Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa. Nami nianze kwa pongezi na kwa hakika wakati ninaingia humu ndani na leo ni siku yangu ya kuchangia nimepokea simu nyingi sana kutoka kwa Wanambarali hususani wakulima wa Mbarali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamenituma nifikishe salamu za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mapinduzi makubwa ya kilimo ndani ya ya Wilaya yetu ya Mbarali hayapigiwi mfano. Pia, wamenihakikishia kwamba, siku Mheshimiwa Rais atakapopita Mbarali tumemwandalia mpunga wa kutosha na ng’ombe wa kutosha kama shukrani kwa kazi kubwa aliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haijaishia hapo. Wanambarali tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri kaka yangu Hussein Bashe na timu yako yote. Kaka yangu yeye ni mtu na nusu na ana utu, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanambarali wameniambia tutamtafutia kiwanja kaka Bashe Mbarali, ili ajenge pale Mbarali awe mkazi wa Mbarali. Hiyo yote ni shukrani kwa kazi kubwa ambayo ametufanyia Wanambarali. Akichelewa kujenga kaka Bashe, sisi Wanambarali tutaanza wenyewe kumjengea lakini haimaanishi aje agombee Ubunge Mbarali, hapana! Anakuwa tu mkazi wa Mbarali. Pia, anaye Naibu Waziri bingwa kabisa, ambaye anamsaidia kazi na sina shaka na wananchi wa Tunduma watampa mitano tena; sina shaka kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii imejipambanua vizuri sana. Kiukweli kabisa wanayo nia ya dhati ya kuwasaidia wakulima kwa sababu wao wenyewe timu ya Wizara wanapenda kilimo na wanawapenda wakulima wa Taifa hili na ndiyo maana wamekuwa wakihangaika kwa dhati kabisa na shughuli za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanambarali kwa muda mfupi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyokuwa madarakani, tumepata miradi mingi ya kilimo mpaka tunashangaa. Hivi ninavyokwambia, tuna miradi mitano inaendelea; wakandarasi wapo huko na mimi huwa ninapita mara kwa mara. Kwa dhati kabisa ana timu nzuri sana ya Tume ya Umwagiliaji, kaka yangu Mndolwa.


Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wasaidizi wake pale Engineer Banzi, wanafanya kazi nzuri sana; ninawapongeza. Leo ukienda pale mradi wa Chosi unaendelea; Mradi wa Matebete unaendelea; Mradi wa Utulo unaendelea; Mradi wa Mbuyuni unaendelea; Mradi wa Msesule unaendelea, zaidi ya shilingi bilioni 80 tumeshapokea miradi yote inaendelea, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametuongezea pia miradi miwili ya shilingi bilioni 60 Mbarali. Mradi wa Madibira phase two na phase three yote inaendelea na tunashukuru inaanza. Pia, mradi mwingine wa Njombe – Isitu ambao unaendelea, tunashukuru sana. Kwa kweli, sisi kule hatuna shaka tunasema Mheshimiwa Dkt. Samia mitano tena, hatuna shaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mingine minne ambayo nimeshukuru sana Tume ya Umwagiliaji walifika, walikutana na wadau na wamesainishana mikataba. Miradi ile ambayo itaenda kwenye World Bank, inayofadhiliwa na World Bank ya P4R minne. Pale tuna Gwiri; tuna Igomelo; tuna Mwendamtitu; na tuna Mradi mwingine wa Utulo. Kwa kweli sisi tunaiona Mbarali baada ya miradi hii kukamilika, Mbarali itakuwa ni kitu kingine eti, kabisa, kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la miradi ya mabwawa. Nilikuwa huko Mbarali, sasa hivi kuna Mkandarasi anafanya study ya mabwawa. Mbarali peke yake tuna mabwawa saba yanayoenda kuchimbwa. Jamani sisi tuseme nini Mbarali, zaidi ya kumsubiria huyu mama na kumpa mitano tena tuanze kazi hii, aimalizie vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Bwawa la Rwanyo, tayari Mkandarasi ameshafanya tathmini; Bwawa la Mto Chimala; Bwawa la Kimani; Bwawa la Mto Mbarali; Bwawa la Dudumizi; Bwawa la Mambi; na Bwawa la Mto Ndembela, yote hii ni kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais anajaribu kutusaidia Mbarali tuondokane na matatizo makubwa. Ninaamini kabisa matatizo makubwa ya Mbarali ya migogoro mikubwa, hii ndiyo suluhu yake. Baada ya miradi hii kukamilika, nina uhakika kabisa tunakwenda kuua baadhi ya migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninayo maombi machache. Mheshimiwa Waziri, kwanza tukushukuru sana na tukupongeze sana kupitia hotuba yako ya jana. Umeweza kulirudisha shamba la ekari elfu sita na, kwa wananchi, tunakushukuru sana na Wanambarali wanakupongeza sana. Mheshimiwa Waziri tuendelee kutafuta maeneo kwa ajili ya wakulima wetu wadogo na hili eneo lililopatikana tunaomba liwafikie walengwa waliokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusione sasa wanaenda kumegeana watu wachache tukarudi kwenye matatizo yaleyale badala ya kwenda mbele zaidi. Nimwombe sana tusimamie kwa uadilifu mkubwa, wakulima wadogo wa Mbarali waweze kusaidiwa wapate maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali. Tunakwenda kutengeneza uwanja ule wa John Mwakangale pale Mbeya wa Nanenane, uwanja ambao utakuwa ni mkubwa East Africa hakuna mfano. Tunashukuru sana Serikali, kupitia maonesho yale ya Nanenane yatawasaidia wakulima wa mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini kuweza kuonyesha umahiri wao kwenye suala zima la mazao; tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Bashe ambalo ninamwomba Waziri kwa dhati kabisa. Nimeona kwenye hotuba yake, kwamba wanakwenda kufungua matawi ya Benki hii ya Ushirika manne na wametaja tawi moja linaenda...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshamaliza muda?

MWENYEKITI: Malizia nusu dakika.

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kiukweli. Nimeona matawi manne ambayo yako Tabora, Mtwara, Dodoma, na Kilimanjaro. Niwaombe kwa Nyanda za Juu Kusini watuwekee tawi pale Mbeya. Ni suala muhimu ambalo litatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru kwa kupata nafasi. Mungu awabariki, tunawaombea Wizara ya Kilimo warudi waendeleze kazi hii na tunawapenda sana na wakulima wanasema “Mitano Tena.” Ahsanteni sana. (Makofi)