Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba niungane na wenzangu kumshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika eneo hili la kilimo. Nitaanza kwa eneo hili la ruzuku. Kwa upande wa ruzuku tunashukuru sana. Hili neno ruzuku ni terminology, lakini maana yake kubwa kwa wakulima ni kwamba Serikali anayoiongoza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inamlipia bei mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya mbolea kabla ya ruzuku ilifika shilingi 130,000 lakini leo tunanunua mfuko shilingi 53,000. Tumelipiwa karibu shilingi 77 Serikali imelipia wananchi. Maana yake ni nini? Tunapozungumza uchumi umekua, basi rasilimali fedha tunazozipata za ukuaji wa uchumi, Mheshimiwa Rais Samia aliridhia zigawanywe kwa wananchi wa kawaida kuwalipia mbolea kwenye mfumo huu wa ruzuku. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunamshukuru sana kwa kufungua masoko. Alipokuwa anasema anaifungua nchi, vilevile alikuwa anafungua masoko ya kilimo. Leo hii ametufungulia masoko ya kilimo. Kwa ajili ya muda, nitatolea mfano moja tu, zao la mbaazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaazi sisi kwetu kule ilikuwa ni mboga, ilikuwa ilifikia mpaka kuuzwa shilingi 100 kwa kilo moja. Kilo 130, lile gunia kubwa lile lumbesa au sisi kwetu tunaliita mbandanga lenye kilo 130 lilikuwa linauzwa shilingi 13,000 ambayo hata bati moja ulikuwa hupati, lakini leo hii gunia hilo linauzwa mpaka shilingi 222,000. Una uwezo wa kununua bati 10. Kilo moja, shilingi 1,710 tuliuza mwaka 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, zao hili la mbaazi tunaposema kwamba limefanya vizuri, na Wizara ya Kilimo mmelisimamia vizuri, ndipo tunapomsifia Mheshimiwa Bashe amefanya vizuri. Hatumsifii, kwa sababu leo kuna mahali nimesikia kwamba wanasema Wabunge kazi yao kumsifia tu Mheshimiwa Bashe kwenye hotuba hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie, hatumsifii Mheshimiwa Bashe kwa sababu ya uzuri wa suti yake aliyoivaa, wala hatumsifii Mheshimiwa Bashe kwa sababu ya urefu wake au u-handsome wake, tunamsifia kwa sababu ya uwezo wake alionao anaosimamia sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo katika sekta hii, eneo hili moja la mbaazi sisi tulikuwa tunauza. Mwaka 2022 tulizalisha tani 3,000 tukauza shilingi 2,536,000,000 lakini mwaka 2023 tukazalisha tani 4,000 tukauza shilingi 9,267,000,000; hizi zilikuwa take home walipata wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2024 tuliuza tani 8,000 kwa shilingi 15,345,000,000. Kwa hiyo, maana yake ni nini? Mmeisimamia sekta hii vizuri sana na mmeisimamia Wizara hii vizuri sana katika eneo hili la mbaazi katika huu Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie wenzangu wenye wasiwasi na huu Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, mfumo huu umefanya kazi vizuri sana; na kupanda kwa uzalishaji na bei kwa wakulima wetu kule Namtumbo kumetokana na huu Mfumo wa Stakabadhi Ghalani na hasa pia mfumo mliouweka wa TMX. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wizara nzima na taasisi zenu mnazozisimamia katika eneo letu hili la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo la umwagiliaji kutokana na muda. Sisi Namtumbo tuna hekta 17,322 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini tunachoweza sasa hivi, kulima ni hekta 1,680 na katika maeneo haya mengi hayana mfumo sahihi au ni kama tumejengewa mfumo wa umwagiliaji.
Mheshimiwa Waziri, nitaomba kupitia Wizara yako mtusaidie, tuna mradi pale wa kienyeji katika Mto Nahange Mtakuja, ambao una hekta 300, lakini hauna mifumo na miundombinu ya umwagiliaji maji. Tuna Mwangaza Limamu hekta 250.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kawawa ahsante.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba sana mtusaidie ili tuweze kufanya katika eneo hili la umwagiliaji, ahsante sana.