Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nami niendelee kuwashukuru na kuwapongeza sana viongozi wetu ambao wanatuongoza kwenye sekta hii, Waziri Mheshimiwa Bashe, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wote wanaoshiriki. Kwa kweli tunawapongeza sana, lakini tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ameweka kipaumbele kwenye kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nizungumze kidogo kwenye maneno yako uliyoyazungumza wakati amemaliza Mheshimiwa Kunambi juu ya zao la kokoa. Ni kweli zao la kokoa na hasa kokoa ya Kyela ni zao ambalo linapendwa sana duniani na ni zao ambalo ni organic na kwa Kyela unaambiwa ile ndiyo kokoa bora duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumefikia mahali pazuri, tunaenda vizuri, lakini bado nina wasiwasi sana. Wasiwasi wangu ni juu ya uendelezaji wa zao hili katika kuhakikisha haya mazao yetu yanakuwa endelevu na hasa kwa jambo la quality na quantity kwa sababu maeneo yetu ni madogo, lakini pamoja na kwamba maeneo yetu ni madogo, bado hakuna mkakati maalum wa kuliendeleza hili zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara na Serikali ianzishe mkakati maalum wa kuendeleza zao hili pale Kyela. Naishauri Serikali, tuko na vijana wazuri sana pale Kyela ambao wamesoma, wanaelewa lile zao toka wako watoto mpaka sasa na wana uwezo wa kuisaidia Serikali kuhakikisha Extension Officers wanafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo nyuma kabla ya kuja Stakabadhi Ghalani, zao letu lilikuwa linaendeshwa na makampuni. Haya makampuni yaliweza kusaidia sana kuleta wataalam wazuri ambao walisaidia sana uendelevu wa zao hili, lakini bado tuna tatizo kwa sababu imeshatokea sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili zao linakimbiliwa na imekuwa ni biashara. Uvundikaji wa zao hili kwenye quality, nataka niseme tutafika wakati tutapoteza hii sifa tuliyonayo. Naomba sana tulisimamie hili, nami najua Serikali ni sikivu na tuko na Mawaziri ambao ni wasikivu, tutafanya vizuri katika hili, sina wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, maeneo yetu ni madogo sana Tanzania, pamoja na kwamba yapo maeneo ambayo ni makubwa, lakini maeneo ambayo yanaweza yakatoa zao la mpunga ambalo ni bora ni Kyela. Kyela tuna maeneo machache na ni eneo dogo. Pamoja na kwamba, ni eneo dogo tumesema hapa sasa hivi tunachokiangalia ni kuzalisha kwenye eneo dogo mazao mengi, na ili ufikie hapo ni lazima tuingie kwenye irrigation.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri atakapomaliza ile skimu yangu ya bilioni 21 ya Makware ambayo Serikali imewekeza fedha nyingi, naipongeza na nampongeza Mheshimiwa Rais. Naomba sana, hebu tuziangalie skimu nyingine ambazo zipo. Kwa mfano, tuna Skimu ya Ngana, kuna Skimu ya Kingiri, yaani hayo ni mabonde ambayo yanafaa kumwagilia. Kuna Ikumbilo, Mwaigoga, Mabunga, Ikama, Kabanga, Katumbasongwe, Tenende na Mwambuzye.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, tukiweka skimu kwenye maeneo haya, tutajuta ni kwa nini hatukufanya mapema. Naipongeza Serikali na ninawapongeza viongozi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)