Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mariam Madalu Nyoka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii adhimu ya kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu ya kilimo. Kwanza nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoipambania Wizara hii ya Kilimo pamoja na wasaidizi wake wote wakiambatana na Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri pamoja na Makatibu Wakuu wao na wasaidizi wao wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba niende kwenye eneo la mafanikio ya Wizara hii ya Kilimo Fungu 43. Mafanikio ya fungu hili ni pamoja na ongezeko la bajeti kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi shilingi trilioni 1.2 mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la 324.4%.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni mafanikio ya kusambaza vitendea kazi kwa maafisa wetu ambao ni maafisa ugani ikiwa ni pamoja na magari, pikipiki, vipima udongo, na mengineyo mengi. Kwenye eneo hili naomba niende kwenye namna ya kuwashauri Maafisa Ugani wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Ugani wetu hawa tunaamini wamepewa vitendea kazi ili wakafanye kazi, lakini nitashauri kwenye maeneo kadhaa. Naomba sasa kwa namna walivyopatiwa usafiri huu, waende vijijini na mashambani wakawasajili wakulima kuliko kukaa madukani kusubiri kuuzia pembejeo kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine wakatoe elimu ya kilimo chenye tija. Eneo lingine waende wakapime afya ya udongo ili waweze kuwashauri wakulima ni zao gani linafaa kwa ardhi hiyo? Eneo lingine waende wakatoe elimu ya mazao kwa namna ya upandaji wenye tija. Pia, waende wakatoe elimu ya uwekaji mbolea kwa wakati sahihi kuliko ilivyo sasa hivi wakulima wanahangaika, kila mkulima anafanya anavyojua yeye, anahangaika ili mradi tu apate mavuno aweze kupata mazao ambayo yataweza kukidhi kibiashara pamoja na familia yake yeye.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini ya kwamba kama Maafisa Ugani wetu wataenda vijijini, wataenda mashambani na wakitoa elimu hii ninaamini sasa wakulima wetu wataweza kupata mazao mengi, mazao yenye tija ili nao waweze kufikia haja ya mioyo yao. Siyo hivyo tu, naomba nishauri ya kwamba kwa sababu Maafisa Ugani wetu tumewapatia vitendea kazi kama pikipiki, naomba basi watengewe bajeti angalau wawe wanapatiwa mafuta hata kwa mwezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Maafisa Ugani hawa wanavyo vitendea kazi vyao, lakini wana-park majumbani na wengine wanazunguka navyo, kama bodaboda kwa sababu wanatafuta hela ya kuweka mafuta, hii siyo sawa. Tunaomba tuangalie Maafisa Ugani wetu ili wakaweze kufanya kazi zao kama tulivyokusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu lingine nitaenda kwenye suala la mbegu bora. Nitaongelea suala la mbegu za alizeti. Tunaona kuna mbegu za alizeti tofauti tofauti zipo, lakini wakulima wengi hasa wa maeneo ya Kiteto wanapendekeza mbegu ya record ambayo inatokea Makutopora ni bora zaidi ukilinganisha na mbegu ambazo zinaitwa Sun Bloom na K-Kwanza. Hizi tunaomba zifanyiwe utafiti zaidi kwani wakulima wengi wamelima kwa kutumia mbegu hizi lakini hakuna walichopata ukilinganisha na record ambayo inapatikana Makutopora.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo lingine ambalo ni mafanikio namba nane ya kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutoka tani 363,599 mwaka 2021/2022 hadi tani 848,884 mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa niwapongeze Wizara hii ya Kilimo kwa kuwa Mkoani kwetu Ruvuma kulikuwa kuna changamoto sana ya namna ya kuifikia hii mbolea kutoka kwa wakulima walioko mashambani na vijijini kwetu, lakini kwa sasa hivi mawakala wamesogea mpaka kule vijijini, mbolea inapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu kuliko ilivyokuwa hapo mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwapongeze Wizara hii kwa namna wanavyofanya kazi kwa ushirikiano wao mkubwa; Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu wao pamoja na wasaidizi wao wote. Yote kwa yote, nawapongeza niwatakie kila la heri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)