Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia Wizara hii muhimu ya Kilimo. Nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati na pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kubwa katika uboreshaji wa masuala mazima ya kilimo katika nchi yetu, na pia katika Jimbo la Kilolo. (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi sana ambayo yamefanyika ambayo Wanakilolo wanashukuru. Wanakilolo wanashukuru sana kwa ruzuku ya mbolea ambayo inaendelea kutolewa na Serikali hii ambayo imeendelea kupaisha kilimo katika Wilaya ya Kilolo. Pia, tunayo shukurani kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais, pia kwa Mheshimiwa Waziri Bashe, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Wizara nzima kwa ujumla kwa uhusiano mzuri na ushirikiano ambao mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kilolo nimeupata wakati wa kufuatilia mambo magumu ambayo yalikuwepo, lakini Wizara hii ikaweza kuyatatua katika kipindi hiki. Siwezi kutaja mengi, lakini nitaje machache.
 Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri atakumbuka alipokuwa Naibu Waziri, alifika Kilolo pale kwenye Kiwanda cha Chai na kwenye mashamba ambayo yalikuwa yametelekezwa kwa miaka 30. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, baada ya ziara ile ilikuwa ni mwanzo wa safari ya ukombozi kwa Wanakilolo kwenye mustakabali mzima wa masuala ya chai. 
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyozungumza, yule mwekezaji ambaye ni kampuni ya kutoka China ameshakamilisha ujenzi wa kiwanda, kimekamilika, na kiko kwenye majaribio.  Kazi kubwa iliyopo ni Mheshimiwa Waziri mwenyewe na delegation yake, pia na viongozi wengine kufika pale kwa ajili ya uzinduzi wa kiwanda kile kwa ajili ya kazi sasa kuanza kuendelea kutekelezwa. (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya kiwanda kile kazi ndogo iliyobaki kwanza ni ya kuhakikisha kilimo cha chai kinafanyika kwenye eneo lile la hekta 3000 ambazo zipo, zimetengwa baadhi kwa ajili ya BBT, ili kukuza upandaji wa chai ambayo italisha kiwanda kile ili kutosheleza kiwanda. 
Mheshimiwa Naibu Spika, uzuri uliopo kwa kiwanda kile, mwekezaji ni kampuni ya kutoka China. China ni soko kubwa la chai, kwa hiyo, kwa vyovyote vile hatutakuwa na ugumu wa kupata soko kwa sababu mzalishaji mwenyewe ana soko kwenye nchi yake. Najua huo ni mlango hata kwa ajili ya viwanda vingine kwenye nchi hii. Kwa hiyo, ni vizuri kuweka jicho pale kuona pia performance ya hiyo kampuni kwa sababu, nchi yake ina soko kubwa. (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, kuona performance yake ili kuangalia soko la chai kwenye nchi kwa ujumla, tunaweza kunufaika vipi na soko ambalo watakuwa wamelianzisha wao? Kwa hiyo, pia kuna haja ya uzalishaji wa chai ile kuwa bora kwamba inaweza kuvutia wale wateja kwenye nchi hiyo na hapo tutakuwa tumefanya jambo la muhimu sana. (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa kulizungumzia. Mheshimiwa Waziri atakumbuka, nimezungumza naye kuhusu horticulture hasa kwenye kilimo cha matunda na mbogamboga. Ili uchumi wa nchi uweze kukua, lazima ipunguze sana import na iongeze export. Sasa sisi tuna-import sana matunda, tuna-import apple, pears, peaches, lakini matunda hayo yote niliyokutajia yanaweza kuzalishwa vizuri sana kwenye baadhi ya maeneo ya nchi yetu, hasa Kilolo. 
 Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ilikuwa kwamba badala ya kuendelea kutumia miche iliyopo ambayo imezeeka sana ambayo ni ya tangu wakati wa ukoloni ndiyo imepandwa, tuna haja ya kuanza kuleta miche bora kwa ajili ya matunda, na pia kuweka viwanda vya matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji wa matunda tu, uzalishaji wa apple tu, uzalishaji wa peaches tu, uzalishaji wa peas tu, ungeweza kutosheleza mahitaji na hata wakati ambapo inatokea hao watu wanakuwa wakorofi na kufungwa masoko hayo, bado ndani ya nchi tungeweza kujitosheleza. Najua tuna nafasi bado ya kuendelea kuhakikisha kwamba tunakuza soko la horticulture kwenye maeneo yetu. (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, Mheshimiwa Waziri atakumbuka kwamba ili tuweze kufanya vizuri kwenye kilimo, tunahitaji integrated programing, yaani kuhakikisha kwamba kilimo kinaambatana na yale mahitaji muhimu. AGRI-CONNECT ambao ulikuwa ni mradi ambao unahusisha kilimo na miundombinu ulifanikiwa sana hata Kilolo kwa mfano kwa sababu mazao yanayozalishwa yanatakiwa yasafirishwe. 
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama miradi ya kilimo itaambatana na component za usafirishaji, tunakuwa tumefanya jambo la muhimu sana. Kwa kuwa kulikuwa na project ya AGRI-CONNECT ambayo imejenga barabara kwa mfano kutoka Kidabaga kwenda Boma la Ng’ombe na inaendelea ina kilometa saba, lakini ile project ya AGRI-CONNECT inaisha. 
 Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni kwamba ni vizuri kufanya mazungumzo na wale watu ambao wamefanya project ya AGRI-CONNECT kuona namna tunavyoweza kuendeleza miundombinu ya barabara ili wakulima wa maeneo ya pembezoni waendelee kupata mindombinu mizuri ya barabara. AGRI-CONNECT iliimarisha zaidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, lakini yako maeneo ambayo yanahitaji madaraja tu, na yako maeneo ambayo yanahitaji barabara nzuri kwa kiwango cha changarawe tu.
 Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hoja yangu ni kwamba ni vizuri Wizara ikafanya mazungumzo na AGRI-CONNECT kufanya uendelevu wa ujenzi wa miundombinu ya barabara  hasa kwenye maeneo yenye fursa za kilimo kama ambavyo ilifanyika ili huu mradi usiishie pale. Kama utaishia pale, basi kuna maeneo mengi, kwa mfano, Wilaya ya Kilolo ambayo yana fursa kubwa sana za kilimo, lakini kinachotatiza usafirishaji wa mazao, ni barabara ambapo sasa inashusha bei na wakulima wanakosa kupata bei nzuri na kwa hiyo, uendelevu wake unakuwa mgumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kama AGRI-CONNECT au mazungumzo yatafanyika ili kuwa na mradi mwingine wa programming kama ile, hata kama ni wa fedha za ndani, au fedha za nje, ni miradi mizuri sana ambayo itawakuza wakulima kwa sababu hatuwezi kuangalia jambo moja. (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni kuhusu umwagiliaji. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara yake pamoja na Katibu Mkuu kwamba skimu zote kubwa za umwagiliaji za Kilolo zinapata fedha. Skimu ya Ruaha Mbuyuni ameipa shilingi bilioni nne na ujenzi unaendelea, Skimu ya Mgambalenga ameipa fedha japo ujenzi ulisimama, lakini nimetaarifiwa kwamba fedha zimepatikana. Kwa hiyo, wataendelea na ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Skimu ya Nyanzwa wameifanyia usanifu na nimeona kwamba iko kwenye bajeti, itapata fedha kwa ajili ya kuendelezwa. Naomba sana, haya mabonde yaangaliwe kwni yangeweza kusababisha pia uzalishaji wa mazao mbalimbali kukua na wananchi wale kujikomboa kiuchumi hasa kwenye maeneo ya Ruaha Mbuyuni, na Nyanzwa kwa sababu yale ni maeneo makavu, yanahitaji sana kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika kwamba kwenye uwekezaji wa umwagiliaji, kama hayo yatafanyika, basi tutakuwa tumefanya jambo kubwa sana litakalowezesha uzalishaji wa mazao haya uweze kusababisha kufanikiwa kwenye sekta nzima ya umwagiliaji. 
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi skimu nilizozitaja hasa ile ya Ruaha Mbuyuni ina-accommodate wakulima wengi sana, zaidi ya wakulima 10,000, na hao ni wakulima wengi ambao wote wanategemea kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, kutolewa fedha zile shilingi bilioni nne sasa, ni msukumo tu wa yule mkandarasi kuhakikisha kwamba anamaliza kwa wakati, lakini nafahamu, Naibu Waziri anafahamu, pia namshukuru sana Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji pia anafahamu na anafuatilia kwa ukaribu, na hilo ni jambo la muhimu sana. (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kuhusu kilimo cha parachichi. Kwanza naishukuru sana Wizara kwa kujenga kiwanda kwenye Mkoa wa Iringa. Najua kinajengwa Nyororo, lakini ni muhimu sana kwetu Wanakilolo kwa sababu sisi wote pia ndipo tutakapopeleka mazao. Ombi langu ni kwamba ujenzi wa kiwanda kile iende kwa kasi ili Wanakilolo wapate soko zuri, maana kukiwa kuna kiwanda kutakuwa kuna jambo zuri. 
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nimkumbushe Waziri, yeye mwenyewe alifuatilia sana uanzishaji wa kitalu cha miche ya parachichi Kilolo, na TARI walianza kufanya hiyo kazi, na walifanya vizuri sana mwanzoni, lakini baadaye kukawa na kusuasua kidogo. Kile kitalu tukifanya tathmini, kufanikiwa kwake kumekuwa kwa asilimia ndogo. Sasa huku tunakoendelea, issue kubwa ni suala zima la miche. Kwa hiyo, naomba sana na hilo pia tuendelee kuliangalia. (Makofi)
 Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana, Mwenyezi Mungu akubariki. (Makofi)