Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo. Pia niungane na Waheshimiwa Wabunge kwanza kwa dhati kabisa kumpongeza Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hasan kwa kuhakikisha kuwa mapinduzi makubwa kwenye sekta ya kilimo yanafanyika; na hii ni sambamba na kuongeza bajeti ya kilimo kwa 324.49%. Niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu maono ya Rais wetu wao wanayasimamia na tunaona mabadiliko. Tunawapongeza sana na hongera sana kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ukuaji wa sekta ya kilimo umeongezeka, tunaona na tunashuhudia. Kwa hiyo tunatarajia na ni matumaini ya Watanzania kwamba mapinduzi haya yako mengine ambayo matunda yake hatuwezi kuyaona moja kwa moja leo, lakini tunatarajia miaka kadhaa ya mbele tuweze kuona haya mapinduzi yanawasaidia Watanzania ambao asilimia kubwa ni wakulima katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nizungumzie wananchi wangu wa Karatu, hasa katika Bonde la Eyasi ambao ni wakulima wa vitunguu. Wakulima hawa; tunafahamu na tunaishukuru Serikali kuna mradi mkubwa pale wa umwagiliaji unaendelea wa shilingi bilioni 21.5; ninatambua kwamba kazi hii inaendelea japo imesuasua kidogo, lakini angalau kuna kazi inaonekana. Kwa hiyo ni matarajio yetu kwamba kazi hii kwa mujibu wa bajeti iliyotengwa itakamilika ili wananchi katika bonde hili la Eyasi waweze kupata uhakika wa kilimo chao; kwa sababu miundombinu yao ya umwagiliaji itakuwa imeimarika kulingana na bajeti iliyotengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo wana changamoto moja. Ninafahamu kuwa si ya Wizara ya Mheshimiwa Waziri moja kwa moja, lakini kwa sababu yeye ni msimamizi wa wakulima nina imani atasaidiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kusimamia hoja ya vifungashio vya hao wakulima wa vitunguu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima hawa wamekuwa wanatumia vifungashio vya kila aina; wana vifungashio vyenye majina tofauti. Kuna kifungashio kinaitwa Net ya Magufuli ambayo ina ujazo wa debe 7.5, kuna Net ya Samia ina ujazo wa debe 8.5 na kuna Net ya Mkenya yenye ujazo wa debe 15. Sasa wananchi wamekuwa wakichanganywa mno; na kila mnunuzi anayekuja na net yake ananunua kwa mahitaji yake, si uhitaji wa soko wakati huo ukoje. Kwa hiyo, imekuwa ikiwaumiza wakulima kwa kiwango kikubwa sana

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Wizara kuwe na vifungashio sahihi vyenye ama ujazo sahihi au turudi kwenye ule utaratibu wa kutumia kipimo cha kilo kwa sababu ninadhani hii ndiyo standard. Kilo moja inapimwa, tunajua mwananchi huyu kwenye kilo moja akichukua ile net inakuwa imeingia kiasi gani cha kilo kwenye net husika. Kwa hiyo, imekuwa ni changamoto ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, tuwasaidie wakulima wetu, hasa hawa wa Bonde la Eyasi. Ukifika pale Bonde la Eyasi anayepanga bei tuna Wakenya kule wamejaa, ndiyo wanaopanga bei, ndiyo wanaoamua soko na ndiyo wanaokwenda mashambani. Kwa namna yoyote; pale na madalali hapo katikati; wanawapangia wakulima. Yaani wanachukua kwa bei wanayotaka wao. Unajua zao la vitunguu linavyolima, yaani linabembelezwa kama mtoto. Ukikosea tu stage moja umeharibu na uwekezaji wake ni mkubwa kwa sababu unahitaji uangalizi wa karibu. Tunaomba sana kwa dhati wakulima hawa wasimamiwe, huu utaratibu wa wanunuzi kwenda mpaka mashambani ukomeshwe, watu wanunue kwa mujibu wa bei iliyopo sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni suala la lumbesa, suala la lumbesa pia, tunaomba wakulima wasaidiwe, wasimamie suala la lumbesa kwa nchi nzima. Tukiweka mkazo upande mmoja wa Bonde la Eyasi kwa wakulima hawa, wanunuzi hawa wanakimbilia upande mwingine. Kwa hiyo ninaomba sana washirikiane na Wizara nyingine ya Kisekta ili wasimamie kukomesha suala la lumbesa kwenye mazao yetu, hasa zao hili la vitunguu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna skimu nyingine muhimu sana ya umwagiliaji, ninadhani hii haifahamiki sana, tunaifahamu zaidi hii ya Bonde la Eyasi, lakini tuna skimu nyingine kwenye Kijiji cha Chemchem katika Kata ya Rhotia, Wilayani Karatu; ni bonde zuri sana. Tunaomba nalo lifikiriwe kutengenezewa miundombinu ya umwagiliaji na skimu bora. Tunajua itawasaidia watu wengi sana kwenye eneo lile kuhakikisha wanazalisha, hasa wanaozalisha mbogamboga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kuwa eneo letu la Karatu ni eneo la kitalii, tuna hoteli nyingi. Tukiwasaidia akinamama hawa na wananchi wa pale, tukawa na skimu watazalisha mboga za kila aina na siyo utaratibu wa sasa kuchukua mboga mbalimbali kutoka Arusha ilihali tuna ardhi inayotosheleza na tuna maeneo. Watusaidie ili tupate skimu ya umwagiliaji katika eneo hili ili kuwakwamua wananchi katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la muhimu. Wilaya ya Karatu pia tuna wakulima wa ngano. Kumekuwa na changamoto ya mbegu za ngano. Mbegu hizi wakati mwingine wananchi wanaletewa na kampuni kubwa kubwa. Kuna hawa wa Breweries wa Serengeti, kila kampuni inaleta mbegu yake, wanakwenda kwa wakulima, wakulima wamepata changamoto mbegu si bora na hazioti kwa wakati. Tunaomba Wizara wasimamie suala hili la ubora wa mbegu ya zao la ngano katika eneo letu la Karatu na katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni kuhusu mbegu ya ruzuku. Tunaipongeza na kuishukuru Serikali kwa utaratibu mpya wa kuweka ruzuku kwenye mbegu zetu za mahindi. Tunaomba; tuimeshuhudia mwaka huu kulikuwa na utaratibu ambao kwa namna moja au nyingine ama wananchi hawakuufahamu au kwa sababu ni utaratibu mpya umekuwa na changamoto. Tunaomba waboreshe zaidi ili hii mbegu ya ruzuku ambayo tunaamini ni nia njema ya Serikali kupitia Mama Samia iweze kunufaisha wananchi wote ambao wana uhitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)