Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Bashe, Naibu wake na timu yake ya Wizara ya Kilimo kwa kutuletea bajeti ambayo kwa kweli inakwenda kutuletea mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo. 
Mheshimiwa naibu Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mwanamapinduzi wa kweli katika kuhakikisha kwamba, anakwenda kuimarisha sekta ya kilimo kwa kwenda kuleta matokeo chanya katika nchi yetu. Tuendelee kumtakia heri na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza ndugu zetu wa TARI kwa kazi nzuri wanayotufanyia ya kuhakikisha kwamba, wanaendelea kufanya tafiti, lakini tuwashukuru wale wanaoendelea kutuzalishia mbegu ambazo zinakwenda kutuletea matokeo chanya ya uzalishaji uliokuwa bora na hatimaye kuleta ustawi wa wananchi wetu kwa maana ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Bashe nakushukuru sana, ulitusimamia kwa sababu nilikueleza changamoto kubwa ya kilimo cha minazi ambayo ilipatwa na ugonjwa na kuendelea kuathirika, na sasa umetuletea mbegu mpya ya minazi na tumepokea, wakulima wa Lindi Mjini wamepata miche ya minazi bure na tunaendeleza zao la minazi. 
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana pamoja na kwamba, bado mgao utaendelea awamu ya pili na ya tatu, tunataka kuondoa mashamba pori yote ili tuhakikishe kwamba tunaiendeleza minazi katika eneo letu la Lindi Mjini. Kwa asilimia kubwa eneo lile tunalima sana minazi, kwa hiyo, kiwango cha ulimaji wa mikorosho ni kidogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri wetu kwa kuhakikisha kwamba changamoto nyingi za wakulima wa korosho amesimamia na zimepungua. Wakulima wa korosho kila siku tukikutana kwenye vikao mbalimbali wanatamani arudi tena na awe Waziri wa Kilimo, auendelee kusimamia sekta ya kilimo kuhakikisha kwamba tunaendelea kukuza sekta ya kilimo. Kwa hakika ameitendea haki Wizara hii ya Kilimo. Tunaendelea kumwombea kila la heri, Mungu amrudishe tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana SWISS Aid, wametupa mafunzo mbalimbali pale Lindi. Pia tunashukuru kwamba, tumefungua benki ya kuhifadhi mbegu za asili na kuendeleza kilimo cha asili ambacho tumekirithi. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri, tuhakikishe kwamba tunawapa support kubwa kwa sababu kazi wanayoifanya ni nzuri, inatuletea matokeo mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, nimempelekea mwekezaji katika Wizara yake. Mwekezaji huyo anakuja kuwekeza Lindi katika kilimo cha agrihood. Sisi wananchi wa Lindi tunaomba Waziri ampokee na ampe support kubwa kwa sababu anakuja kubadilisha maisha ya wananchi wa Lindi kuelekea kukuza uchumi katika eneo letu la Lindi Mjini. 
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kumtakia kila la heri, Mheshimiwa Waziri. Pia naomba Wizara ya Fedha ihakikishe kwamba wanatoa fedha kama ambavyo bajeti inasema katika Wizara hii ya Kilimo kwa sababu kuna mambo mengi mazuri ambayo tunayategemea kwamba yataleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika nchi yetu. Kubwa ni kuhakikisha kwamba, fedha zilizotengwa zinakwenda kwa wakati ili Mheshimiwa Waziri Bashe pamoja na wenzake waweze kutekeleza mipango ambayo wametuletea katika bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)