Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia bajeti ya kilimo. Kwanza kabisa, naomba nimpongeze Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe, Naibu Waziri na watendaji wote wa wizara hii. Kama kuna kipindi ambacho kilimo kinavutia, ndiyo kipindi hiki cha sasa hivi. Kilimo kilikuwa kimebaki kwa wazee, lakini kupitia BBT na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kilimo, sasa kilimo kinavutia vijana, kinavutia wawekezaji, wasomi wako huko na matajiri. Kwa hiyo, hongereni sana watendaji wa kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, naomba tu mchango wangu moja kwa moja niuelekeze kwenye zile changamoto chache zilizobaki kwa wakulima. Wakulima wadogo ambao ni 90% ya wakulima wote wa nchi hii na ndiyo wazalishaji wakubwa wa chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima kama mkulima vitu ambavyo viko karibu naye ni pembejeo za kilimo na masoko ya mazao yake. Kwenye pembejeo ya kilimo kwa maana ya mbegu, mbolea na viuatilifu, changamoto ni upatikanaji wa pembejeo, bei pamoja na ubora, kwa sababu wakulima bado sehemu nyingine wanakutana na pembejeo feki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika upatikanaji wa pembejeo za kilimo, tunaishukuru Serikali, kwa kweli wameliona hilo, wameweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo. Tulianza na mbolea muda uliopita na mbolea tumefanya vizuri. Msimu uliopita ruzuku imewekwa kwenye mbegu, sasa hili jambo bado limeleta changamoto kwa wakulima kwa sababu upatikanaji ndiyo umezidi kuwa mgumu kwa sababu ya bureaucracy ya makampuni fulani ambayo mbegu hizi za ruzuku wanatoa kwa mawakala wachache sana pale wilayani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utashangaa kwamba kwenye wilaya moja pembejeo za ruzuku zitapatikana kwa wakala mmoja, watakaa kwenye foleni. Mahali pengine mtandao unasumbua. Hii imeleta adha kubwa sana kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, yote makubwa ameyaweza; hili nalo analiweza. Naomba pembejeo za kilimo ziende kwa mawakala wale wa chini kabisa ambao wako karibu na wakulima. Tena zipatikane kabla ya muda wa msimu wa kilimo, lakini kwa changamoto ya bei kubwa, tunazalisha sasa hivi mbegu kwa 60%. Nami naiomba kabisa Serikali yangu sikivu, tuendelee kuongeza bajeti kwenye uzalishaji wa mbegu ili sasa tujitosheleze kwa uzalishaji wa mbegu na ziada, tuweze kuziuza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni kwenye maghala. Maghala haya kwa utaratibu wa stakabadhi wa mazao ghalani, kama kuna sehemu wakulima wamepata bei nzuri kidogo ya mazao yao, ni kupitia stakabadhi ya mazao ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzoni walikuwa hawajaelewa, lakini toka wameelewa Stakabadhi ya Mazao Ghalani imesaidia sana wakulima mazao yao yamepata bei nzuri, lakini wamepata taarifa za masoko. Sasa haya maghala yajengwe vijijini na kwenye kata; na kuna maghala ambayo yalishakuwepo yakarabatiwe ili sasa Stakabadhi ya Mazao Ghalani na mazao yote yaingie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona sehemu nyingine watu binafsi wana maghala yao na wananunua mazao ya wakulima kupitia Stakabadhi ya Mazao Ghalani. Jambo hili ni jema liendelee kuwepo kila sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni kuhusu huduma za ugani, tumeomba sana upatikane uwakala wa Maafisa Ugani. Vinginevyo uwekezaji mkubwa sana tunaoweka kwenye kilimo utakuwa hauna maana kama tutashindwa kuboresha hali ya Maafisa Ugani; na katika kuboresha tumeomba wawe na wakala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji huu mkubwa tunaoweka, kwa mfano kwenye miradi ya umwagiliaji, kama kwenye skimu hapatakuwepo Afisa Kilimo atakayeshauri kuzalisha kwa utaalamu, na atakayeangalia miundombinu ikiwepo mifuko ya ukarabaki, basi kipato pale kitakuwa kidogo na uwekezaji huu mkubwa utakuwa hauna sababu. Sasa ili Maafisa Kilimo waweze kufanya vizuri, tunaomba Serikali iharakishe upatikanaji wa Maafisa Ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango mwingine ni kuhusu centre hizi za Agro mechanisation. Naipongeza Serikali, wamenunua trekta za kutosha pamoja na power tiller. Sasa hivi ni kipindi cha kutoka kwenye kilimo cha jembe la mkono. Zilikuwepo power tiller ambapo watu walikopa kipindi kile cha Kilimo Kwanza, kwa sababu teknolojia hii ni mpya, zimekufa, hawajui pakupata spare parts, na hawana taaluma za kuendesha. Kwa hiyo, tutakavyokuwa na hizi Agro mechanisation centre angalau kubwa kwa kila wilaya, na kule kwenye kata, tuendelee kuboresha world resource centre sehemu ambazo watu watapata taaluma kwa urahisi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, hii iende ili kilimo chetu kiendelee kuwa bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine, naipongeza Serikali kwa kuanzisha Benki ya Ushirika, hongera sana. Hii benki inaweza ikawa mkombozi kwa wakulima. Hii benki sasa ipewe fedha. Kama inapewa fedha na Benki Kuu, ikopeshe wakulima kwa sababu wakulima ni kikundi ambacho walikuwa hawakopesheki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Rahhi, nawe ni mkulima mzuri.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)