Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
							Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, na ni bahati iliyo njema kupata hizi dakika tano za kuchangia Wizara nyeti ya Kilimo na huwezi kuzungumza kilimo bila kuzungumza Mkoa wa Morogoro. Mheshimiwa Naibu Spika umefika kwetu, umefika kwenye kiwanda cha sukari na umejionea sisi tulivyokuwa wakulima wazuri. 
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yote yaliyosemwa na Wizara hapa yapo katika namna mbili; kusaidia nchi yetu kujitegemea kwa chakula ambapo sasa hivi tunajitegemea kwa 130% na pili tuuze mazao ya mwisho nje ya nchi yetu tuweze kupata fedha za kigeni. Mimi ni Mswahili, na Waswahili wanasema, njia rahisi ya kuleta umaskini ni kuuza malighafi badala ya kuuza ile final product. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza kwa namna mbili; kwa furaha na kupendezwa kwa maana Kiswahili ni chata na tamwa, na pia nitazungumza kwa chona na kibubuti (kwa masikitiko) kule mwishoni endapo muda wangu utafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa furaha nataka kusema wazi kwamba nina furaha isiyo kifani kwa viongozi wote wa hii Wizara na Wakurugenzi wote. Ningetaja taasisi zote, lakini muda hautoshi.
Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wenzako wote na Mheshimiwa Rais amempongeza mpaka Katibu Mkuu wako kwamba alikuwa anaonekana kama kijana kijana, akipiga suti yake hivi, unaweza ukamdharau ukasema kijana wa mjini, lakini Katibu Mkuu ni mtu muhimu sana katika Wizara yenu, na ni engine kubwa ya Wizara. Mkurugenzi wa COPRA, nimeona COPRA imeshaanza kuwasiliana wasiliana na sisi kuhusu mpunga ili tuuze mazao kidigitali, na tunaomba zao la mpunga ikibidi baadaye liende katika mambo ya kidigitali ya Stakabadhi Ghalani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TFRA imesajili wakulima 4,500,000 na wakulima wangu wamepewa vishikwambi, ninashukuru sana. Kiwanda kipya cha sukari Mheshimiwa Waziri amekiona tunakushukuru sana, pia tunashukuru kwa kikao chake cha AMCOS, tunashukuru kwa upembuzi yakinifu wa Bonde, amesema pia Mheshimiwa Kunambi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bonde la Kilombero litatusaidia mabwawa manne ambayo yatasaidia ku-control mafuriko. Tunashukuru kwa mbolea za ruzuku na tunashukuru kwa kitalu cha mbegu KATRIN. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba Mheshimiwa Waziri Chuo cha KATRIN kwa maana ya Kilombero Agricultural Training and Research Institute kibaki kama chuo wakati mambo mengine yanaendelea kwa sababu sisi kwenye bonde tuna mkakati mkubwa. Serikali imeshawekeza mabweni pale wanafunzi walale pale. Sasa tukibadilisha, tukifanya kikiwa ni sehemu ya kuahirisha teknolojia, itakuwa tumeondoa nafasi kubwa ambayo wenzetu waliyaona huko nyuma. Naomba katika vyuo vitano vilivyobaki uongeze na hicho cha KATRIN kama cha sita kibaki kama chuo. 
Mheshimiwa Waziri Bashe mimi nilikuwa ninakuona wakati unasoma Hotuba hapa umesimama, unainama, umesimama; nikasema hee, sasa nikajiuliza, siku moja ukiwa haupo kwenye hii Wizara itakuwa namna gani? Mheshimiwa Bashe andika kitabu, rekodini Youtube, elezeni mipango na idara zote zinazowakabili. Katika dunia ya sasa hivi, tuone kuna leo na kesho katika mambo haya. Tunakuomba sana, andika vitabu. 
Mheshimiwa Naibu Spika, hakika kuandika kitabu ni kugoma kufa hata baada ya kufariki. Namwomba Mheshimiwa Waziri jambo la kwanza tunataka kufanya semina kwa wakulima wetu, tusaidiwe; pili, yale matrekta tuletewe mgao; na ya tatu, tusaidiwe haya mabwawa haraka ili tuweze kupata mafuriko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkurugenzi wa Umwagiliaji amekuja kule kwetu mara kadhaa, tunaomba sana atusaidie katika mambo ya umwagiliaji kwa sababu kama mvua zisingechelewa mwaka huu kwenye mpunga, tungepata hasara kubwa sana. 
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atembelee Kiwanda cha Mang’ula Machine Tools, kina majengo, kina hekta 200, kimekaa pale zaidi ya miaka 20, kinakufa na watu wa viwanda wameshindwa kukifufua. Naomba aweke mwekezaji pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa ufupi, naongea kwa chonda na kibubuti (sikitiko) mambo mawili. Kwanza la miwa, kwa sababu wakulima wangu wako hapa sasa hivi wananitazama. Suala la 10% nimempatia Mheshimiwa Waziri. Nimempelekea barua kwamba juzi AMCOS zote 17 ziligoma kuendeleza kwenye kikao cha Kiwanda cha Ilovu kwa sababu walikatwa pesa zao 10% na hawajapewa pesa zao. Mheshimiwa Waziri, ninakuomba nitaunga mkono hoja kwa masikitiko lakini naomba ulisemee jambo hili, kwani wanaangalia television huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima anapouza mua anakatwa pesa. Wakati msimu unaanza, wanataka kuchukua ile 10%, anaambiwa hawezi kupewa. Ni balaa huko sasa hivi ninavyokwambia, wako kwenye TV wanasubiria kuona hali hii. Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana nisaidie sana chonde chonde nisaidie. Prof. Bengesi ukimtazama unaona anapenda kilimo cha mua, lakini kuna saa anaona kama mambo magumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Prof. Bengesi alikuja kule wakati mua unaungua moto, tukaenda mpaka porini. Ni mtu mzuri sana na mtu anayetusaidia sana, lakini naomba majibu ya 10% hii ili mwishoni nipate nafasi ya kuweza kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema rendement ikiwa chini ya 10, wakulima wanapata hasara, 10% yenyewe hawapewi. Kwa hiyo, hawatafanya chochote, hawatavuna mua mpaka wapewe hii 10%. Nimesikia Mheshimiwa Venant na Mheshimiwa Prof. Muhongo hawataki kilimo cha mua. Sisi tunakitaka; Mheshimiwa Waziri leta pesa, leta ruzuku, lipa wakulima wangu waendelee kulima kilimo cha mua tuendelee kujitosheleza kwa sukari. Tunalima, sasa hivi tunavuna sukari tani 480,000 na tunataka tani 700,000. Lete mambo hayo Kilombero sisi tunataka kilimo cha mua, wao hawataki. Kwa hiyo, sisi tupatie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niongelee kokoa, amesema Mheshimiwa Kunambi nami ninataka kusisitiza. Kokoa kule kwetu inanawiri. Sasa lipo eneo linasemekana na wakulima na ni watu wazima; na kama hawa wakulima wamenidanganya wamekuja mpaka hapa, nimeenda mpaka kule, wanasema wana heka zaidi ya 200 zimezuiliwa na hifadhi, wamepigwa viboko. Naomba Mheshimiwa Waziri twende tukaone kama hawa wakulima wakweli ama sisi ni wakweli.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asenga, ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mzigo halmashauri, tunaomba Mheshimiwa Waziri ausaidie Msitu wa Kiogosi, Hifadhi ya Shamba la Kiogosi la Halmashauri ya Ifakara alisaidie liweze kulima kokoa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asenga, ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)