Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Samweli Xaday Hhayuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara ya Watanzania (Wizara ya Kilimo). Nataka tu nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, kwamba wakati nachangia bajeti ya 2023/2024 niliongea maeneo mahususi ambayo yanafaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji Wilaya ya Hanang. Nilitaja eneo la Duru pale Masakta, nikataja eneo la Getasam, Endagaw, Endasiwold, Qutesh, Nyamurah ambayo ipo katikati ya Bassotughang na Mara, nikataja Bwawa la Bassotughang, nikataja maeneo ya Endasak, eneo la Balang’dalalu ambapo maji yapo karibu lakini eneo la Mogitu ambalo lina maji mengi chini, nikataja na Ziwa Bassotu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili nimesema haya maeneo kwa maana ya kukumbushia yale niliyokuwa nimeyasema. Nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri ametuma wataalamu, wametembelea maeneo kadhaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini utaharakisha uwekezaji wa mifumo ya umwagiliaji kwenye maeneo hayo ili Wanahanang ambao kwa sasa sehemu kubwa wanategemea mvua ya Mwenyezi Mungu ili waweze kulima, waweze kutegemea umwagiliaji na waweze kulima zaidi ya mara moja kwa msimu kwa sababu ardhi ya Hanang sasa imekuwa finyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, ameanza kazi vizuri, naye na timu yake wanajitahidi na wanafanya kazi sawasawa. Yale ambayo nimewaomba wamefanya sehemu kubwa, namwomba sana aongeze kasi, Wanahanang wanamsubiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Mheshimiwa Waziri hapa Bungeni alishawahi kuahidi yale mashamba ambayo yako kwa wawekezaji ekari 30,000 angewarejeshea wananchi. Wanahanang wanasubiri hiyo ahadi.

Mheshimiwa Waziri, pia, Wanahanang wanakusubiri uwatembelee uende ukaongee nao. Wawekezaji waliowekeza kwenye ekari zaidi ya 42,000 mara nyingi wanakuja kwako wakileta siasa nyingi. Mwaka huu mashamba yao yamelimwa na wananchi wa Hanang na wamezalisha. Peleka jicho lako ukaone jinsi Wanahanang wanavyoweza kuzalisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo Shamba la Bassotu Plantation ambalo liko chini ya usimamizi wa halmashauri. Shamba lile likabidhi kwa halmashauri wawekeze pamoja na wananchi. Wakiwekeza pamoja na halmashauri, matunda utayaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wanahanang ni wachapakazi na wanajituma. Mheshimiwa Waziri, kete wataalamu tuzalishe kadri unavyotaka ili hatimaye Wanahanang tuzalishe. Pia, yale mashamba ya wawekezaji angalia namna ambavyo wale wawekezaji wanaweza kushirikiana na halmashauri ili yale maeneo yaweze kutumika vizuri. Tembelea Hanang, Wanahanang wanakusubiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ninataka niseme ni suala la kilimo cha ngano. Wakati Mheshimiwa Rais anafungua Bunge hili la Kumi na Mbili, alionyesha kwamba tunayo nakisi ya zaidi ya milioni moja. Mheshimiwa Waziri nimeangalia kwenye vitabu vyako kwamba 2022/2023 tulikuwa tumefikia tani 86,000 lakini 2023/2024 tani laki moja na zaidi, bado tuko chini sana.

Mheshimiwa Waziri, ninachoomba, ile kasi uliyokuja nayo Jimboni Hanang mwaka 2020, hebu uirudie ile ile angalau tuweze kuzalisha ngano zaidi ili wakulima wetu waweze kulisha nchi yetu badala ya kutegemea kuagiza ngano kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamsubiri Mheshimiwa Waziri Hanang. Naomba wakati anahitimisha angalau atenge muda kidogo aseme kwamba wananchi wa Hanang, wakulima wa Hanang wanamsubiri akaseme nao, wana issue naye kwenye suala la Stakabadhi Ghalani na wanapenda sana Stakabadhi Ghalani.

Mheshimiwa Waziri, nafahamu ulikuwa unatarajia nitasema hili, lakini nalisema kwa sababu sasa hivi ni wakati ambapo watu wanaandaa mazao. Watu ule mvuto wa fedha haujaja, nenda kaongee nao sasa. Peleka timu yako ya COPRA, peleka timu ya CPB wakawaelimishe wananchi mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ule wa fedha, kila mtu alichanganyikiwa na fedha, hakuna mtu anamsikiliza mwenzie. Twende tukaongee sasa ambapo fedha hazijawa karibu. Wanakushukuru wananchi wa Hanang…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Samweli, ahsante.

MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)