Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa. Leo tarehe 22 Mei, 2025 katika Wizara hii ya Kilimo naomba nami niwe miongoni mwa wachangiaji kwenye bajeti hii, ambayo kimsingi inagharimu pesa za Kitanzania, kwa makadirio yake ni shilingi trilioni 1.2 na ushee. Naomba nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ya kutukuka katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika nitumie nafasi hii kumpongeza sana Waziri mwenye dhamana kwa kazi nzuri anayoifanya, yeye pamoja na Naibu Waziri wake na delegation yake yote. Taasisi zote ambazo zina Wakurugenzi, kongole nyingi sana kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niseme, Mheshimiwa Bashe mimi huwa nataka nikufananishe na mtu mmoja ambaye ni kiongozi mahiri sana, mzalendo, kiongozi kijana, naye sio mwingine ni Kepteni Ibrahim Traore, Rais wa Burkina Faso. Traore ni Rais ambaye amefanya mageuzi makubwa sana katika nchi yake. Nataka nikwambie Mheshimiwa Bashe, utaenda mbali kwa sababu una uwezo mkubwa, una uwezo wa kufanya maamuzi, na huyo Naibu Waziri wako pia ninamfananisha kwamba angekuwa Naibu wako kama alivyo Rais Traore wewe ninavyokufananisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii sasa kuzungumza kwenye suala la mahindi. Mheshimiwa Bashe unafanya kazi nzuri sana, nawe umekuwa kipenzi cha wakulima, lakini naomba kwenye suala la zao la mahindi bado kila mwaka unatuwekea pesa shilingi 700 katika kitengo cha NFRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Bashe, uzalishaji wa mahindi kila mwaka unaongezeka, gharama zinaongezeka, gharama za kulima, gharama za kupalilia, gharama za kutia mbolea, gharama za kila kitu zinaongezeka, lakini iweje ni mfululizo wa miaka mitatu sasa bei ameweka ni shilingi 700 tu? Kila mwaka shilingi 700, kila mwaka shilingi 700! Tunaomba sasa kwa sifa hizo tunazompa, na kwa upendo wake kwa wakulima, aje alete bei nyingine. Ungeniambia leo nipendekeze bei gani? Ningekwambia lete bei ya shilingi 900 kwa wakulima wangu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kilo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Bashe inawezekana, kwa sababu wewe una uwezo mkubwa na una mapenzi na mahaba makubwa sana kwa wakulima wetu wa mazao haya ya nafaka ambayo yanalimwa sana katika Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nafahamu Mheshimiwa Bashe ni mbunifu sana amefanya vitu vingi, lakini naangalia kwenye suala la majanga na mabadiliko ya tabianchi wamejipangaje Wizara kwa ajili ya kuweka mkakati mzuri dhidi ya suala la kumkomboa mkulima pindi inapotokea majanga? Kwa mfano, mwaka huu, chupuchupu tukose mazao. Tumepata mazao kidogo kutokana na hali ya mabadiliko ya tabianchi, mvua zimenyesha kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fulani ilitokea jua linawaka sana baadhi ya mashamba yamekauka, je, mmetoa elimu kwa wakulima ili waweze kutambua umuhimu wa bima katika kilimo chao ili waweze kukata bima? Naomba sasa Wizara yako iende na mkakati wa kwamba, wakulima waende wakapate elimu ili waweze kupata bima kwa ajili ya mazao yao, ili pindi inapotokea majanga, basi wasijikute wanyonge, waweze kupata fidia kupitia bima ya mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la Hazina. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nakuomba sana, peleka pesa kama mvua kwenye Wizara ya Kilimo ili miujiza hii tuendelee kuitunza; miujiza hii ambayo inaendelea kutokea katika sekta ya kilimo. Ni sekta muhimu sana na kwa sababu tuna malengo ya kulisha dunia hii, bila kupeleka fedha hakuna muujiza wowote utakaotokea. Peleka fedha Mheshimiwa Bashe a-relax, afanye kazi vizuri. Ongeza mazao katika nchi yetu na tupeleke mazao mpaka nje ya nchi huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la kiwanda. Tumekuwa wazalishaji katika Mkoa wa Ruvuma zaidi ya miongo mitano, tunashika nafasi ya kwanza katika uzalishaji wa mazao ya nafaka. Kwa hiyo, tunapofanya vizuri namna hiyo, tunastahili kupata zawadi ya kujengewa kiwanda cha mbolea pale, kwa sababu sisi ndio wazalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua Mheshimiwa Bashe hakuna anachokishindwa, tena ananikonyeza hapa anachekelea kabisa, inawezekana Mheshimiwa Bashe. Tuwekee kiwanda cha mbolea pale ili sisi kazi yetu iwe ni kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo, inawezekana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni suala la kilimo mseto.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msongozi.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo mesto…, namalizia wewe ni rafiki yangu sana. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo mseto…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msongozi tunakwenda kwa time, ukichukua time na leo mko wengi sana humu ndani na wote ni wakulima, na kila mtu anataka kuchangia, nikuombe tu ukae.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)