato cha kati) lipo, lakini lenyewe ukiliwekea mpango mahususi litaweza kusaidia sana katika mradi huu bila kumwongezea gharama kubwa sana. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwa mfano katika ukurasa wa 80 na 81 wa randama ya Waziri. Ukurasa wa 80 umeongelea kuwezesha zana za kilimo, 81 umeongelea kuwezesha upatikanaji wa ardhi; lakini hawa walio tayari, tayari wana ardhi na wengine wao tayari wana mitaji. Kwa hiyo utajikuta sasa kwamba, kinachohitajika ni kuwasaidia vitu fulani fulani tu.  Kwanza Waziri awasaidie miundombinu, ambapo awapelekee kule barabara na visima kwa ambao watakuwa tayari; lakini vilevile awapatie miche na ugani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba hawa, Waziri awawekee mfumo ambao utawawekea vivutio. Kwa mfano, anaweza kusema kwamba kama una ardhi tayari na una kitu hiki na mmejikusanya mpo 10 kwenye mashamba ya ukubwa huu, then nitawaletea barabara au mtakuwa eligible kupata visima. Kwa hiyo watajikuta kwa hawa watu ambao wana ardhi, wana mitaji yao, basi yeye awamsaidie kuwaongezea kama visima ili  kumwagilia vizuri, awasaidie waweze kupata barabara ili waweze kufika katika ule mradi wao kwa urahisi zaidi. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kulenga mradi mmoja wa BBT ambao Mheshimiwa Bashe akiulenga nao utatusaidia sana. Katika mpango wake nimeona kuna BBT Tanga, (Korogwe au wapi) kuna BBT ambayo ameilenga kuwa ya mkonge ambayo iko Tanga. Ninapendekeza angekuwa ana BBT nyingine pale Butiama ingemsaidia katika ule mradi wa umwagiliaji Butiama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi ni mradi dada wa mradi wa Bugwema ambao ulikuwepo. Ninaufahamu vizuri kwa sababu nilianzia kazi pale ambapo tayari bwawa la kumwagilia lipo, shamba lipo na pale jirani kuna Chuo cha Mwalimu Julius Nyerere University of Agriculture and Technology. Kwa hiyo akiunganisha ile elimu ya pale ya kilimo na BBT pale shamba la umwagiliaji ninadhani atapata matokeo mazuri zaidi na kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona umeniwashia taa. Ninaunga mkono hoja, ahsante sana.  (Makofi)