Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kuunga mkono hoja. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa mpango huu wa ruzuku. Hapa kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kwani amekuwa mshauri mzuri wa Rais kwa kuendelea kumshauri vizuri mpango huu wa ruzuku na sasa ni miaka mitatu mfululizo imeendelea kutolewa ruzuku ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mbinga bila mbolea hatuvuni. Kwa maana hiyo, bei ya mbolea ilipokuwa juu tulikuwa tuna mashaka sana ya namna ya kilimo chetu, lakini nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, umekuwa na mikakati mizuri na ushauri mzuri kwa Mheshimiwa Rais, juu ya mbolea hizi za ruzuku na sasa mbolea inapatikana vizuri Mbinga. Wananchi wa Mbinga wanapata mbolea, wanalima na wanavuna vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale katikati kidogo tulipata shida ya mbolea, lakini nashukuru kupitia kiwanda cha ndani ambao ulikuwa mkakati wa Mheshimiwa Waziri wa kufanya Tanzania tuwe na kiwanda cha ndani cha mbolea. Tunacho kiwanda hiki hapa cha ITRACOM, kina mbolea zile za otesha, pandisha, za aina karibu tatu, nne hivi; zilitusaidia sana zile mbolea pale ambapo mbolea nyingine zile za chumvichumvi zilipoonekana kupungua, tuliziweka zile.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, shida iliyopo ni uelewa wa watu kwa sababu mbolea ni zile zile. Sifa ya hii mbolea, tunaambiwa, pamoja na kunenepesha mmea, lakini inaenda pia mpaka kwenye nini? Kwenye udongo. Kwa hiyo, elimu ikitolewa kwa wananchi, huko watakuwa wanunuzi wazuri wa mbolea hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaambiwa sasa hivi hiki kiwanda kina uwezo mkubwa, kina uwezo wa kuzalisha hadi tani 600,000 na kina uwezo mkubwa zaidi ya tani 600,000 na sisi matumizi yetu sasa hivi ndio yamefika 800,000 mpaka 900,000 hapo. Kwa hiyo, kumbe tuna uwezo mkubwa. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, amefanya kazi nzuri na leo hii wananchi wa Mbinga wanakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimeambiwa hapa kuna madeni kwenye hiki kiwanda, sasa naomba kilipe. Tunajua taasisi nyingi hapo katikati zilipata shida. Zilianza vizuri kwa nguvu nzuri lakini mwisho wa siku zikadidimia kwa sababu ya madeni. Sasa hivi hiki kiwanda kinadai zaidi ya bilioni 11. Kwa kweli kilipeni kiende kufanya kazi nzuri, wananchi wetu wasipate shida tena ya mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, ambalo nampongeza Mheshimiwa Waziri, ni suala la ujenzi wa maghala. Mwaka 2024 Mheshimiwa Waziri alifanya ziara Wilayani Mbinga, akakuta ukusanyaji mkubwa wa mazao, na mazao yametapakaa karibu kila kona. Alituahidi ataenda kujenga maghala. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, nimepata taarifa zaidi ya shilingi milioni 109 zimeshatolewa, eneo limenunuliwa na tayari maandalizi yako vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri aje atuambie, ni lini anaenda kujenga yale maghala? Wananchi wale wangependa mwaka huu 2025 au mwakani 2026 waanze kutumia yale maghala.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna Mheshimiwa Waziri alivyosema, najua atayajenga mapema iwezekanavyo, ikiwemo pia na wale wananchi wa kiwanda kile cha kukoboa kahawa na wenyewe walikuja wakamwona, najua amewapa ahadi nzuri kwamba ujenzi wa maghala ya kahawa utaenda sambamba na ujenzi ule wa maghala ya mahindi. Kwa hiyo, tunamshukuru na tunaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita, ikitamka inatekeleza. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2024 huo huo Mheshimiwa Waziri alituma timu pale Jimboni kupokea matatizo na changamoto za wakulima wa kahawa. Walikaa pale zaidi ya mwezi mmoja wakaja wakampatia andiko Mheshimiwa Waziri na akaitisha kikao cha wadau wa kahawa. Kwenye kikao kile Waziri alitoa maelekezo kuwaambia wadau wa kahawa wakae wajipange kisaikolojia. Anaenda kufanya reform kubwa ya kahawa ya namna ya mfumo wenyewe wa kahawa wa mauzo na mambo mengine yote yanayohusiana na kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, amefanya vizuri sana kwenye korosho na amefanya vizuri sana kwenye kahawa huko upande wa robusta, wakulima sasa hivi hawana kelele. Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara pale Jimboni kuna maelekezo pia alitoa na hata hapa wakati anawasilisha bajeti yake kuna maelekezo alitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, yuko mtu mmoja kule sasa hivi anapita na uongo mdomoni, anazurura pale Jimboni anapita na uongo mdomoni anasema uongo, anatamka maneno kwamba umeyasema wewe. Maneno umeyatoa wewe kama Serikali kurekebisha mfumo wa malipo ya kahawa, kurekebisha mfumo wa zao la kahawa na watu namna gani wanaenda kukopa mbolea...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kapinga, ahsante kwa mchango mzuri, mengine mwandikie Mheshimiwa Waziri.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri, tolea ufafanuzi hilo. Ni nini mlichokifanya? Nini ulichoelekeza; na nini kinachofanyika pale Mbinga Vijijini? Ahsante sana. (Makofi)