Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi mchana wa leo kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujaalia afya njema. Pia, niende moja kwa moja kwamba, ninaiunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nianze kwa kuwapongeza askari miavuli wa Wizara hii ya Kilimo kuanzia: Mheshimiwa Bashe; Naibu wako Mheshimiwa Silinde; Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa namna ambavyo wamemsaidia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka rekodi mpya kwenye Sekta ya Kilimo ndani ya miaka minne ya Utawala wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imeshuhudia kauli mbiu mbalimbali. Kulikuwa na masuala ya “Siasa ni Kilimo”; “Kilimo cha Kufa na Kupona”; na “Kilimo Kwanza”, lakini ndani ya utawala wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ajenda ya 10/30 imeleta matumaini na imekifanya kilimo kwa watu wengi kuwa kwamba inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapochangia bajeti ya Wizara hii ya Kilimo, binafsi ni shuhuda wa mafanikio yaliyopatika kwenye Sekta hii hususan nikijielekeza kwenye pembejeo na viuatilifu hasa vya zao la korosho. Mheshimiwa Waziri kwanza, hotuba umeiandaa ya kimataifa, hotuba nzuri ambayo imeainisha mafanikio unayaona moja kwa moja, nikupongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyosema jina la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan litaandikwa kwa wino wa dhahabu kwa namna ambavyo ameimarisha kilimo, lakini wewe Mheshimiwa Waziri ni Waziri pekee kwenye Wizara hiyo ya Kilimo ambaye ameweka rekodi ambayo itakuwa kwenye vizazi na vizazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema mimi ni shuhuda. Tumefanya ziara na UWT-Taifa chini ya uongozi wa mama Chatanda na mama Shomari kwenye Mikoa ya Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo, kupitia mikutano ya hadhara kwenye kata na vijiji, tumepokea salamu za shukrani kwa wakulima, hususani wanawake. Tumeona kwa kushuhudia namna pembejeo zilivyowafikia wananchi, namna viatilifu vilivyowafikia wananchi na tumeshuhudia mabwawa haya yanayoendelea kujengwa na Wizara yako, likiwemo Bwawa la Membe la hapa Dodoma; binafsi nimetembelea bwawa hili, nilipangiwa kutembelea Bwawa la Msagali, Wilaya ya Mpwapwa. Tumeona block farming, ambayo ipo hapa Kata ya Makambako, ni kazi kubwa iliyofanywa na Wizara, lakini nimpongeze pia ndugu yangu Raymond kwa kazi nzuri aliyofanya katika sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ombi, pamoja na ongezeko kubwa la bajeti kufikia shilingi 1.2 trillion na mabwawa yanayoendelea katika Mkoa wetu wa Pwani, wamefanya upembuzi yakinifu kule Rufiji, Ngorongo pale na Kibiti na pia, wameshapata mkandarasi, ombi langu ni wazitazame hizi skimu, ya pale Ruvu, Chauru na Bagamoyo, ni ambazo miundombinu yake ni chakavu. Wakitenga pesa kidogo tu pale, tunataka ukarabati wa miundombinu, kutujengea tuta kwenye Skimu ya Bagamoyo, ili kuzuia mafuriko na vifaa, kama trekta na power tiller, kwa ajili ya wakulima wetu, lakini wanashukuru sana kwa mbolea ya pembejeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye Skimu ya pale Chauru wameomba kuongeza eneo la umwagiliaji hekta kama 1,300 zinaweza kutosheleza. Tunashukuru kwa BBT ya Kisarawe, wametuweka kwenye mpango kwenye wilaya 20, ambapo pale Palaka eneo limejengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kiwanda cha kubangua korosho cha kwanza, baada ya miaka mingi vile vingine vya Kibaha kufa, wanakijenga Wilaya ya Kisarawe. Hivi karibuni, kama wiki mbili zilizopita, Mama Chatanda alikitembelea pale Mzenga na kazi inaendelea. Tunaomba tu usimamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea viatilifu vya korosho kutoka kwa ambao wanendelea kugawa mbegu katika maeneo yetu. Ninataka niseme, Mheshimiwa Bashe amepewa maua yake, siku ile ya kuzindua benki ya ushirika mimi binafsi nilikuwa kwenye Wilaya ya Nzega, kwenye mkutano wa ndani, Mambali pale, Mwamala na maeneo mengine; nimemsemea vizuri kwamba, Wilaya ya Nzega na Mkoa wa Tabora imetupatia kijana mpambanaji. Niwatakie kila la kheri na ninawaomba wawarudishe ninyi wote wawili na ikimpendeza Mwenyezi Mungu waendeleze hii ajenda ya 1030.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, lakini kwa kweli, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka rekodi ambayo itaishi vizazi na vizazi kwa kutuwezesha, hasa wanawake ambao ni 65% wanaojihusisha na kilimo, kupata pembejeo na bei nzuri ya mazao. Ahsante sana. (Makofi)