Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa ya kusema hapa Bungeni siku ya leo. Awali ya yote nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyejalia uhai na ametupa fursa ya kukutana tena kutimiza majukumu yetu hapa Bungeni siku ya leo. Pili, nitumie fursa hii, kwanza kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utendaji wake uliotukuka na hususan kwa kuleta miradi mingi ya maendeleo kwenye Jimbo letu la Nzega, lakini pili nimshukuru kwa kuendelea kumwamini Waziri wetu wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, niwapongeze Mheshimiwa Rais, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri Hussein Bashe, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu ndugu Mweli na watendaji wote wa Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kwenye sekta hii nyeti, ambayo ni uti wa mgongo wa maisha ya Watanzania, ni uchumi wa Watanzania. Bajeti ya kilimo ni bajeti ya watu na kwa namna ambavyo Mheshimiwa Rais na Waziri, Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, wanafanya kazi kwenye Wizara hii ni wazi kabisa majina yao siyo tu yataandikwa kwa wino wa dhahabu, lakini pia, yatakuwa casted kwenye mwamba imara wa jiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, leo nimekusudia kuongelea jambo moja tu na ndilo ambalo kwa kweli, limeniinua niseme hapa Bungeni siku ya leo baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu na lenyewe ni suala la umwagiliaji. Kama kuna jambo la busara, la hekima na la mapinduzi ambalo, Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, akiongozwa na utashi na mwongozo (vision) sahihi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, litafanywa katika nchi yetu tayari, tumeanza kufanya kwa uchache wake na ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii unaona sasa tunaenda kimkakati na kwa ukubwa zaidi, basi ni suala la umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo litaenda kuleta mapinduzi makubwa kwenye maisha ya watu, ni jambo ambalo kiukweli sina maneno mazuri zaidi ya kuwapongeza, lakini binafsi kwa uelewa wangu mdogo wa uchumi wa mwaka 2050 unaokuja, naona litaenda kui-position Tanzania kwenye nafasi kubwa na ya kipekee sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo niwapongeze sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa kuamua kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la umwagiliaji. Kwa nini nasema hivyo? Ukisoma Taarifa ya Idadi ya Watu Duniani, ambayo inatolewa na Shirika la Kiuchumi na Maendeleo ya Watu la Umoja wa Mataifa iliyotoka mwaka 2022, World Population Prospects ya mwaka 2022, unaona Dunia kufikia mwaka 2050 itafikisha idadi ya watu takribani bilioni 10, bilioni 9.7 Afrika, ambayo ndiyo itakuwa ina ukuaji wa hali ya juu wa idadi ya watu, itakuwa na mchango kwenye idadi hiyo wa takribani 25%. Katika nchi za Afrika ambazo zitakuwa zina ukuaji mkubwa wa idadi ya watu Tanzania ipo kwenye top four, ikiwemo DRC, Nigeria na Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, kutakuwa kuna changamoto kubwa sana ya uhakika wa chakula, food security, ifikapo Mwaka 2050, lakini Tanzania tuna bahati na fursa ya kipekee; tuna maziwa na mito ya maji baridi. Tunaweza tukawa food exporters kwa nchi za jirani na pia, kwa dunia kwa ujumla wake, lakini pia, Tanzania tutakuwa na changamoto ya kuwalisha takribani Watanzania milioni 140 ambao wanakadiriwa, kwenye ripoti hiyo, kuwa watakuwepo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mbali na uwepo wa idadi kubwa ya watu miaka 25 tu ijayo wengine humu, kama tutajaliwa kuwa hai, tutashuhudia. Tutakuwa tuna fursa ya kuwa na food exporters kwa nchi za jirani na nyinginezo, kwa hivyo, Mheshimiwa Bashe, endelea kuwekeza kwenye diplomasia ya chakula, food diplomacy, kama juzi hapa alivyofanya kwa wenzetu, ili tujenge soko imara kwenye uchumi unaokuja katika dunia, ambapo sisi tunakadiriwa kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo zitakuwa zinakuwa kwa kasi zaidi kwa idadi ya watu na pia, kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo gani tufanye. Mheshimiwa Bashe kwenye ripoti yake ameanzisha mradi mkubwa sana kutoka Ziwa Victoria na pia, kutoka Ziwa Tanganyika, ambao utakuja mpaka huku ndani kabisa ya nchi yetu. Ninampongeza kwa wazo hilo, ninaamini mradi huu ukitekelezwa, kama ambavyo anaeleza kwenye ripoti yake, utakuwa umefanya jambo la kukumbukwa katika historia kama ambavyo Farao Amen Het wa kule Misri anakumbukwa kwa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji. Utakumbukwa kama wale wa Iraq ama Wambulu walivyofanya Skimu yao ya Umwagiliaji kule Engaruka miaka takribani 500 na 600 iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi unashangaa kwamba, sasa sisi watu wa leo tunashindwa akili na ancestors wetu wa miaka 500, 600 iliyopita? Kwamba, kwa nini tulikuwa hatuendi kwenye kilimo cha umwagiliaji wakati tuna historia ya kuwa na skimu miaka 600 iliyopita kule eneo la Engaruka Katikati ya Mlima Oldonyo Lengai na Bonde la Ziwa Natroni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini leo hii hatuna kilimo cha umwagiliaji? Kwa nini Skimu ya Engaruka ilikufa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata tukijifunza pale tu tunapata somo kubwa sana la kui-position Tanzania, kama giant food manufacturers na food exporter katika dunia inayokuja kwa hivyo, nikupongeze kwa kufikiria wazo hili. Mambo ya kuzingatia ya muhimu, kwa sababu ya muda; lazima skimu hii kubwa ambayo unaijenga, achilia mbali hizi nyingine mbalimbali ambazo mmeanza kuzijenga ikiwemo Skimu yangu ya kule Budushi, ya kule Manonga, Nehele na maeneo ya jirani, hii skimu kubwa ambayo inakuja, Waziri ahakikishe wanavyoi-design wawe wamei-pair up, wamei-link up vizuri, wameifungamanisha na wazalishaji kwa sababu, kwenye hiyo ripoti ya mwaka 2050 zaidi ya 50% ya Watanzania watakuwa wanaishi kwenye majiji. Maana yake ni wakulima hawa wa leo wa jembe la mkono hawatokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha wakati huo kitakuwa ni cha kibiashara, kitakuwa ni cha watu wakubwa zaidi, kwa hivyo kitatoa ajira nyingi, kitatusaidia kutatua tatizo la ajira ambalo linakusudiwa kuwa ni tatizo mama la mwaka 2050. Kwa hivyo, huu mkakati wanaoenda kuwekeza sasa hivi ni mkakati ambao utapunguza vurugu na chaos ambazo zinatarajiwa, kama tusipo tatua tatizo la kuwa na young population kwa zaidi ya 65% ifikapo mwaka 2050.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lazima scheme hii iwe designed kufanya Agro-industrialization. Kuwe kuna viwanda pembeni ya skimu, kuwe kuna ushirika ambao unakuwa linked na ku-manage hizi skimu. Kuwe kuna ulinzi wa vyanzo vya maji, mito, mabonde na pia, kuwe kuna mkakati mzuri wa GIS, kutumia better science, kwa ajili ya ku-manage idadi ya watu katika Taifa letu na namna wanavyosambaa kwenda kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Skimu ya Engaruka ilikufa kwa sababu, Wamasai ambao ni wafugaji walienda kuwavamia Wambulu. Hata huko mbele hivyo hivyo wafugaji watavamia maeneo ya wakulima, kwa hivyo, ili kilimo kiwe salama ni lazima mikakati ya kulinda maeneo ya ardhi ya kilimo iwekwe vizuri; kuwe kuna upimaji, lakini pia, kuwe kuna ugawaji mzuri wa maeneo, ili ardhi ambayo ni fertile ya kilimo isipotee kwa sababu, hatujajipanga vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwe kuna uendelevu wa mradi huu ni lazima uanzishwe Mfuko wa Kilimo cha Umwagiliaji ambapo, kutakuwa kuna muda mrefu wa kutekeleza miradi ya umwagiliaji, kutakuwa kuna vyanzo vya uhakika vya fedha na hakutokuwa na athari, ambayo itasababishwa na mabadiliko ya viongozi kwenye hii Wizara. Hapa sasa hivi namwombea dua, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais asimwondoe kwenye Wizara hiyo mpaka miradi hiyo aimalize.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Kigwangala.

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima sasa mifumo iwekwe na Serikali, ambayo italinda kilimo cha umwagiliaji na miradi mikubwa kama hii kwa muda mrefu, kama tulivyofanya kwenye barabara na tunavyofanya sasa kwenye reli. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)