Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa dhati kabisa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nina kila sababu ya kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu kuu moja ya utashi wake wa kisiasa kuwekeza fedha nyingi kwenye sekta hii muhimu ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona ongezeko la bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022 bajeti ilikuwa shilingi bilioni 294, lakini kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bajeti imekua na kufika shilingi trilioni 1.248. Jambo hili ni kubwa na ndiyo maana nikasema nampongeza Mheshimiwa Rais anavyowekeza fedha nyingi kwenye sekta ya kilimo, sekta pekee inayotoa ajira kwa Watanzania walio wengi. Maana yake ni nini? Anawagusa kwa asilimia kubwa Watanzania, watu wazima, vijana na itoshe tu kusema sasa hivi wamesema wengine, vijana wamehamasika sana na kilimo kwa sababu wameona kina tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru Mheshimiwa Waziri, Bashe na Naibu wake pamoja na Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii. Hapa nirejee mafundisho ya hadithi muhimu ya Mtume Muhamad, anasema haya kwa Waislam, “Hubra twani minal iman” maana yake nini? Anasisitiza habari ya uzalendo. Anasema, “Kuipenda nchi yako ni sehemu ya Imani.”

Mheshimiwa Naibu Spika, hakika Mheshimiwa Bashe ni mzalendo na anafuata mawaidha ya Mtume Muhamad. Kwa hilo tu, itoshe kusema Mungu atambariki. Nasi vijana, wadogo zake tunamuunga mkono kwa kuwa tumeona ana maono na hatutamwangusha. Tunajua nia yake ni njema na uwezo wake tunaujua. Apige kazi, sisi tupo tutamuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, mimi nijielekeze kwenye eneo la kilimo cha umwagiliaji. Kama kuna mambo ambayo Taifa letu na Mheshimiwa Bashe utaweka alama na unaenda kutengeneza na Mheshimiwa Rais anakwenda kutengeneza historia katika Taifa letu, kwa muda mrefu sana Watanzania tunasema tunazalisha, lakini bado kilimo chetu tunatumia kilimo cha kutegemea mvua ambacho siyo kilimo cha uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona fedha nyingi zinakwenda kuwekezwa kwenye kilimo cha umwagiliaji, mathalani, pale Mlimba nimeona utashi wa Serikali kuwekeza kwenye umwagiliaji katika Bonde la Mto Kilombero, hekta takribani 53,000 usanifu unaambiwa umekamilika, lakini katika hili nadhani tumechelewa na siyo Mheshimiwa bash, yeye ameikuta Wizara katikati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme tu kwamba kama kuna eneo ambalo linakwenda kulisha Taifa letu, ni Mkoa wa Morogoro. Labda nitoe mfano pale Mlimba sisi tunazalisha mchele kwa mwaka tani 400,000; na nchi nzima sasa hivi mchele unazalishwa metric tone milioni 3.046. Maana yake 400,000 zinatoka Mlimba kwa kilimo cha kutegemea mvua. Hatuna umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa uwekezaji wa kilimo cha umwagiliaji Mlimba, maana yake nini? Tutakwenda kuleta tija kubwa kwenye zao hili la nini? La mchele. Labda niseme tu, duniani kote, katika idadi ya watu duniani takribani bilioni nane, bilioni 3.5 wanakula mchele na chakula cha kwanza duniani kwa kuliwa watu walio wengi ni ngano, na cha pili ni mchele. Tuwekeze kwenye zao la mchele. Nami nasema tu, tukiwa na surplus tutapata fedha za kigeni kupitia mchele.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee eneo lingine la Mradi wa BBT. Mwanzoni ilikuwa kama sielewielewi hivi, lakini sasa nimejifunza mengi. Kaka yangu Mheshimiwa Bashe mwanzoni ilinipa shida kidogo lakini nikueleze kwa dhati, sasa nimeona dhamira yako ilivyo njema, lakini nikuombe sasa nataka nifanye polishing tu kidogo. Sasa hivi nikuombe njoo pale Mlimba nenda kwa wale vijana kule wanaofanya kazi ya kilimo. Usiishie tu kwenye maeneo haya, maeneo yote siyo tu Mlimba, uende Mbeya, uende Iringa, uende Njombe na najua mpango huo unao, lakini nataka tu uende haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, twende pale Mlimba tukapate takwimu ya vijana wanaofanya kilimo cha zao la mpunga. Tujue wako wangapi pale? Tuwaulize changamoto zao ni nini? Watakwambia, “Eneo langu mimi ni dogo, ukinipa ekari 10 nitaongeza kipato”, atakwambia, “Mimi pembejeo ni changamoto”, na atakwambia, “Mimi pembejeo na masoko.” Sasa haya yote utayapata kule na kwa sababu wewe una passion, uwekezaji wako ni mdogo sana kama kumsukuma mlevi kwenye mteremko.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo,...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nihitimishe kwa kusema, zao la Cocoa Mheshimiwa Bashe tusaidie, Kata ya Michenga na Kata ya Mbingu wewe unafanya jitihada kubwa kuhakikisha unahamasisha zao la Cocoa lakini wenzako wanakata mi-cocoa, na hili naomba ulitolee maelezo hapa. Tuna changamoto Michenga na tuna changamoto pale Mbingu Fuatiwa.

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Kunambi.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wamejenga ule upande wa Cocoa lakini zinafyekwa, ahsante. (Makofi)