Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, bajeti ya wananchi. Ili kuweza kuongoza nchi kwa utulivu ni lazima kuangalia usalama wa chakula na hili Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweza sana. 
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema ameweza kwa sababu, ni kwa kipindi chake amekwenda kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka shilingi bilioni 294 hadi shilingi trilioni 1.2. Hii siyo kazi rahisi, Mheshimiwa Rais ameonesha kwa vitendo dhamira yake njema kuhakikisha Watanzania walio wengi wanakwenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye kilimo hii Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ameendelea kutupigania Watanzania. Ninashukuru na ninampongeza sana Waziri wa Kilimo, ndugu yetu Mheshimiwa Hussein Bashe, msaidizi wake Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde, Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Kilimo pamoja na watumishi wote kwa namna ambavyo wanasimamia kwa vitendo dhamira njema ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinakuwa na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kuongelea suala la kilimo cha umwagiliaji. Tumekuwa tukiongelea suala la umwagiliaji kwa muda mrefu, lakini tumeona kipindi hiki cha Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekwenda kufanya mapinduzi makubwa kuhakikisha ameanzisha skimu za umwagiliaji katika maeneo mbalimbali. Katika Mkoa wetu wa Manyara tumepata skimu nyingi; tumepata Skimu ya Bashay, Kiru Six, Matufa, Kisangaji, Gichameda, Tlawi na maeneo mengine. Maeneo haya kwa sasa yanazalisha vitunguu, mpunga na viazi. Tunaona ni kwa namna gani wananchi wetu wamekwenda kujikomboa kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kushauri; kwa sababu, kilimo tulichonacho cha umwagiliaji kwa sasa ni kwa njia ya mifereji, ninapendekeza, Mheshimiwa Waziri, tuangalie namna ya kuweka umwagiliaji kwa njia ya matone ili tuweze kumwagilia maeneo makubwa zaidi. Kwa sababu kwenye umwagiliaji wa mifereji tunaweza kumwagilia.  Kwa mfano mtu analima heka moja, lakini tukipeleka kwa njia ya umwagiliaji wa matone (drip irrigation) tunakwenda kumwagilia maeneo makubwa zaidi badala ya heka moja mtu unamwagilia hadi heka nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninapenda nipendekeze hili ili Wizara ione namna gani ya kwenda kusaidia wananchi wetu ambao tayari wamejihusisha na kilimo cha umwagiliaji wakamwagilie maeneo makubwa na kuzalisha mazao ya kutosha katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze kwa kuanzishwa kwa maabara ya kuanzisha miche. Hili linakwenda kuleta mapinduzi makubwa kabisa kwa sababu tutapata miche iliyo bora, miche ambayo inaweza ikastawi katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kwamba pilot ianzie katika Mikoa ya Manyara, Arusha na Kilmanjaro; kwa maana ya kwamba tutakwenda kuzalisha zaidi kulingana na mazingira yetu. Kwa hali ya hewa iliyo katika maeneo yetu tupate miche ya kutosha ili wananchi wetu wakazalishe mazao ya kutosha. Pia Mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro ni wazalishaji wazuri pia wa zao la ndizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara itafute namna ili tuwekeze kwa kiwango kikubwa katika mikoa hii niliyoitaja uzalishaji wa ndizi ili tuzalishe zaidi na kwenda kufanya export ya mazao yetu na kupata fedha za kutosha katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kuomba Serikali isogeze huduma ya kifedha ya Benki ya Kilimo pamoja na ule Mfuko wa Pembejeo. Benki hizi ziko kikanda, kwa hiyo niombe sasa Serikali itafute namna ya kuwasogezea wananchi katika maeneo yao ili mtu anapohitaji kukopa iwe rahisi kupata mikopo badala ya kusubiri watu kutoka maeneo ya kanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze uboreshaji wa TARI na ASA katika kuboresha uboreshaji uliyofanyika. Niendelee kuomba, kwamba sasa Serikali itafute namna ya kuboresha miundombinu, iboreshe vifaa, iwaboreshee wataalam wetu na kuwapatia ujuzi wa kutosha ili waweze kwenda na kasi iliyopo pamoja na kwenda na mazingira tuliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiagiza baadhi ya matunda katika nchi yetu kutoka nje; kwa mfano, mapeasi na matunda kama ma-apple. Niombe Serikali itafute namna ya kwenda kuzalisha mazao haya au matunda haya katika maeneo yetu. Mfano mdogo tu, kwamba tunayo maeneo ambayo tunaweza kuzalisha matunda kama peasi, apple, mfano, Babati, Manyara, Mbulu, tuna uwezo wa kuzalisha matunda haya. Kwa hiyo niombe matunda haya yawekewe msisitizo ili tuweze kuzalisha hapa nchini badala ya kuagiza nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na niwatakie sana Wizara ya Kilimo utendaji mwema. Ninaunga mkono bajeti hii ya Wizara ya Kilimo kwa asilimia mia moja. (Makofi)